November 24, 2024

YouTube yajipanga kuzuia matangazo ya biashara kwenye video za watoto

Mtandao huo nakusudia kuondoa matangazo ya biashara yanayomlenga mtumiaji wa simu ya mkononi ambaye anaangalia video zote ambazo zina maudhui ya watoto.

  • Matangazo hayo hayataonekana tena kwenye video zenye maudhui ya watoto chini ya miaka 13. 
  • Hiyo ni hatua ya kuwalinda dhidi ya maudhui yasiyowahusu na yasiyoendana na umri wao. 
  • Huenda maamuzi haya yakaishushia mauzo kampuni ya Google kupitia YouTube.

Dar es Salaam. Mtandao wa YouTube unakusudia kuondoa matangazo ya biashara yanayomlenga mtumiaji wa simu ya mkononi anayeangalia video zote zenye maudhui ya watoto.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa  maamuzi hayo yamefikiwa na YouTube, inayomilikiwa na kampuni ya Marekani ya Google, baada ya mashirika mbalimbali kulalamika juu ya mtandao huo kushindwa kuwalinda watoto hasa pale wanapokuwa wanatumia simu za wazazi wao.

YouTube huweka matangazo mwanzo na katikati ya video zilizopakiwa katika mtandao huo ambayo hutokea bila ridhaa ya mtumiaji. Matangazo hayo, ambayo mengi huwa na sekunde 30 hadi dakika moja, huwezi kuyakwepa mpaka angalau utazame kwa sekunde tano.

Baadhi ya wazazi wakiwemo wa Tanzania wameonyesha kukerwa na matangazo hayo huku wakionya kuwa maudhui yake yanaweza kuwa na athari za moja kwa moja kwa watoto wao. 

Verediana Mwashi mkazi wa Boko jijini Dar es Salaam, ni kati ya wazazi wengi ambao huwapa watoto wao simu kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali kupitia mtandao wa YouTube.

Mwashi amesema mara kadhaa wakati mtoto wake akiangalia video YouTube yamekuwa yakijitokeza matangazo kama ya filamu za Netflix kabla ya video kuanza na wakati mwingine matangazo ya michezo ya kielektroniki, ambayo hayafai kwa watoto.

“Unakuta unaweka video za Ubongo Kids ili Janelle (mtoto wake) ajifunze alfabeti na namba lakini kabla video haijaanza, tangazo la filamu linaanza. Saa zingine tangazo hilo halimfai kabisa mtoto,” ameema Mwashi.

Tafiti za kituo cha utafiti cha Pew zinaonyesha kuwa video zinazolenga watoto chini ya miaka 13 zinatazamwa mara tatu zaidi ya video zisizo na maudhui ya watoto.

Mathalani, wimbo wa “Baby Shark” ambao ni maarufu sana kwa watoto kujifunzia umetazamwa na watu zaidi ya bilioni 3.3 huku ukiwa na miaka mitatu tu tangu kuwekwa kwenye mtandao wa YouTube, ikiwa ni mara nne ya wimbo wa “I will always love you” ulioimbwa na marehemu Whitney Huston. Wimbo wa Huston umetazamwa mara milioni 836.8 licha ya kuwa umedumu katika mtandao huo kwa miaka nane.

Video za kujifunzia watoto zinazopatikana kwenye Youtube ni msaada kwa waalimu na wazazi. Picha| Rodgers George.

Kutokana na video za watoto kupata watazamaji wengi, baadhi ya makampuni yamekuwa yakitumia fursa hiyo kutangaza huduma na bidhaa zao kwa ajili ya kujipatia wateja. 

Mwashi amesema marakebisho hayo yanayofanywa na YouTube yatasaidia kwa kuwa mtoto hataona matangazo ambayo hayaendani na umri wake wakati akijifunza kupitia maudhui ya mtandao huo.

Faida za marekebisho hayo ni kwamba, video zote zinazowalenga watoto chini ya miaka 13 hazitokuwa na matangazo ambayo hayawahusu na hivyo kupelekea kuwepo kwa mazingira salama wakati wa kujifunza kwao.


Zinazohusiana


Licha ya kuwa YouTube inafanya marekebisho hayo, bado imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mtandao huo unakuwa sehemu salama kwa watoto dhidi ya hatari yoyote inayoweza kuwapata wakiwa mtandaoni. 

Ina chaneli maalum ya watoto ya “YouTube Kids” ambayo imekuwa ikitumika na wazazi kwa ajili ya kuwafunza watoto wao hasa katika sekta ya elimu na afya. 

Hata hivyo, wazazi wengi kama Mwashi, bado hawafahamu juu ya chaneli ya YouTube Kids kwani mara nyingi simu inaponunuliwa inakuja moja kwa moja na programu ya YouTube ambayo inakuwa haijatofautisha chaneli ya watoto. 

Hadi sasa, YouTube bado haijaweka wazi ni video gani zinazohesabika kama video za watoto kwani baadhi ya miziki kama “We are the World” ya Michael Jackson ni kati ya video zinazotazamwa na rika la watu wote.

Pamoja na hayo, huenda maamuzi haya yakaishushia mapato kampuni ya Alphabet inayomiliki Google ikizingatiwa kuwa watalazimika kuondoa matangazo yote kwenye video za watoto. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2019, Alphabet ilipata mapato ya Dola za Marekani 36.34 bilioni (Sh82.5 trilioni)  ikiwa ni chini kidogo ya matarajio ya Dola za Marekani 37.33 bilioni sawa na Sh84.7 trilioni.