November 24, 2024

Samsung yazindua mashine inayosafisha nguo kwa mvuke

Ni mashine maalum ya kuondoa vumbi, wadudu kwenye nguo kwa kutumia hewa na mvuke wa joto na kuziacha zikiwa safi na kuvutia.

Mashine hiyo itasaidia kuokoa gharama za umeme na muda ambao watu wanatumia kufua nguo. Picha | Mtandao.


  • Imetengenezwa na kampuni ya Samsung na inaondoa vumbi, wadudu kwenye nguo kwa mvuke, joto hewa. 
  • Inatatua changamoto ya kufua nguo kwa muda mrefu na gharama ya umeme.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inaongeza ushindani wa bidhaa za kielektroniki duniani, kampuni ya Samsung ya nchini Korea Kusini inatarajia kuingiza sokoni mashine maalum ya kuondoa vumbi, wadudu kwenye nguo kwa kutumia hewa na mvuke na kuziacha zikiwa safi na kuvutia. 

Mashine hiyo inayojulikana kwa lugha ya kimombo “AirDresser” ilizinduliwa Januari 20, 2020 Soul, Korea ikiwa ni hatua ya kukidhi mahitaji ya watumiaji ambao wanataka vifaa vya nyumbani vyenye ufanisi wa kusafisha nguo zao ili zinukie vizuri na kuzitenga na wadudu.

“Samsung kwa mara nyingine inainua maisha ya kisasa kwa kubadilisha jinsi tunavyojali nguo zetu nyumbani, kuwapa watumiaji uhuru zaidi wa kutumia muda wao kufanya mambo wanayotaka kufanya,” amesema Jennifer Song, Makamu wa Rais wa Biashara ya Vifaa vya Dijitali wa Samsung.

Kwa kutumia kifaa cha “JetSteam” cha mashine hiyo yenye muundo wa jokofu  jembamba unaloweza kuning’iniza nguo zisizozidi tano kwa wakati mmoja, inatakasa mavazi ili kuondoa bakteria, virusi, na mzio (allergens). 

“Inapenyeza mvuke wa joto ndani ya kitambaa, kuvunja chembe chembe zinazosababisha harufu mbaya iliyosababishwa na jasho, tumbaku, na chakula, huku ikizuia harufu zisizofurahisha kujengeka ndani ya nguo,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Samsung. 

Teknolojia hiyo ya kujisafisha nguo inafanya kazi bila kuhitaji sabuni nyingi wala maji bali mchanganyiko wa joto, hewa, na mvuke. Inafanya kazi kwa utulivu bila kutoa kelele.  


Zinazohusiana:


Samsung inaeleza kuwa mashine hiyo itasaidia kuokoa gharama za umeme na muda ambao watu wanatumia kufua nguo zao kwa mikono au kwenye mashine na kuzianika juani. 

Mashine hiyo ina utofauti na mashine ya kufulia nguo ambapo kwenye mashine ya nguo inambidi mtu kuweka nguo kati ya nusu saa hadi saa 1. Lakini mashine hiyo ina uwezo wa kusafisha nguo kwa dakika zisizozidi 25 tofauti na mashine za kawaida.

Mashine hiyo itatumika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, japo Samsung bado hawajatoa tamko rasmi ya lini na bei itakayouzwa bidhaa hiyo kwajili ya matumizi na ya nyumbani.