Google yafungua fursa kwa wafanyabiashara 2020
Imeingia ubia na programu tumishi ya Pointy kuwasaidia wafanyabiashara kupata soko kwa njia ya mtandao.
- Imeingia ubia na programu tumishi ya Pointy kuwasaidia wafanyabiashara kupata soko kwa njia ya mtandao.
- Sasa bidhaa na huduma kupatikana kwa urahisi katika sehemu ya kitafutio cha viti cha Google.
- Huenda ikawasaidia wafanyabiashara kuongeza wigo wa soko na mapato.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Tanzania wenye mpango wa kuzipeleka biashara zao mtandaoni, sasa wana kila sababu ya kufurahi baada ya kampuni ya Google kuwafungulia fursa ya kutafuta soko la bidhaa na huduma zao kwa haraka na urahisi.
Kampuni hiyo ya Marekani imeingia ubia na programu tumishi ya Pointy ya Uingereza, inayomuwezesha mfanyabiashara kuweka bidhaa zake mtandaoni na kupewa kipaumbele katika sehemu ya kutafutia cha vitu (browser) cha Google.
Programu hiyo inarahisisha upatikanaji wa haraka wa bidhaa au huduma katika mtandao wa Google ambao umekuwa ukitumiwa na wafanyabiashara kujitangaza mtandaoni.
Ili kutumia fursa hiyo, mfanyabiashara anatakiwa kupakua programu tumishi ya Pointy, kisha kuweka bidhaa zake katika kipengele kinachoonyesha bidhaa mpya zilizopo sokoni kinachosimamiwa na Google, na kupata soko la watu watakaokuwa wanaotafuta bidhaa hiyo kwenye Google.
Pia itasaidia shughuli mbalimbali za kuendesha biashara zikiwemo utunzaji wa taarifa, ufanyaji wa mahesabu na tathmini ya mwenendo wa biashara kwa ujumla.
Hata hivyo, Google bado hawajabainisha siku rasmi mfumo huo utakapoanza kufanya kazi na taratibu wanazotakiwa kufuata wafanyabiashara ili kunadi bidhaa zao mtandaoni.