Youtube yaongeza udhibiti wa maudhui kwa watumiaji wake
Sasa, kila mchapishaji atatakiwa kuonyesha lengo la kuchapisha maudhui yake. Hatua hiyo ni kuwalinda watoto na maudhui yasiyofaa hasa matangazo yasiyoendana na umri wao.
- Sasa, kila mchapishaji atatakiwa kuonyesha lengo la kuchapisha maudhui yake.
- Hatua hiyo ni kuwalinda watoto na maudhui yasiyofaa hasa matangazo yasiyoendana na umri wao.
Siku chache baada ya Google kutozwa faini ya Sh390 bilioni kwa mtandao wake wa Youtube kukiuka sheria ya faragha kwa watoto (Child privacy), mtandao huo umeanza kudhibiti maudhui yanayochapishwa na watumiaji wake.
Youtube walifanya kosa la kuingilia jumbe zinazohusu watoto ambao ni moja ya wateja na wenye haki ya kuwa na faragha katika maudhui wanayoangalia na kutumia vibaya takwimu za watumiaji wake kupata matangazo.
Ili kukwepa kurudia makosa yaliyotokea, sasa wanaotaka kuchapisha maudhui katika mtandao huo wanapaswa kueleza lengo lao ili kuondoa mkanganyiko na muingiliano wa maudhui hasa ya watoto walio chini ya miaka 13.
Pia maudhui yao yatahakikiwa kabla ya kuchapishwa ili yaangaliwe na watu waliokusudiwa na siyo watoto.
Youtube wamebadili mpangilio unaohusu maudhui ya watoto kwa kuhakikisha maudhui yote yanazohusu watoto yanaendana na watoto walio na umri kuazia miaka 13 ili kuepusha balaa la kuingilia maudhui hayo.
Baada ya Youtube kuchukua hatua hizo, wachapishaji maudhui wameanza kubadili dhima ya maudhui yao ili wasiende kinyume na masharti ya mtandao huo.
Hata hivyo, Youtube bado hawajatoa vigezo vya namna maudhui yanatakiwa kuwa ila wamesisitiza juu ya suala la kuchapisha maudhui yenye kulenga watoto wa miaka 13 na kuendelea lakini kuhakikisha maudhui ya watoto hayachangamani na matangazo yasiyowahusu.