November 24, 2024

Serikali yawataka wahisani kuangazia changamoto za ubunifu Tanzania

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha amewataka washirika wa maendeleo kuwekeza fedha kwa wabunifu wa teknolojia wenye mawazo yanayotekelezeka ambayo yanatatua changamoto za msingi zinazoikabilia Tanzania.

  • Wahisani watakiwa kuwekeza fedha kwa wabunifu wenye mawazo yanayotatua changamoto za jamii. 
  • Wadau wa ubunifu wamewasisitiza wabunifu kufikia changamoto za vijijini na siyo kubaki mjini pekee.
  • Hata hivyo, ubunifu isikaririke kuwa ni lazima utumie teknolojia.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha amewataka washirika wa maendeleo kuwekeza fedha kwa wabunifu wa teknolojia wenye mawazo yanayotekelezeka ambayo yanatatua changamoto za msingi zinazoikabilia Tanzania. 

Olenasha aliyekuwa akizungumza leo (Machi 9, 2020) katika uzinduzi wa Wiki Ya Ubunifu kwa mwaka 2020 jijini Dar es Salaam amesema hali hiyo imekuwa changamoto katika kukuza ubunifu Tanzania kwa sababu wabunifu hawafikiwi katika kiwango kinachohitajika. 

Amesema hata wabunifu wanaosaidiwa wengi wao ni wale ambao bidhaa ziko kwenye wazo bado hazijaenda sokoni, jambo linalochukua muda mrefu kutoa suluhisho la changamoto za jami.

“Tumefikia wabunifu wangapi? Nimesikia humu ndani wabunifu wote wanajuana, ni wale wale.Tunaweza kuwa tunarundikana kutoa uhisani kwa mbunifu mmoja. Wabunifu wapo wengi huko nje,” amesema Ole Nasha. 

Amesema ni vema wigo wa ubunifu Tanzania ukapanuliwa kuhahakikisha vijana wengi wenye mawazo ya kibunifu wanasaidiwa kuendeleza kazi zao ili kuwarahisishia maisha Watanzania kwa teknolojia rahisi.  

Wiki ya Ubunifu (#IW2020) imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ikiwemo Tume Ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Seedspace Dar es Salaam na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).

Pia ni jukwaa muhimu kwa wabunifu kuonyesha kazi zao hasa suluhisho za teknolojia zinazogusa sekta mbalimbali ili kuboresha maisha ya watu na kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuishi.


Soma zaidi:


Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi akizungumza katika uzinduzi huo amesema changamoto nyingine ni kuwa wabunifu wengi wanakwama kwasababu wanashindwa kuangalia changamoto za moja kwa moja zinazowakabili Watanzania. 

Akitolea mfano wa M-Pesa, Hendi amesema sababu za mfumo huo kufanikiwa ni kuwa uliangazia shida ambayo watu walikuwa nayo na siyo watu wa mjini tu hata wa vijijini.

Wadau mbalimbali wa ubunifu wamekubaliana na njia moja ambayo imeonekana kujirudia kwenye vinywa vyao ambayo ni kumulika kwa karibu changamoto halisi za wananchi na kuzitafutia suluhisho la teknolojia la kudumu. 

 Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Christina Musisi amesema ubinifu sasa unatambulika kama suluhisho kwa changamoto ambazo zinaikumba jamii na ili kuuweka ubunifu katika nafasi hiyo, wabunidu na wavumbuzi hawana budi kuangazia changamoto ambazo ni kiini cha maisha duni ya wananchi.

Amesema suluhisho za teknolojia ni muhimu zilenge kutengeneza fursa za ajira kwa vijana ili kuboresha maisha yao.