October 6, 2024

Kutana na shule ya mtandaoni inayofanya mapinduzi ya elimu Tanzania

Ni Shule ya mtandaoni inayoohitaji intaneti tu, kwa mafunzo mubashara kati ya mwalimu na mwanafunzi.

  • Ni programu tumishi ya SmartClass iliyogunduliwa na vijana watatu walioona fursa ya elimu ya mtandao mwaka 2018.
  • Ina wanafunzi zaidi ya 20,000 huku ikitoa nafasi za waalimu 5,000.
  • Jukwaa hilo linatoa nafasi ya kujifunza kila somo kwa ngazi ya msingi na sekondari.

Dar es Salaam. Ni ndoto ya kila mzazi kuona mtoto wake akifanya vizuri kielimu ili kuweza kufikia malengo ambayo mara nyingi ni kuwa na maisha mazuri mbeleni.

Ili kuhakikisha kuwa mtoto anapata elimu bora, wazazi wengi hulipa fedha kwa ajili ya masomo ya ziada (Tution) hasa kipindi cha likizo na jioni baada ya watoto kutoka shule.

Changamoto inayofanya masomo hayo ya ziada kushindwa kufikiwa na wengi, ni pamoja na kutokuwepo kila sehemu na hivyo kuweka uzio kwa wanafunzi hasa wenye umri mdogo kuvifikia.

Hiyo ndiyo changamoto ambayo iliwafanya wabunifu watatu kufikiria njia ambayo inaweza kuweka uwezekano wa wanafunzi kusoma kwa njia ya mtandao kwa gharama nafuu ilimradi wawe na intaneti.

Hapo ndipo lilipoibuka wazo la kutengeneza shule ya mtandaoni ya  SmartClass mwaka 2018. 

Baaada ya kusikia juu ya SmartClass nilitamani kufahamu wanachokifanya na wanawezaje kuacha alama yao katika sekta ya ellimu Tanzania. 

Kiu hiyo imenikutanisha na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Mipango, SmartClass Tanzania, Adam Duma (25) na haya ndiyo yalikuwa mazungumzo yetu.

Nukta: Nieleze kwa ufupi kuhusu SmartClass

Duma: SmartClass ni jukwaa la kiteknolojia linalowaunganisha walimu bora kabisa hapa Tanzania na wazazi pamoja na wanafunzi kwa ajili ya masomo ya mtandaoni yani masomo mubashara.

Hiyo ina maana kuwa mwalimu anaweza kumfundisha mwanafunzi somo analochagua kusoma huku mwanafunzi akiwa na nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa papo kwa papo.

Nukta: Hakuna ambalo limeanzia angani, Je SmartClass imeanzia wapi?

Duma: SmartClass ilianza mwishoni mwaka 2018, lakini baada ya kupata ufadhili kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) Ikaanza rasmi Januari 19, 2019. 

Wazo la awali la kuanzishwa kwa SmartClass lilikuwa ni kuangazia ni kwa namna gani teknolojia itawapatia Watanzania fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Afrika Kusini na duniani ili wajipatie kipato cha kumudu maisha ya kila siku.

Nukta: Mwitikio wa walimu ulikuwaje baada ya kuanzisha jukwaa hili linalowahusu kwa kiasi kikubwa?

Duma: Safari ilianza kwa kusajili walimu kwenye jukwaa lakini tulizingatia vigezo mbalimbali kwani siyo kila mtu aliyemaliza ualimu atafaa kuwa mwalimu kwetu.

Nukta: Tanzania ina walimu wengi sana. Nieleze mliwezaje kufanikiwa.

Duma:  Ubora wa mwalimu kwetu unategemea na vyeti vyake kuanzia ngazi ya sekondari hadi chuo kikuu kwa yale masomo anayotaka kufundisha.

Haiishii hapo, timu yetu ya taaluma watakagua uwezo wake pamoja ni nini refa wake wanasema juu yake na wakijiridhisha watapata kuridhia awe mwalimu kwenye SmartClass.

Mwaka 2019 pekee tulipata maombi zaidi ya 22,800. Watu wanataka kuwa walimu mpaka wa ngazi ya diploma ila 3,000 tu ndiyo walifanikiwa kujiunga kwa mwaka jana ambapo mpaka kufikia mwaka huu wapo walimu 5,000.

Nukta: walimu ni wengi sana kuliko hata shule inavyoweza kuajiri. Mnawalipaje au ni siri?

Duma: Hapana siyo siri. Kila mwalimu ana gharama zake lakini kiwango cha mfumo ni Sh3,000 kwa kiwango cha chini.

Pesa hiyo inafaa kwa kipindi cha saa moja na nusu na kunakuwa na makubaliano ya mwalimu na mzazi.

Mwanzo, SmartClass ilikuwa inaruhusu wazazi kuweka makubaliano ya muda na walimu ambapo walimu walikuwa wakienda majumbani nyakati za jioni na kuwafundisha wanafunzi wao.

Hata hivyo, kwa kipindi hicho, bado wazazi wengi walipendelea masomo ya ana kwa ana kuliko njia ya video. Wengine walikuwa wanatumia madarasa mtandaoni lakini haikuwa idadi kubwa kama madarasa ya ana kwa ana.

Wazazi wengi walipendelea masomo ya ana kwa ana kuliko njia ya video lakini kwa sasa masomo ya mtandao yameongezeka. Picha| Tovuti ya SmartClass.

Nukta: Kwa sasa hali ikoje hasa kwa kuzingatia wanafunzi wengi wapo nyumbani?

Duma: Ugonjwa wa Corona imesababisha wengi wao kuhamia mtandaoni. Idadi ya wanafunzi wa madarasa ya mtandaoni imekuwa mara 20 ya ile ya kwenda nyumbani kufundisha.

Hadi sasa, SmartClass ina wanafunzi zaidi ya 20,000 waliojisajili na kwa sasa mwalimu mmoja ana uwezo wa kufundisha hadi wanafunzi 50 kwa wakati mmoja. Uelewa wa wanafunzi unaridhisha na maswali wanayopewa wanayafanya vizuri.

Nukta: Tofauti ya SmartClass na majukwaa mengine ya elimu ni nini?

Duma: Zaidi ni uendeshaji. Wakati majukwaa mengine ya Afrika Mashariki yanatoa dhana za kujifunzia zikiwemo notsi na maswali kitu ambacho kinapelekea wanafunzi kukariri na siyo kuelewa kiundani zaidi.

Kwa upande wa jukwaa letu, tunawapa walimu nafasi ya kufundisha wanafunzi mahala popote walipo kwa madarasa mubashara na wanafunzi kuchagua walimu kwenye jukwaa hilo.

Madarasa hayo huja na gharama za ufundishaji zilizopo kwenye vifurushi ambavyo huwa kwenye mfumo wa ada inayojumuisha kila kitu zikiwemo gharama za usafiri kwa mzazi atakayechagua masomo ya ana kwa ana.

Nukta: Mzazi anawasiliana vipi na mwalimu?

Duma: Baada ya mzazi kujisajili kwenye mfumo wetu atachagua somo na  ngazi ya elimu.

Baada ya hapo mzazi  atachagua mfumo wa ufundishwaji yaani kama ni mtandaoni. Hatua nyingine ni kubonyeza kitufe cha “find tutor“ (tafuta mwalimu) na kisha ataona wasifu wa walimu wa somo hilo na mwisho, atachagua anaymfaa na atawasiliana naye kwa kufuata maelekezo na kisha kulipa na mtoto wake kuanza kusoma.

Kuna walimu wa ngazi ya msingi na sekondari na hutoza gharama za vifurushi vya saa moja, siku, wiki, mwezi na hata kwa “topic”(mada) moja.

Nukta: nani anayesimamia mawasiliano hayo?

Duma: Mlolongo wote wa makubaliano baina ya mwalimu na mzazi husimamiwa na SmartClass kwa ajili ya usalama.


Zinazohusiana


Nukta: kuna gharama za kujiunga na Smart Class?

Duma: Unachohitaji ni kifaa kinachoweza kukuunganisha na intaneti. 

Utatembelea  https://www.smartclass-tz.com/ na utafata taratibu nilizotoa awali. Usajiri ni bure. 

Nukta:SmartClass imetoa mchango gani katika sekta ya ajira? 

Duma: SmartClass imetoa ajira kwa watu zadi ya watu 100 wanaofanya kazi kama mawakala na ina timu ya watu nane wanaohakikisha mambo yote yanaenda sawa. 

Lengo ni kuwa na wakala 20,000 na ifikapo mwaka 2030 na kumfikia kila Mtanzania. 

Mimi na wenzangu wawili ndio tuliibuka na wazo hili ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa hilo Salvatory Kessy (28) na Mkurugenzi wa Teknolojia wa SmartClass Seraphin Kimaryo(28).

Nukta: Mna mpango gani kwa watu wasio na intaneti?

Duma: SmartClass inayo suluhu ya kuwafikia vijana wasiokuwa na interneti ambapo idadi yao ni zaidi ya asilimia 55 ya Watanzania lakini suluhu hiyo ina gharama kwa sababu inahitaji wawekezaji na wadhamini. Lengo hilo linaweza kufikiwa.

Endapo suluhu yetu itafanikiwa, itakuwa ya kwanza barani Afrika kwani njia yetu hii haijafanyika mpaka sasa kwa bara la Afrika ambapo ndiyo kuna shida ya intaneti.”

Hadi sasa, SmartClass imefikia mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mbeya, Kilimanjaro na Pwani. Mingine ni Mwanza na Dodoma na mwaka huu tumefungua tawi lingine nchini Kenya.

Natumaini umefahamu kwa undani kuhusu shule hiyo. Toa maoni yako katika mitandao yetu ya kijamii ili kuendelea kuinua elimu ya watoto wetu. Hadi wakati mwingine, endelea kusoma Nukta.