November 24, 2024

Tanzania yapewa changamoto kukusanya takwimu kidijitali

Njia hiyo itasaidia kukusanya takwimu za kijamii badala ya kutegemea data na mipango kutoka jumuiya za kimataifa.

  • Njia hiyo itasaidia kukusanya takwimu za kijamii badala ya kutegemea data na mipango kutoka jumuiya za kimataifa.
  • Pia itaharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Dar es Salaam. Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinazotaka kufikia kwa ubora Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) zinapaswa kubuni teknolojia zao wenyewe zitakazosaidia kukusanya takwimu za kijamii badala ya kutegemea data na mipango kutoka jumuiya za kimataifa.

Mmoja wa waanzilishi wa spika janja ya Kaya, Isaya Yunge ametoa ushauri huo wakati akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani, amesema barani Afrika data nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuleta matokeo chanya katika shughuli za maendeleo.

Amesema takwimu hizo zinaweza kukusanywa na kuchambuliwa kwa njia ya kidijitali hasa matumizi ya mitandao ya kijamii inayokuwa kwa kasi barani humo. 

Mitandao hiyo itasaidia kufahamu hali halisi za wananchi na mahitaji yao na kubuniwa kwa teknolojia rahisi ya kuboresha hali zao. 

“Mimi nafikiri bara la Afrika waamke waweze kuona thamani ya data. Tunaamini kuwa tuna dhahabu, madini ya thamani lakini kuna dhahabu mpya ambayo ni dijitali ambayo ni data,” amesema Yunge.


Zinazohusiana:


Akizungumzia kuhusu spika ya Kaya, amesema inaweza kufanya kazi kwa kumsikiliza binadamu ambayo ni ndoto ya Afrika kutafuta takwimu zake yenyewe kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

“Smart Kaya kama akili bandia ya spika janja ina uwezo wa kuvuna data, kuzitafsiri na kuweza kuziweka katika makundi ambayo Serikali au watafiti wanaweza kuzitumia katika kufanya maamuzi.

“Kwa mfano tunaweza kutambua katika kaya za kiafrika kuna akina mama wangapi ni wajawazito.” amesema Yunge na kuongeza kuwa, “kwa hiyo ukujua ni kiasi gani idadi ya watu inaongezeka na pia ukajua kiasi gani cha dawa upeleke hospitali na ukaweza kujua watu hawa wako mkoa gani, wilaya gani, tarafa au kijiji fulani.”