Startups sita zilizoboresha maisha ya Watanzania 2019
Zimewekeza katika kutumia teknolojia ili kuboresha maisha ya wananchi na kujipatia umaarufu ndani na nje ya Tanzania.
- Ni kampuni zinazochipukia katika matumizi ya teknolojia kugusa maisha ya watu.
- Zimekuwa mstari wa mbele kuibua njia za kisasa kutatua changamoto za jamii.
- Miongoni mwa kampouni hizo ni Nukta Afrika, Viamo na Drone Wings.
Dar es Salaam. Katika safari ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2020, zipo sababu lukuki za kutambua mchango wa kampuni zinazochipukia (Startups) zinazotumia teknolojia zilizogusa maisha ya Watanzania.
Tanzania imekuwa na vijana mahiri katika kuvumbua na kuibua suluhu za teknolojia ili kuboresha maisha ya jamii zinazowazunguka na kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.
Katika uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz wa startups mbalimbali zinazotumia teknolojia kurahisisha na kuboresha maisha ya watu, tunakuletea baadhi ya kampuni hizo ambazo zilifanikiwa kufanya vizuri mwaka 2019:
Nukta Africa
Nukta Africa ni kampuni ya teknolojia na habari iliyojikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na takwimu ili kuyawezesha mashirika, kammpuni pamoja na watu katika maeneo mbalimbali kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za maendeleo.
Pia inamiliki tovuti ya habari ya www.nukta.co.tz na hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu na matumizi ya mifumo dijitali katika kuzalisha habari.
Kwa mwaka 2019, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali likiwemo shirika lisilo la kiserikali la Internews wamefanikiwa kutoa mafunzo ya uandishi wa habari za takwimu (data journalism) na uthibitishaji habari (Fact Checking) kwa wanahabari zaidi ya 60.
Mafunzo hayo yamesaidia yamewawezesha wanahabari hao kuzalisha habari kwa ubora wa hali ya juu na zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na kwa vyombo habari husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen akifundisha wanahabari katika darasa maalum la wanahabari khusu nishati jadidifu lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Hivos Afrika Mashariki (Hivos East Africa) na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET). Picha | Nukta Africa.
Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni kuchaguliwa kuingia katika programu ya kampuni ya Marekani ya Google kupitia mpango wa “Google News Initiative G Suite” unaolenga kuziwezesha kampuni za habari duniani zinazochipukia kuongeza ufanisi wa utendaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Kwa sasa, kampuni hiyo inayosimamiwa na vijana wa Tanzania na yenye makao yake jijini Dar es Salaam, inashirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Hivos Afrika Mashariki (Hivos East Africa) na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kutekeleza mradi wa mafunzo maalum ya miezi sita ya wanahabari kwa vitendo katika masuala ya nishati jadidifu (Renewable energy reporting).
Drone Wings
Drone wings ni kampuni inayotumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones) katika kutoa mafunzo, kukusanya data na kufanya uchambuzi wa njia sahihi za kusimamia mazingira na kutatua changamoto za jamii kwa ujumla wake.
Kampuni hiyo, imekuwa ikitumia teknolojia kutoa huduma na bidhaa ili kutatua changamoto za jamii. Moja ya kazi kubwa ya startup hiyo ni kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika upimaji wa ardhi zao ili zitumike kwa usahihi katika shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo.
Licha ya kampuni hiyo kuwa changa, imefanikiwa kuwa moja ya kampuni za mwaka 2019 zilizochaguliwa kuingia katika shindano la dunia la Seedstars World, linaloendeshwa na kampuni ya ujasiriamali wa teknolojia na uwekezaji ya Seedstars ya nchini Switzerland ambayo ina matawi katika majiji mbalimbali duniani likiwemo Dar es Salaam.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua.
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018.
- “Startups” za Tanzania zapewa somo la uwazi, uwajibikaji kuvutia mitaji ya uwekezaji.
Summit Point
Ni programu tumishi ya simu inayoendeshwa na kampuni ya Bluefin Solution Limited inayotumika kuwezesha mipango ya kuendesha mikutano, matamasha na maonyesho katika mashirika na makampuni mbalimbali nchini.
Programu hiyo inayasaidia mashirika mbalimbali kupunguza gharama za kutafuta kumbi na sehemu za kisasa za mikutano au maonyesho. Lakini pia inapunguza matumizi ya kuchapisha agenda za vikao, vipeperushi na majarida kwa ajili kutangaza tukio husika.
Imekuwa rafiki wa mazingira kwa sababu inahamasisha mashirika na makampuni kutumia mifumo ya kidijitali iliyo salama na kuachana na matumizi ya makaratasi ambayo yamekuwa yakichochea ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.
Imefanikiwa kuendesha mikutano mingi ikiwemo mkutano wa mawakili wa Chama Cha Mawakili cha Tanganyika (TLS) mwaka jana, uliofanyika kwa urahisi na ufanisi mkubwa kwa sababu ya teknolojia ya simu iliyotumika katika uendeshaji wake.
Mkutano wa Mawakili uliofanyika jijini Arusha mwaka 2019 ambao Summit Point ulitoa huduma yake ya kuuendesha kidijitali. Picha| Bluefin Solution Limited. Picha| Summit Point.
Toolboksi
Ni tovuti maalum ambayo imekuwa nyenzo muhimu mwaka 2019 kuwaunganisha vijana wa rika tofauti wenye ujuzi na stadi za maisha kama uselamala, ufundi ujenzi, magari, vifaa vya umeme, utunzaji wa bustani, nyumba na fursa mbalimbali za ufundi zilizopo katika jamii.
Tovuti hiyo, iliyobuniwa na kuendeshwa na kampuni ya teknolojia ya Toolboksi Limited ya Tanzania, ni jukwaa linalowasaidia vijana waliojiajiri kuwafikia watu na taasisi zenye uhitaji wa kutengenezewa au kukarabatiwa vifaa au kitu chochote cha ofisini au nyumbani kinachosaidia shughuli zingine zifanyike.
Toolboksi inafanya kazi na mashirika na taasisi zinazowajibika moja kwa moja katika kuendeleza ujuzi na ufundi stadi kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), taasisi ya Digital Opportunity Trust (DOT) na kampuni ya ujenzi ya JINGU.
Mwaka jana, ilitangazwa kunyakua tuzo ya kampuni bora inayochipukia yenye tija kwa jamii (Best Social Impact Startup) nchini Afrika Kusini kupitia huduma zake wanazozitoa kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia stadi za maisha.
Moja ya kibarua kigumu kampuni hiyo changa inakabiliana nacho mwaka huu wa 2020 ni kuhakikisha inakamilisha programu tumishi (App) ya huduma hiyo kwa kuwa sehemu kubwa ya watumiaji wa huduma za intaneti wanatumia simu za mkononi kupata huduma mbalimbali.
Jenga Hub
Ni mradi unaosimamiwa na taasisi ya NengestiSumari Foundation, ambao unaotoa fursa na jukwaa kwa watoto kujifunza zana na maarifa muhimu ya teknolojia yaliyo na mchango mkubwa katika kuwawezesha kufanikiwa katika elimu.
Mradi huo ulioasisiwa na aliyewahi kuwa mlimbwende wa Tanzania mwaka 2005, Nancy Sumari siyo tu unatoa mafunzo bali unawawesha watoto kuwa wabunifu ili kutafuta njia mbalimbali za kidijitali zinazoweza kutumika katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowazunguka.
Jenga Hub kama jukwaa muhimu limefanikiwa kutoa mchango wake kwa jamii kwani imeweza kuwajengea watoto wa jiji la Dar es Salaam, ujuzi wa namna ya kutumia teknolojia wakiwa mashuleni na hata nyumbani na kuwawezesha kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano..
Pamoja na mafanikio hayo, taasisi hiyo ilifanikiwa kuendesha semina ya watoto iitwayo Global Children’s Designathon mwaka 2017 jijini Dar es Salaam, iliyokuwa na lengo kuu la kuwafundisha watoto namna ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
Moja ya kazi ya Jenga Hub ni kuwawezesha watoto wa umri kati ya miaka 7 hadi 12 kuwa wabunifu hasa kuvumbua njia za teknolojia zitakazotatua changamoto zilizopo kwenye jamii. Picha|Mtandao.
Viamo
Hii ni kampuni inayohusisha matumizi ya teknolojia rahisi na nafuu katika kukusanya na kusambaza takwimu kwa ajili ya huduma za umma kupitia matumizi ya simu za mkononi.
Kampuni hiyo iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, inaunganisha mashirika na watu binafsi wanaotumia teknolojia za kidigitali katika kufanya maamuzi ya maisha binafsi, afya na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali, mashirika ya kijamii na biashara mbalimbali.
Inatumia teknolojia ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu (SMS) na ujumbe wa sauti (IVR, Interactive Voice Response) ili kuwafikishia taarifa sahihi watu mbalimbali wa vijini na mjini kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi yahusuyo maisha yao.
Viamo imefanikia kuyafikia masoko zaidi ya 20 katika nchi za Afrika Mashariki na bara la Asia ambapo kwa sasa inafiwakia takribani watu 100,000 kwa siku.
Tumeingia mwaka 2020, kampuni hizi zitaendelea kufanya vizuri na kuibua teknolojia mpya kuboresha bidhaa na huduma zao? Huenda zikaibuka startups zingine zikiibuka na kutoa ushindani utakaosadia kuboresha maisha ya watu kwa kutumia teknolojia