Teknolojia kutunza taarifa za wagonjwa yapatikana Tanzania
Mfumo huo ambao ni programu tumishi ya simu (App) ya Afya Tek inasaidia wadau wa sekta ya afya kufanya maamuzi sahihi kupitia taarifa sahihi za wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya afya.
Mfumo huo unamsaidia Daktari kufuatilia maendeleo ya mgonjwa kwa kutumia simu ya mkononi. Picha|Fondation Botnar.
- Ni mfumo wa kidijitali unasaidia kutunza na kutumia kwa sa usahihi taarifa za wagonjwa kutoa tiba sahihi.
- Unatumia alama za vidole na simu za mkononi zinazotumia mfumo endeshi wa Android.
- Unapunguza mrundikano wa taarifa tofauti za wagonjwa kwenye vituo vya afya.
Dar es Salaam. Huenda upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa kwenye zahanati na vituo vya afya nchini Tanzania ukapatiwa ufumbuzi wa kudumu, baada ya wabunifu kutengeneza mfumo wa utunzaji kumbukumbu za matibabu kidijitali.
Mfumo huo ambao ni programu tumishi ya simu (App) ya Afya Tek inasaidia wadau wa sekta ya afya kufanya maamuzi sahihi kupitia taarifa sahihi za wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya afya.
Afya Tek ambayo inasimamiwa na shirika la D Tree International linaloshirikiana na mashirika mengine yakiwemo Apotheker na Simprints, inasaidia kuondoa mkanganyiko wa taarifa za wagonjwa na kuwezesha kuwa na taarifa endelevu ambazo zinaweza kutumia na watoa huduma mbalimbali katika shughuli za matibabu.
Akiuongelea mfumo huo, mtengenezaji wa programu za kompyuta kutoka shirika la D Tree International, Isaya Mollel amesema mbali na mifumo mingine ambayo inamuunganisha mgonjwa na vituo vya afya tu, Afya Tek unaunganisha vituo vya afya, watoa huduma, maduka ya dawa na mgonjwa au mtu anayetaka kupata matibabu.
“Sio watu wote huenda kwenye vituo vya afya, baadhi wala hawafiki kwenye vituo vya afya badala yake wanaishia kwenye maduka ya dawa. Mtu anaweza kuamka anakohoa na akaenda duka la dawa na akapata dawa bila hata ya kuenda hospitali,” amesema Mollel.
Kutokana na hali hiyo, amesema vituo vya afya vinakosa matibabu endelevu kwa mtu na hivyo kusababisha mrundikano wa taarifa za watu kiasi cha mtu mmoja kuwa na majarada zaidi ya matatu kwenye hospitali au zahanati moja.
Lakini Afya Tek ambayo ilianzishwa mwaka 2019 inaondoa changamoto hiyo kwa wahudumu wa afya kutumia taarifa moja ambayo ni sahihi katika maeneo tofauti tofauti.
Mfumo wa Afya Tek unaunganisha vituo vya afya, watoa huduma, maduka ya dawa na mgonjwa au mtu anayetaka kupata matibabu. Picha| Simprints.
Unavyofanya kazi
App hiyo ambayo ni rahisi kutumiwa na wafanyakazi wa afya ya jamii (CHW) inatumia simu zenye mfumo endeshi wa Android zikiwemo za Samsung, Techno na Huawei.
Kupitia mfumo huu, mfanyakazi wa afya anasajili taarifa za mgonjwa kwa alama za vidole na kumpatia namba ya kitambulisho chake ambapo kila atakapokwenda kutibiwa atazikuta taarifa zake na hatatakiwa kusajili tena.
Lakini ni njia rahisi ya kufuatilia maendeleo ya afya za wagonjwa kuliko kutegemea taarifa zilizopo kwenye makaratasi ambazo zinaweza kupotea.
Mollel ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa taarifa za wagonjwa ambazo zitakuwa zikihifadhiwa kwenye mfumo huo, zitawasaidia wadau wa afya (watoa maamuzi) kufanya maamuzi sahihi yakiwemo ya kuboresha huduma za afya katika maeneo yao.
“Kupitia Afta Tek, mtoa huduma anaweza kuona maendeleo ya mgonjwa na kama amefika eneo ambalo ameshauriwa kwenda.
“Kama CHW akimshauri kwenda duka la dawa, akiwasili, atapokea taarifa juu ya kuwasili kwake. Pia App ya Afya Tek itakuwa inatoa maelekezo juu ya dalili za magonjwa mbalimbali hivyo mtoa huduma anaweza kuona kuwa hili ni la hospitali moja kwa moja au duka la dawa,” amesema mdau huyo wa teknolojia.
Zinazohusiana
- Wanufaika wa bima ya afya waongezeka, Serikali ikijiandaa kutunga sheria mpya
- Watafiti wa afya watofautiana matumizi mashine za kukausha mikono
- Kutana na shangazi roboti wa Tanzania aliyepania kutokomeza mimba za utotoni
Kwa sasa mfumo huo umeanza kutumika katika zahanati na vituo vya afya katika Halmashauri ya mji wa Kibaha ambapo unalenga uwafikia watu 130,000 hasa wanawake, watoto na wajawazito ambao wako kwenye kundi linalohitaji uangalizi wa karibu wa afya zao.
Naye Mhandisi wa programu wa kampuni hiyo, Kassim Sheghembe amesema mfumo huo ni mkombozi wa sekta ya afya kwani mbali na kuondoa mrundikano wa taarifa kwenye vituo vya afya, mfumo huo unasaidia kurahisisha utoaji maamuzi kupitia takwimu na kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu.
Sheghembe amesema, dhamira kubwa ya Afya Tek ni kuepusha makosa madogo madogo ambayo yaliyokuwa yakifanyika awali yakiwemo ya kuchanganya dawa za wagonjwa na mrundikano wa taarifa za wagonjwa kwenye vituo vya afya na watoa huduma.
“Kwa kuanzisha mifumo ya afya ya kidijitali, kuna nafasi kubwa ya kufikiria upya namna huduma za afya zinaweza kuzifikia ngazi zote za huduma za afya, kuboresha upimaji, tiba na pia uwajibikaji kuwezesha huduma yenye heshima na inayowajali watu,” amesema.