Wabuni programu ya simu inyoendesha mikutano kidijitali
Inawezesha utekelezaji wa mipango ya kuendesha mikutano, matamasha na maonyesho katika mashirika na makampuni mbalimbali nchini kwa njia ya mtandao.
- Inawezesha utekelezaji wa mipango ya kuendesha mikutano, matamasha na maonyesho katika mashirika na makampuni mbalimbali nchini kwa njia ya mtandao.
- Inapunguza gharama za uchapaji, vipeperushi na matangazo ya kawaida.
- Ni rafiki wa mazingira kwa sababu inasaidia kupunguza ukataji wa miti.
Dar es Salaam. Kama bado unawaza ni jinsi gani utaendesha vikao, mikutano au makongamano kwa njia iliyo rahisi na yenye ufanisi, basi huna haja ya kuhofia maana teknolojia inakupa kila kitu.
Kampuni ya Bluefin Solution Limited inayosimamiwa na vijana wa Tanzania wamebuni programu tumishi ya simu ya Summit Point inayotumika kuwezesha mipango ya kuendesha mikutano, matamasha na maonyesho katika mashirika na makampuni mbalimbali nchini.
Programu hiyo inawasaidia waandaji wa mikutano kuratibu na kutekeleza shughuli zao mtandaoni bila ya kutumia muda mwingi kuzunguka ili kuweka mambo sawa.
Summit Point inayasaidia mashirika mbalimbali kupunguza gharama za kutafuta kumbi na sehemu za kisasa katika zamikutano au maonyesho. Lakini pia inapunguza matumizi ya kuchapisha agenda za vikao, vipeperushi na majarida kwa ajili kutangaza tukio husika.
Pia ni rafiki wa mazingira kwa sababu inahamasisha mashirika na makampuni kutumia mifumo ya kidijitali iliyo salama na kuachana na matumizi ya karatasi ambayo yamekuwa yakichochea ukataji wa miti.
Zinazohusiana
- Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
- Apps za elimu zitakazowasaidia wanafunzi 2019
Mratibu wa Program hiyo, Chris Bwemo ameiambia www.nukta.co.tz kuwa programu hiyo inatatua changamoto ya kuingia gharama kubwa katika kuratibu mikutano, maonyesho na uchapishaji wa majarida yanayotumika katika mikutano kwani kwa kutumia programu hiyo hakuna haja ya kuingia gharama zote hizo.
“Kwa kutumia programu hii, issue ya gharama za kuendesha mikutano na printing (uchapishaji)ya ratiba na vipeperushi katika event (matukio) inabaki kuwa historia kwani kila kitu kinafanyika ndani ya App,” amesema Bwemo
Utofauti wa programu hiyo na nyingine tumishi ni kwamba, ni ya kwanza kuanzishwa na kutumika nchini Tanzania na malengo ya mbeleni ni kuwa programu itakayotumika katika mikutano ya kimataifa kwani haina kizuizi juu ya matumizi yake inaweza kutumika popote.
Mkutano wa Mawakili uliofanyika jijini Arusha hivi karibuni ambao Summit Point ulitoa huduma yake ya kuuendesha kidijitali. Picha| Bluefin Solution Limited.
Bwemo amesema imeshaendesha mikutano mingi ikiwemo mkutano wa mawakili uliofanyika Arusha (Tanganyika Law Society) mwaka huu, ulifanyika kwa urahisi na ufanisi mkubwa kwa sababu ya teknolojia ya simu iliyotumika katika uendeshaji wake.
Ili kutumia programu hiyo, unaweza kupakua katika simu zote za Android na iOS kupitia duka la mtandaoni la Play store.
Program hiyo imelenga kusogea mbele huduma zake kwa kuingia ubia na makampuni mbalimbali binafsi na ya kiserikali ili kuendesha mikutano yao na kufanya ufanisi mkubwa katika kazi na matukio mbalimbali yanayofanyika na kampuni husika.