November 24, 2024

Italia mbioni kutumia app ya kufuatilia wagonjwa wa Corona

Italia ina mpango wa kutumia programu ya simu za mkononi inayoweza kufuatilia maambukizi ya kirusi cha corona, wakati ikijitayarisha kuondosha zuio la shughuli za kawaida za kimaisha mwezi ujao wa Mei.

  • Programu hiyo itakuwa na uwezo wa kuwasaidia watu kumtambua mwenye virusi vya COVID-19 waliyekaa naye karibu.
  • Programu hiyo itasaidia kuwapata wagonjwa kirahisi na kuwapatia matibabu.

Kwa mara ya kwanza, Italia ina mpango wa kutumia programu ya simu za mkononi inayoweza kufuatilia maambukizi ya kirusi cha corona, wakati ikijitayarisha kuondosha zuio la shughuli za kawaida za kimaisha mwezi ujao wa Mei. 

Programu hiyo itakuwa na uwezo wa kuwasaidia watu kumtambua mwenye virusi vya COVID-19 waliyekaa naye karibu. 

Programu hiyo itasaidia kuwapata wagonjwa kirahisi na kuwapatia matibabu, ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa ya Ulaya yaliyoathirika zaidi na janga hilo. 

Takwimu za Shirika Afya Duniani (WHO) za hadi jana Aprili 18, 2020 zinaeleza kuwa nchi hiyo imeripoti wagonjwa 182,816 wa Corona huku kati yao 19,130 wamefariki dunia. 

Duru za kimataifa zinaeleza kuwa Kamishna anayesimamia mapambano ya Corona wa Italia, Domenico Arcuri, alisaini sheria maalum Aprili 16, ambayo imetoa mkataba wa kuendesha programu hiyo kwa kampuni moja mjini Milan ya Bending Spoons.


Zinazohusiana


Umoja wa Ulaya (EU) ulipendekeza matumizi ya programu za simu za mikononi kama sehemu ya mpango wa kuzisaidia nchi kulegeza marufuku, ambazo zimeuporomosha uchumi kwenye umoja huo. 

Kwa mujibu wa sheria hiyo, programu hiyo haitaweka hadharani majina wala maeneo waliyo watu, lakini itaweza kufuatilia maambukizi popote yalipo kwa kutumia kifaa cha “bluetooth” kama inavyopendekezwa na EU.

Mataifa kama Israel na Korea Kusini yamekuwa yakitumia programu hizo ambazo zinawasaidia watu kujuwa ikiwa wamekaa karibu na mtu mwenye maambukizi ya kirusi cha corona.

Tangazo la Italia linakuja wiki chache baada ya kampuni za Apple na Google za Marekani kuweka wazi mipango yao ya kutengeneza programu ya simu ya kubaini wagonjwa wa ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani. 

Mpango huo utawezesha programu za simu watakazotengeneza zinazotumia mfumo endeshi ya Android na Apple kubadilishana taarifa muhimu.