November 24, 2024

Apps za usafiri zinavyochuana Tanzania

Huenda viti vya enzi vya wadau hao wa usafiri vikaota miba baada ya mdau mwingine kuingia kwenye tasnia hiyo ya usafiri.

  • Ni programu tumishi za simu za usafiri za Twende, Bolt na Uber.
  • Twende imeenda mbali inawawezesha wateja wake kulipa nauli kwa kutumia malipo kwa njia ya simu za mkononi.
  • Apps hizo pia zinakimbizana kutoa huduma bora kuwapata wateja wengi.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya sayansi na teknolojia yameendelea kubadili mtindo wa maisha wa binadamu kila siku huku ushindani wa masoko ukiendelea kuhakikisha huduma zinazotolea kwa msaada wa teknolojia zinazidi kuboreshwa.

Katika nyanja ya usafiri, awali watu walilazimika kuwa namba za madereva taxi na hata daftari la mawasiliano la simu la baadhi ya wadau kuja namba za madareva wa bodaboda.

Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni teknolojia imepunguza ulazima wa kufanya hivyo baada ya programu za usafiri kuanzishwa nchini zikiwemo Uber na Bolt (zamani taxify).

Hata hivyo, huenda viti vya enzi vya wadau hao wa usafiri vikaota miba baada ya mdau mwingine kuingia kwenye tasnia hiyo ya usafiri. 

Ni programu ya Twende App ambayo inapatikana kwenye maduka ya kupakua programu za simu zinazotumia mfumo endeshi wa Android yaani Play store.

Programu hiyo inamuwezesha mtu kuita taxi, bajaj na bodaboda popote alipo kwa kutumia simu na kupelekwa anakotaka. 

Programu hii kama zilivyo zingine zinatumia programu ya ramani na mahala ulipo (Location) kufanya kazi hivyo kuhitaji matumizi ya intaneti.

Licha ya kwamba kuna maelewano ya nauli baina ya dereva na abiria, kwa usafiri wa bajaji kianzio ni Sh1,500 kwa wanaotumia App ya Twende. Picha| Data collaborative for local impact.

Tofauti na huduma nyingine za usafiri mtandaoni ambazo tayari zimepanga bei, abiria anayetumia Twende anaweza kukubaliana gharama ya usafiri na dereva kabla ya kuanza safari. 

“Kama ukichukua usafiri wa gari la Twende, nauli utakayolipa mwisho wa safari itatokana na makubaliano mliyofanya mwanzo. Utalipa nauli kulingana na makubaliano yako na dereva wetu,” imesomeka sehemu ya taarifa iliyoandikwa kwenye mtandao wa Instagram wa programu hiyo.

Hata hivyo, wakati kampuni hiyo inasema kuwa bei ya usafiri ni kati ya dereva na abiria, Tayari imeweka nauli ya kianzio kwa kila aina ya usafiri.

Kwa usafiri wa bodaboda, nauli ya kianzio nia Sh1,000 huku usafiri wa bajaji ukianzia Sh1,500 na usafiri wa gari ukigharimu kiazio cha Sh3,000 huku ukipatikana kwa saa 24.


Zinazohusiana 


Twende App ambayo inashirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Tigo, hadi sasa inapatikana kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro huku tofauti na Uber na Bolt ikiwa ni uwezo wa kulipia safari zako kwa mfumo wa Tigo Pesa.

App ya uber na Bolt zinaruhusu malipo kwa njia ya pesa taslimu au unaweza kulipa kwa mfumo wa kadi ya malipo iliyounganishwa na benki. 

Hadi sasa, madereva zaidi ya 1,000 na abiria zaidi ya 50,000 wamepakua app hiyo kwenye duka la Playstore na wanaeleza kuwa ni rahisi kutumia.

Hata hivyo, app hiyo itaweza kuhimili ushindani wa kampuni za Uber na Bolt ambazo zimejiimarisha katika maeneo mbalimbali duniani?