Watumiaji huduma za posta Tanzania wapungua miaka miwili mfululizo
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2019 watumiaji wa huduma za posta walikuwa 346,684 kutoka 353,742 wa mwaka juzi.
- Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2019 watumiaji wa huduma za posta walikuwa 346,684 kutoka 353,742 wa mwaka juzi.
- Hata wakati, idadi ya watumiaji ikipungua, vifurushi vinavyosafirishwa na watoa huduma za posta wameongezeka.
Dar es Salaam. Licha ya kuonyesha matumaini ya ukuaji katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, idadi ya watumiaji huduma za posta nchini Tanzania imeendelea kushuka kwa miaka miwili mfululizo, jambo linaloibua maswali mengi kuhusu huduma hiyo katika kufanikisha mawasiliano ya shughuli mbalimbali za kijamii na kibiashara.
Huduma za Posta ni mfumo wa kusafirisha na kupokea barua na vifurushi kwa kutumia anuani maalum na stempu za malipo kutegemeana na ukubwa au uzito wa barua au kifurushi. Pia kutegemea kasi ya kufikisha ujumbe au mzigo sehemu husika.
Uchambuzi wa takwimu za robo ya mwisho ya mwaka 2019 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2019 watumiaji wa huduma za posta walikuwa 346,684 kutoka 353,742 wa mwaka juzi.
Hiyo ni sawa na kusema ndani ya mwaka mmoja, huduma hizo zimepoteza wateja 7,058 sawa asilimia 1.9 ya wateja waliokuwepo mwaka 2018.
Wateja wa wanaotumia huduma za posta inajumuisha watu, taasisi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi yanayofanya kazi nchini na kimataifa.
Hali hiyo inaondoa matumaini yaliyoanza kuonekana mwaka 2017 ambapo kulikuwa na watumiaji 445,160 baada ya kuongezeka kutoka watumiaji 381,376 wa mwaka 2017.
Miaka miwili iliyofuatia ya 2018 na 2019, idadi ya watumiaji ilishuka mfululizo kwa viwango tofauti.
Soma zaidi:
- Kama unafikiri mtandao unaweza kuua huduma za posta Tanzania, utasubiri sana
- Nini kimetokea kuporomoka kwa huduma za posta 2018?
Hata wakati idadi ya watumiaji ikipungua, watoa huduma za posta na vifurushi vinavyosafirishwa vimeongezeka.
Takwimu hizo zinaeleza kuwa idadi ya watoa huduma za posta nchini imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka 28 wa mwaka 2018 hadi 92 mwaka jana ambao hujumuisha mtoa huduma wa umma ambaye ni Shirika Posta Tanzania (TPC), watoa huduma za posta za kimataifa, Afrika Mashariki, katika mikoa na ndani ya miji.
Sambamba na hilo, vifurushi na mizigo iliyosafirishwa mwaka jana nayo imeongezeka jambo linalotoa mwanga kuwa huduma za posta zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao kwa kusaidiwa na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano na biashara ya mtandaoni (E-commerce)
Mathalan, vifurushi vilivyosafirishwa na TPC ndani na nje ya nchi mwaka jana vilikuwa milioni 12.2 kutoka milioni 10.8 vya mwaka juzi.
Mtaalam wa Usalama Mtandaoni kutoka kampuni ya Kabolik, Robert Matefu amewahi kuiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa matumizi ya huduma za posta hasa utumaji na upokeaji vifurushi yataendelea kuwepo kwa sababu ni njia rahisi ya watu kupokea mizigo wanayonunua kwenye maduka ya mtandaoni.
Shirika la Posta (TPC) linalomilikiwa na Serikali katika mikakati yake limeeleza kuwa linaendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo kuongeza wigo wa kuwafikia wateja wengi ambao wanatuma na kupokea vifurushi ndani na nje ya nchi.