November 24, 2024

UN yatoa mwelekeo kuziba pengo la migawanyiko mtandaoni

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema teknolojia ya dijitali ndiyo inayounda dunia hivi sasa na inakwenda kwa kasi isiyo ya kawaida hivyo kila mtu katika dunia anapaswa kwenda na kasi hiyo ili kufaidika na fursa zinazoambatana nayo

  • Amezitaka nchi kufanya kazi kwa pamoja ili kuziba pengo hilo.
  • Wadau zikiwemo Serikali zimeshauriwa kwenda sambamba na kasi ya teknolojia ya dijitali.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema teknolojia ya dijitali ndiyo inayounda dunia hivi sasa na inakwenda kwa kasi isiyo ya kawaida hivyo kila mtu katika dunia anapaswa kwenda na kasi hiyo ili kufaidika na fursa zinazoambatana nayo.

Akizungumza katika kongamano la kimataifa la udhibiti wa masuala ya intaneti Ujerumani jana (Novemba 26, 2019) nchini Ujerumani, Guterres amesema fursa ya upataji wa mtandao wa bure na wazi iko katika hatari kwa sababu hakuna juhudi za pamoja kuondoa mgawanyiko wa kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

“Lakini hili linaweza kubadilika. Na kuonyesha ni jinsi gani tunaweza kushirikiana mustakabali wa kidijitali kwa pamoja , vyema na kwa matarajio yetu sote,” amesema Guaterres.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UN, Katibu Mkuu huyo ameonya kuwa, endapo nchi hazitofanya kazi kwa pamoja kushughulikia pengo la fursa za kidijitali pamoja na migawanyiko yote ya kijamii na kisiasa inayochangiwa na pengo hilo, kizazi cha sasa kitasambaratisha ahadi ya awali ya intaneti.


Soma zaidi: 


Akianisha jukumu kubwa la intaneti katika kufikia mustakabali ulio sawa amesema, “kuwaunganisha watu wote duniani na mtandao wa intaneti ifikapo 2030 inapaswa kuwa kipaumbele chetu cha pamoja, siyo tu kwa ajili ya maendeleo endelevu bali pia kwa usawa wa kijinsia.”

Amesema siyo tu tunajenga kuta zilizo bayana zinazotenganisha watu lakini pia kuna hulka ya kujenga kuta zisizoonekana kwenye mtandao ambazo pia zinawatenga watu, na kuongeza kuwa  suluhu pekee ya janga hili ni mustakbali wa dunia moja, intaneti moja na mtazamo mmoja.

Aidha, amesema intaneti inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu sana kwa kufanya yaliyo mema, lakini  inaweza kuwa ni nyenzo inayoweza kutumika katika mambo mabaya.