October 6, 2024

Youtube kushiriki Uchaguzi Mkuu 2020

Imewatengenezea jukwaa maalum wagombea wa nafasi mbalimbali ili kunadi sera zao kwa wananchi.

  • Imewatengenezea jukwaa maalum wagombea wa nafasi mbalimbali ili kunadi sera zao kwa wananchi.
  • Wagombea hao watatumia kifaa maalum kupeperusha matangazo yao kwa watu wanaowahitaji mtandaoni.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wanasiasa wanaweza kutumia vizuri majukwaa ya mtandaoni kujinadi kwa sera zao ili kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.

Ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya wanasiasa, mtandao wa YouTube imeanzisha kifaa maalum cha “Instant Reserve” mahususi kwa wagombea kunadi sera kwa wapiga kura katika maeneo yao. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa kifaa hicho kitawawezesha wanasiasa kupanga mbinu zitakazoendesha kampeni zao na kuwapa nafasi ya kunadi sera zao kupitia mtandao huo. 

Youtube imeona haja na umuhimu wa kuwafikia wanasiasa mbalimbali ulimwenguni kutokana na hamasa iliyopo katika mitandao ya kijamii na teknolojia kwa ujumla.

 Hii itasaidia wagombea kufikia watu wengi kwa muda uliowekwa kwajili ya kampeni kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Huduma hiyo itakuwa wazi kuanzia Novemba 15, 2019 ambapo wagombea au wanasiasa watakaotaka nafasi ya kunadi sera zao kupitia mtandao huo, watatakiwa kununua nafasi (Space) katika mtandao huo kuwafikia watu wengi ndani ya muda wote wa kampeni.

Fursa hii ni muhimu kwa wagombea ulimwenguni kutumia teknolojia katika kuhakikisha wanatimiza malengo yao na kufanikisha waliyopanga ndani ya muda huo wa uchaguzi hasa katika kipindi cha kampeni.

Hata hivyo, katika kufuatia vigezo na masharti, YouTtube wametoa mfumo wa namna matangazo hayo yanatakiwa kuwa pindi yakiwekwa katika mtandao kwaajili ya kufikia wananchi.

Huenda hatua hiyo ikawasaidia wanasiasa kuwafikia watu wanaotumia mtandao na ambao wanashindwa kuhudhuria mikutano ya kampeni.