Ni sahihi kushiriki kila shindano la mtandaoni?
Kabala ya kushiriki shindano la mtandaoni (Challenge) ni vema ukatambua lengo lake, faida utakazopata na unatoa ujumbe gani kwa wanaokuzunguka.
- Kabla ya ushiriki michuano yoyote ya mtandaoni, ni vyema ukajiuliza kama itakufaidisha kwa namna yeyote ile.
- Pia unaweza kujiuliza kama haitakuacha na majuto miaka ijayo.
- Badala ya kuwa mtumwa wa mtandao, unaweza kufanya mambo mengine uwapo nyumbani.
Dar es Salaam. Kuanzia mtandao wa video za muda mfupi wa TikTok, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya kijamii, michuano au unaweza kuiita “challenge” kwa lugha iliyokuja na meli inazidi kupamba moto.
Kila ukiamka, utakuta kuna mchuano huu, kuna mchuano ule, huyu ana vuma kuliko huyu, huyu kafanya vizuri kuliko yule. Ni ushindani unaotapakaa mithili ya moto kwenye mbuga ya nyasi kavu.
Ipo michuano mingi iliyovuma na inayoendelea hata sasa ikiwa na “Hashtag” mbalimbali ikiwemo ya #dontrushchallenge na #fliptheswitchchallenge.
Huwezi kuzimaliza kwa kuzitaja na nyingi zimevuma baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona uliolazimu watu kukaa majumbani na hivyo kujikuta wakishiriki katika michuano hiyo ili kuepukana na hali ya upweke.
Hata hivyo, zipo challenge zingine ambazo zinaenda nje ya reli kwa maana ya kuwa hazina ulazima kushiriki hasa kwa kijana ambaye kesho yake bado haifahamu.
Usininukuu vibaya! Sikupangii maisha yako na jinsi ya kuishi na kutumia mwili wako lakini, yapo maswali ambayo unapaswa kujiuliza kabla hujaamua kushiriki kwenye michuano ambayo unaifungulia dunia kuona.
The best one 😍#DontRushChallenge
#TikTok
pic.twitter.com/UmxPlzWv3B— TikTokWorld (@tik_tok_world_) May 6, 2020
Jaribu kujiuliza maswali haya kabla ya kushiriki michuano hiyo:
1. Hautajutia ifikapo kesho?
Ni mara ngapi umewahi kupiga na kuweka mtandaoni picha ambazo umeishia kuzifuta mara baada ya kuzianika kwenye mtandao?
Wakati unawaza kujirekodi video ya kukata kiuno chako kwa wimbo wa “Okwonko” kwenye mtandao, ni bora ukawa na uhakika kuwa shindano hilo halisababisha majuto siku zijazo.
2. Ni kwa manufaa gani?
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes, Kennedy Mmari ameshauri wote wanaoshiriki kwenye michuano hii ni bora wakajiuliza kama kuna manufaa yoyote wanayopata.
Mmari ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa, ipo michuano yenye mlengo wa burudani na hata kuelimisha na huandaliwa kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii ikiwemo COVID-19.
“Sitaki kulaumu. Wanaweza kurudi nyuma na kusema “we can do better” (tunaweza kufanya kitu bora zaidi),” amesema Mmari ambaye ni mtaalam wa mitandao ya kijamii akiwashauri watu ambao huenda wameingia kwenye michuano hiyo kwa mkumbo.
Soma zaidi:
- Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
3. Kuna kitu chochote kitaongezeka kwako?
Ni wakati sasa wa kuachana na uteja wa kila jambo linaloingia kwenye jamii ya mtandaoni. Huenda kuna michuano imekupita mtandaoni lakini unaweza kwenda na kujionea michuano ya kuvua nguo mbele ya mpenzi wako akiwa anacheza michezo ya kidijitali (PS) na hata #shampoobottlechallenge ambayo ndiyo unaweza kubaki mdomo wazi.
Hivyo ni kusema, kama hauwezi kuongeza chochote kupitia michuano hiyo, haina haja ya wewe kushiriki maana inaweka baadhi ya mambo yako ambayo si vema kuyaonyesha mbele za watu.
Hata hivyo, wapo ambao wameshiriki kwenye michuano hiyo na kuishia kupata fursa fulani. Je wewe unaweza kufikia hapo?
4. Unamnufaisha nani?
Wakati mwingine unaweza kutumia nguvu nyingi kuwanufaisha watu wengine kuliko unavyojinufaisha mwenyewe.
Kabla ya kushiriki mchuano wa mtandao tafakari nani ananufaika na kwa nini?
Kwa wewe kuvaa nguo nusu utupu, au kufanya kitu nje ya maadili, wanaokuzunguka wanakuchukuliaje na wana lolote la kujifunza?
Ni kweli utapata “like” na “comments” nyingi kwa uhodari wako lakini ni sahihi kufanya ulichokifanya kwa jamii yako.
Zipo challenge ambazo ukishiriki zinasaidia kuleta amani na usalama kwenye jamii ikiwemo kuzuia mauaji ya kimbali. Picha|Mtandao.
Wakati mwingine challenge hutegemeana na tamaduni za watu fulani. Kabla hujaingia, tafakari kama katika tamaduni za kwenu ni sahihi kushiriki.
Khalila Mbowe amesema hana haja ya kushiriki kitu ambacho hakimongezei chochote.
“Kama mchuano unaniingia akilini, nitafanya lakini kama haunipatii sababu za kutosha kushiriki, nitautazama na jicho la kwanini,” amesema Khalila Mbowe mtumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, kama lengo ni kufurahi na kuepuka kuboreka uwapo nyumbani, kuna mambo mengi ya kufanya yakiwemo kuangalia filamu, kucheza na familia yako na kutengeneza marafiki wapya wenye faida mtandaoni.
Hadi muda mwingine, Kwaheri.