Facebook yazuia matangazo yanayopotosha tiba virusi vya Corona
Yasema baadhi ya matangazo hayo siyo ya kweli yanalenga kuwanufaisha wahalifu kibiashara.
- Yasema baadhi ya matangazo hayo siyo ya kweli yanalenga kuwanufaisha wahalifu kibiashara.
- Mbali ya matangazao hayo, itadhibiti taarifa za uzushi katika mtandao huo
- WHO yasema chanjo zaidi ya 20 dhidi ya virusi hivyo zinaandaliwa.
Wakati virusi vikiendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali duniani, kampuni ya teknolojia ya Marekani ya Facebook imezuia matangazo ya watu wanaotaka kujinufaisha kibiashara kwa kudai wana dawa ya kutibu ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, Facebook inatumia nyenzo za uthibitishaji habari (Fact Checking) ili kukabiliana na habari za uzushi na matangazo kuhusu virusi hivyo ambavyo chimbuko lake ni katika jimbo la Wuhan nchini China.
Wadhibiti maudhui wa mtandao huhakikisha kila bandiko (post) iliyowekwa yenye viashiria vya kupotosha kuhusu Corona huondolewa mara moja ili kuwalinda watumiaji wake na madhara zaidi ya mtandaoni.
Jarida la Business Insider la Australia likiinukuu taarifa ya Facebook limeeleza kuwa, “ kwa sasa tunatekeleza sera ya kuzuia matangazo yanayohusiana na virusi vya Corona ambayo yanatengeneza dhana ya dharura ikiwemo ukosefu wa vifaa au madai ya kutibu au kuzuia ugonjwa huo.”
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fecebook, Mark Zuckerberg. Mtandao huo umezuia matangazo yanayopotosha kuhusu kutibu virusi vya Corona. Picha|Mtandao.
Facebook kama yalivyo majukwaa mengine ya mtandaoni, inachukua hatua mbalimbali kufuatilia kwa karibu mijadala ya Corona, virusi ambavyo hadi jana (Februari 29, 2020) kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) vimeua watu 2,858 huku watu walioambukizwa wakifikia 83,652 katika nchi 51 duniani ikiwemo China ambayo ina maambukizi mengi.
Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo wanaingia katika makundi ya watu mtandaoni kuuza na kununua vifunika uso (face masks), jambo ambalo ni hatari na linawazuia wataalam wa afya kukabiliana na ugonjwa huo kikamilifu.
Kampuni nyingine za teknolojia pia zinakutana na changamoto ya watu kutumia corona kama sehemu ya kupiga pesa.
Mathalan, Jumanne Februari 25, 2020 mtandao wa Wired ulilipoti kuwa baadhi wauzaji katika duka la mtandaoni la Amazon walijaribu kupandisha bei za vifunika pua na mdogo kutoka bei iliyozoeleka.
Chanjo zaidi 20 dhidi ya Corona zaandaliwa
“Ongezeko la idadi ya wagonjwa sambamba na nchi zilizoathirika katika siku za karibuni bila shaka ni jambo linalotia hofu,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus akiongeza kuwa wafuatiliaji wa magonjwa wa WHO wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya sasa na wameongeza kiwango cha hatari ya ugonjwa huo duniani na kufikia kiwango cha juu kabisa.
Amesema kutokana na tangazo hilo la kiwango cha juu cha hatari, serikali zinapaswa kuelimisha umma, kupanua wigo wa ufuatiliaji, kusaka, na kutenga na kuhudumia kila mgonjwa na kufuatilia watu waliokuwa karibu na mgonjwa na kuwa na kuzingatia mfumo wa kiserikali na kijamii katika operesheni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Ghebreyesus amesema kwa sasa tayari zaidi ya aina 20 ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona (COVID-19) zinatengenezwa maeneo mbalimbali duniani, sambamba na dawa za tiba, na matokeo yanatarajiwa kutangazwa wiki chache zijazo.