October 6, 2024

Ramani ya mtandaoni yazinduliwa kupambana na saratani duniani

Ni kitabu cha ramani ya saratani kinachompatia msomaji hali ya saratani kwa kila nchi, sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa.

  • Ni kitabu cha ramani ya saratani kinachompatia msomaji hali ya saratani kwa kila nchi, sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa.
  • Msomaji anaweza kupakua ramani, taarifa na ujumbe kwa njia ya mtandao.
  •  Ramani hiyo inakupatia uwezo wa kulinganisha hali ya saratani katika nchi mbalimbali duniani. 

Dar es Salaam. Huenda kuzinduliwa kwa toleo la tatu la tatu la kitabu cha ramani kinachoonesha hali ya saratani duniani, kutasaidia na kuongeza kasi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupambana na kuutokomeza ugonjwa huo. 

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa saratani (IARC) na wadau wake wamezindua toleo la tatu la kitabu hicho juzi (Oktoba 16, 2019) kando ya mkutano wa kimataifa wa viongozi walio kwenye harakati dhidi ya saratani huko Astana, Kazakhstan.

Kitabu hicho kilichopatiwa jina la “Upataji huduma huchochea maendeleo”, kinampatia msomaji hali ya saratani kwa kila nchi, sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na ugonjwa huo hatari.

Msomaji anaweza kupakua ramani, taarifa na ujumbe kwa njia ya mtandao kuhusu vichochezi vya ugonjwa huo katika kila eneo la dunia na hatua ambazo Taifa fulani limechukua hatua kutokomeza.

Walengwa, kwa mujibu wa IARC ambayo ni taasisi tanzu ya shirika la afya duniani (WHO) ni serikali, mashirika ya afya ya umma, watunga sera pamoja na wagonjwa na wahanga wa saratani na umma mzima kwa ujumla.

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN), Mkurugenzi Mkuu wa IARC, Dk Elisabete Weiderpass akizungumzia ramani hiyo ya ugonjwa wa saratani duniani amesema inampatia mtu kujua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo kuanzia hatua kuu zinazohitaji ushirikiano wa dhati baina ya mifumo ya afya na ugonjwa wenyewe. 

“Ni chapisho kubwa lenye vielelezo tosha vya picha vinavyokupatia tathmini na kuelezea simulizi ya manufaa ya kujizuia na saratani na kuzuia tofauti za maeneo yenye ugonjwa huo, kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo endelevu,” amesema Dk Weiderpass. 

Saratani zinazowatesa zaidi watu wengi ni pamoja na ile ya mapafu, matiti, shingo ya kizazi na utumbo mpana ambapo matokeo yanatoafutiana kwa kuangalia chanzo, eneo, aina, sababu za kuenea na hata udhibiti wa ugonjwa huo.


Zinazohusiana:


Hali ya saratani Afrika Mashariki

Kwa kuangazia vigezo vya vichochezi, mzigo wa saratani na hatua zinazochukuliwa, ramani hiyo inakupatia uwezo wa kulinganisha nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, ulinganifu wa vichochezi katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda, uvutaji sigara miongoni mwa wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea umeshika kasi zaidi Kenya kwa asilimia 20.2 ukifuatiwa na Tanzania kwa asilimia 19.9. 

Hata hivyo suala la uzito uliopitiliza miongoni mwa wanawake kama kichochezi cha saratani limeshika kasi zaidi Tanzania kwa asilimia 25.8 ikifuatiwa na Kenya kwa asilimia 25.5.

Ni kitabu cha ramani ya saratani kinachompatia msomaji hali ya saratani kwa kila nchi, sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa. Picha|UN.

Kwa upande wa mzigo wa saratani, tezi dume inaongoza kwa wanaume katika nchi zote nne ilhali kwa wanawake ni saratani ya kizazi.

Mataifa yote manne yametia saini mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku, (FCTC), lakini bado kuna changamoto ya kuwepo kwa lebo dhahiri kwenye pakiti za sigara kuonya watu juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku.

Hata hivyo nchi zote nne ziko mstari wa mbele kupatia chanjo wananchi wake dhidi ya homa ya ini aina ya “Hepatitis B”, ambapo Rwanda inaongoza kwa asilimia 98, ikifuatiwa na Tanzania asilimia 92, Kenya asilimia 78 na Uganda asilimia 78.