October 6, 2024

App ya Sheria Kiganjani yatwaa tuzo ya matumizi bora ya teknolojia Afrika

Ushindi wa App hiyo ya Tanzania umetokana na uwekezaji iliyofanya katika matumizi ya teknolojia kutoa msaada wa kisheria mtandaoni.

  • Imetwaa tuzo hiyo  jana jijini Johannesburg, Afrika Kusini katika tuzo za sheria Afrika (The African Legal Awards 2019).
  • Ushindi wa App hiyo umetokana na uwekezaji iliyofanya katika matumizi ya teknolojia kutoa msaada wa kisheria mtandaoni. 
  • Imezibwaga kampuni tano za Afrika ilizoshindanishwa nazo. 
  • Hivi karibuni ilichaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika shindano la dunia la Seedstars nchini Uswisi. 

Dar es Salaam. Kampuni ya uwakili ya  Extent Corporate Advisory (ECA) inayosimamia programu tumishi (App) ya Sheria Kiganjani imetwaa tuzo ya Afrika  ya matumizi bora ya teknolojia katika utoaji wa msaada wa kisheria mtandaoni, jambo linalowasaidia Watanzania kufanya maamuzi sahihi ya kisheria. 

Sheria Kiganjani ni app ya Tanzania inayotoa msaada wa kisheria kwa njia ya mtandao ikiwemo elimu ya sheria na kuwaunganisha wananchi na mawakili katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha haki inakuwa sehemu ya jamii ya Watanzania.

ECA inayoendesha na vijana wa Tanzania imeibuka mshindi wa kwanza katika tuzo hizo za sheria za “The African Legal Awards 2019” zilizofanyika jana (Septemba 6, 2019) jijini Johannesburg, Afrika Kusini katika kipengele cha kampuni za sheria zinazotumia teknolojia kutoa huduma za msaada wa sheria. 

Kupitia App yake ya Sheria Kiganjani, ECA imezibwaga kampuni tano ilizoshindanishwa nazo za Anjarwalla & Khanna (A&K) ya nchini Kenya, Epoq Legal – JusDraft na LAW FOR ALL (Afrika Kusini), JUDY Innovative Technologies Limited (Nigeria), na SchoemanLaw Inc (Afrika Kusini).

Kampuni hizo sita ni miongoni mwa kampuni zaidi 100 zinazohusika na shughuli za kisheria Afrika zilizoingia katika vipengele 26 zikichuana kuchukua tuzo hizo ambazo washindi wa vipengele hivyo walitangazwa jana usiku katika klabu ya Wanderers jijini humo. 

Wakili Neema Magimba (aliyevaa nguo nyeusi) akipokea tuzo kwa niaba ya wafanyakazi wa ECA wanaoendesha App ya Sheria Kiganjani  baada ya kuibuka mshindi katika kipengele cha matumizi bora ya teknolojia kutoa huduma za kisheria, katika tuzo zilizotangazwa jana Afrika Kusini. Picha|Nabiry Jumanne.

Mmoja wa Wabia wa ECA, Wakili Nabiry Jumanne ameiambia www.nukta.co.tz kuwa tuzo hiyo aliyoipata jana ni heshima kubwa hasa katika kuthamini msaada wa kisheria wanaoutoa kupitia teknolojia ya simu za mkononi. 

Jumanne amesema tuzo hiyo imewaongezea nguvu zaidi ya kuboresha huduma zao kuhakikisha zinamfikia kila Mtanzania kufaidika na taaluma za sheria. 

“Tunaamini Safari bado ni ndefu katika kuhakikisha si tu haki inatendeka bali inaonekana ikitendeka nia yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania bila kujali hali yake ya kiuchumi anapata msaada wa kisheria,” amesema Jumanne na kuongeza kuwa,

“Tutaendelea kuwekeza mawazo yetu katika kufanikisha urahisi katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa watu wa hali ya chini.”

Tuzo za sheria Afrika za kila mwaka huandaliwa na kampuni ya Legal Week na Chama cha Ushauri wa Mashirika cha Afrika Kusini (CCASA) ili kutambua mchango wa taasisi za umma na binafsi zilizobobea katika shughuli za kisheria Afrika. 


Soma zaidi:


Unaweza kusema mwaka huu ni wa Sheria Kiganjani kutamba kimataifa, ikizingatiwa kuwa Agosti 23, 2019 iliibuka mshindi wa kwanza katika shindano la Seedstars World lililofanyika jijini Dar es Salaam na kupata fursa kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa dunia wa Seedstars nchini Uswisi mwaka ujao na kujiweka katika nafasi ya kushindania mtaji wa uwekezaji wa takriban Sh2.3 bilioni na tuzo zingine. 

Katika shindano hilo, app hiyo ilifanikiwa kuzibwaga kampuni 11 zilizoshindanishwa zikiwemo nne za Zanzibar na saba za Tanzania bara. Startups za Zanzibar ni Zanzibar Health Innovation, Nyumbani Care, Drone Wings na Zanzibit.

Kwa upande wa Tanzania bara, startups saba zilizokuwa zikichuana na Sheria Kiganjani ni Mtabe App, MyHI, Kilimo Fresh Foods na Noobites zimefanikiwa kuingia katika fainali hiyo. Nyingine ni Nuru, EX-Africa Tanzania, na MITZ Innovations.