November 24, 2024

Teknolojia inavyosaidia kupunguza athari za mafuta mwilini

Ni mashine inayosaidia kuepukana na hatari ya kupata magonjwa kama saratani na unene uliopitiliza.

  • Wabunifu wametengeneza mashine inayopika chakula kwa mafuta kidogo.
  • Inasaidia watu wanaoshindwa kujizuia kula vyakula vyenye mafuta mengi.
  • Inasaidia kuepukana na hatari ya kupata magonjwa kama saratani na unene uliopitiliza.

Dar es Salaam. Mara nyingi teknolojia huvumbuliwa ili kutatua changamoto katika jamii kwa lengo la kuboresha maisha ya watu.

Baadhi ya watu wamekuwa wakijaribu kukabiliana na changamoto ya matumizi ya mafuta mengi katika upikaji au uaandaaji wa chakula ili kukabiliana na ongezeko la mafuta mwilini.

Wataalam wa afya wanatahadharisha kuwa matumizi makubwa ya mafuta ya kupikia kwenye vyakula yanaweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata uzito uliopitiliza, magonjwa ikiwemo ya moyo, kiharusi na saratani.

Kama ni miongoni mwa watu wanaojaribu kupunguza matumizi makubwa ya mafuta katika uaandaaji chakula,basi wabunifu wametengeneza mashine maalum inayosaidia kuandaa chakula kwa kutumia kiwango kidogo cha mafuta ya kupikia.

Mashine hiyo i najulikana kama  “Air Fryer”, imetengenezwa na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Phillips  ambayo mtu anaweza kupika chakula chochote hata chipsi kwa kutumia kijiko kimoja cha mafuta na chakula kinakuwa tayari kwa ajili ya kutumiwa.

Inasaidia kupunguza matumizi makubwa ya mafuta kwenye kupikia. Picha | Mtandao.

Imeanza kutumika katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Uingereza na sasa inatumika Tanzania na inaweza kuwa njia sahihi ya kupunguza athari zitokanazo na mafuta mengi mwilini.

Chakula kinatakiwa kuwekwa kwenye chombo maalum cha mashine hiyo, kisha kuweka kijiko kimoja cha mafuta na kuchomekwa kwenye sokoti ya umeme tayari kwa maandalizi ya chakula hicho. 

Inarahisisha uandaji wa chakula na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa na athari kwa mazingira na afya ya binadamu. 

Air Fryer ni njia moja tu ya kupunguza matumizi makubwa ya mafuta. Njia nyingine ni kwa kupikia chakula kwa kuchemsha bila kuweka mafuta au kuweka mafuta kidogo n akuepuka kabisa kutumia mafuta ya wanyama. 

Mashine hii inawafaa zaidi watu wenye umeme katika nyumba zao, jambo linaloweza kuwaongezea bili ikiwa hawatatumia ipasavyo. Lakini watu vijijini ambao wanahitaji nishati mbadala, watabaki nyuma katika matumizi ya teknolojia hii hasa wale ambao hawana umeme.


Zinazohusiana:


Daktari wa mafunzo  tiba katika Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Cha Muhimbili (Muhas), Edrick Mwaipinga amesema kila mtu kutokana na mwili wake kuna kiwango stahiki cha mafuta kinachohitajika,  lakini visizidi vijiko viwili kwa siku. 

Amesema matumizi ya  teknolojia zinazodhibiti matumizi makubwa ya mafuta ni moja ya njia zinazoweza kutumika kuepukana na magonjwa yatokanayo na matumizi makubwa mafuta mwilini. 

“Hakuna ubaya kwenye matumizi ya vifaa hivyo. Ila tu vitumike kwa kiasi kwa sababu kila mtu ana kiwango chake cha mafuta kinachohitajika mwilini bila kuzidi kiasi cha vijiko viwili kwa siku hii ni kutokana na maumbile aliyonayo mtu,” amesema Edrick

Hata hivyo, mbali na jitihada za kupunguza mafuta katika upikaji ni vyema kuzingatia kanuni za afya ikiwemo ufanyaji wa mazoezi ili kupunguza uwezekano au hatari ya kupata magonjwa yanayosababishwa na matumizi makubwa ya mafuta au vyakula vyenye asili ya mafuta.