October 6, 2024

Uber yafanya mabadiliko makubwa kumaliza 2019

Imeboresha App yake ili kumsaidia msafiri kufahamu kwa urahisi gari aliloita kulingana na rangi aliyopewa wakati anaita usafiri kwenye simu yake.

  • Imeboresha App yake ili kumsaidia msafiri kufahamu kwa urahisi gari aliloita kulingana na rangi aliyopewa wakati anaita usafiri kwenye simu yake. 
  • Pia itamkumbusha mteja kuvaa mkanda wa siti akiwa kwenye usafiri wa uber, kufunga milango vizuri pamoja na kujua safari yake inapokuwa imeisha yaani kufika anapokwenda.

Dar es Salaam. Kampuni ya usafiri mtandaoni ya Uber wamekuja kivingine baada ya kuifanyia mabadiliko makubwa programu yake tumishi ikiwemo kumsaidia msafiri kufahamu kwa urahisi gari aliloita kulingana na rangi aliyopewa wakati anaita usafiri kwenye simu yake. 

Uber ni miongoni mwa kampuni nyingi zinazotoa huduma za uchukuzi duniani kwa watumiaji kuomba taxi kwa kutumia programu ya simu (App) huku kila kitu katika mchakato wa kukodi taxi kinafanywa na app.

Teknolojia au mabadiliko hayo yanakwenda kwa jina la Beacon 2.0 na itakuwa inafanya kazi kwa rangi maalum aliyoonyeshwa mteja wakati anaomba taxi kuonekana katika kioo cha simu yake. 

Itawasaidia wateja kujua usafiri upi wanatakiwa kupanda kwenye mkusanyiko wa magari mengi yanayoweza kumchanganya akiwa anasubiri gari.

Mbali na uwezo wa kutambua gari sahihi kwa mteja, teknolojia hiyo itakuwa na uwezo wa kumkumbusha mteja kuvaa mkanda wa siti akiwa kwenye usafiri wa uber, kufunga milango vizuri pamoja na kujua safari yake inapokuwa imeisha yaani kufika anapokwenda.

Mabadiliko hayo yanategemea kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi Novemba katika baadhi ya miji na wilaya nchini Marekani kama Chicago, Denver, Las Vegas na  Washington DC na baadaye kuendelea katika nchi nyingine duniani.


Zinazohusiana:


Mabadiliko hayo yatawaondolea wateja wa Uber, tatizo la kuchanganya magari na kutolewana na madereva wakati wakitumia usafiri huo.

Minja Augustine ni mmoja ya madereva waliojiunga na Uber anaefanya kazi hiyo kwa takriban mwaka mmoja, amesema mabadiliko hayo ni muhimu kwa sababu yatawarahisishia wakati wakitimiza majukumu yao ya kuwasafirisha watu katika maeneo mbalimbali.

“Nimeshawahi kubeba mteja ambae aliita Uber nyingine bila kujua kwa sababu alikuwa anaongea na simu alipokuwa anapanda, mfumo huu utasaidia sana kwani inampa mteja uhakika wa usafiri alioita kwa hali yoyote,” amesema Minja ambaye anafanya shughuli zake Jijini Dar es Salaam.

Mabadiliko hayo ni muendelezo wa kampuni hiyo kujiboresha ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wake kote duniani na kuendelea kutoa ushindani kwa kampuni zingine zinazotoa huduma hiyo kama Bolt.