October 7, 2024

Mozilla inavyopambana kuwalinda watumiaji wake mtandaoni

Programu hiyo na zingine ikiwemo Chrome zimefanya maboresho mbalimbali kukulinda dhidi ya wadukuzi na matumizi mabaya ya taarifa zako mtandaoni lakini bado hazifanya kama inavyotakiwa.

  • Inatoa huduma ya “Tracking Protection” kumzuia mtu wa tatu kuona na kutumia taarifa za watumiaji.
  • Vivinjari vingine kama Safari navyo vinabuni njia mbalimbali kuwalinda watu wake.
  • Wadau wa teknolojia wamesema watumiaji wa mtandao wanapaswa kujiongeza kulinda taarifa zao.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mmoja wa watu wanaotumia programu ya Mozilla Firefox kutafuta vitu mbalimbali mtandaoni na bado una mashaka na usalama wa taarifa zako.

Programu hiyo na zingine ikiwemo Chrome zimefanya maboresho mbalimbali kukulinda dhidi ya wadukuzi na matumizi mabaya ya taarifa zako mtandaoni.  

Tangu Octoba 2018, kivinjari cha Mozilla Firefox toleo la 69 kimehakikisha faragha kwa watumiaji wake kwa kuzuia uwezekano wa mtu asiyehusika kufuatilia kile unachofanya mtandaoni hasa pale unapotumia intaneti ya kuunganishwa (Wi-Fi).

Imeweka huduma ya kumzuia mtu wa tatu kuona unachofanya (“Tracking Protection”) ambayo mtu anaweza kuchagua kuiwasha na kuizima pale atumiapo kivinjari hicho.

Kwa mujibu wa Firefox, maboresho hayo yanadhamiria kuongeza faragha kwa watumiaji wake na kumzuia mtoa huduma za intaneti kuhifadhi taarifa zao kwa ajili ya kuziuza kwingineko ikiwemo makampuni ya matangazo.

Hadi sasa, zaidi ya asilimia 20 ya watumiaji wa kivinjari hicho wanatumia huduma ya “Tracking Protection” na matarajio ya Mozilla ni kutoa ulinzi wa faragha za watumiaji wake kwa asilimia 100.


Zinazohusiana:


Huenda maboresho hayo yatawasaidia na kuwalinda watu wanaofanyabiashara, manunuzi na kufanya miamala ya fedha kwa njia ya simu na mtandao.

Pia kampuni ya Apple nayo inatoa huduma ya kivinjari cha Safari ambacho nacho kimefanyiwa maboresho ya kuzuia ‘traching’ lakini bado baadhi ya watu wamekuwa wakilalamikia taarifa zao kutumiwa vibaya.

Kivinjari cha Safari kina uwezo wa kumzuia mtu wa tatu kabisa lakini Mozila bado ina changamoto baada ya kushindwa kumzuia mtu wa tatu anayetumia “cookies” kukusanya taarifa kwa ajili ya matangazo.

“Cookies” ni taarifa ndogo ndogo ambazo mtoa huduma anazitunza kwa ajili ya kukutambua pale unapotumia mtandao.

Kivinjari cha Mozilla Firefox toleo la 69 kimehakikisha faragha kwa watumiaji wake kwa kuzuia uwezekano wa mtu asiyehusika kufuatilia kile unachofanya mtandaoni. Picha| Mtandao.

Wadau wa usalama mtandaoni

Mtaalam wa programu za kompyuta, Emmanuel Mtuchi amesema suala la usalama mtandaoni bado ni changamoto kubwa kwa sababu hata watoa huduma hawajafanya juhudi za kutosha kuwalinda watumiaji wao.

“Baadhi ya vivinjari kama Opera vinawezesha mtu kuwasha VPN (Virtual Private Network) ili kukabiliana na mtu wa tatu. Lakini bado sio salama kwani Opera wana tabia ya kutunza data za watumiaji wao.

“Kwa Google, ipo wazi kwamba data zako wanazitunza na wanazitumia kwa ajili ya matangazo,” amesema Mtuchi.

Mfanyabiashara   wa jijini Dar es Salaam, Peter Mathias ambaye anatumia mtandao kufanya malipo na manunuzi ya bidhaa zake kwa njia ya E-Bay na maduka mengine ya mtandaoni lakini yeye hutumia njia tofauti kujilinda.

Mathias amesema yeye hulazimika kubadilisha maneno ya siri kila baada ya kufanya miamala ya mtandaoni.

“Japo mimi ni mfanya biashara lakini nimesoma kidogo mambo ya utaalamu wa kompyuta. Haya mambo yapo najua yapo,” amesema Mathias.

Hata hivyo, bado watalaam wa teknolojia wanaendelea kutafuta njia za kudumu kuwalinda watu wanapotafuta vitu mtandaoni.