Kwanini unatakiwa kumfuatilia mtoto wako anapokua mtandaoni?
Ni njia mojawapo ya kumlinda mtoto wa uhalifu wa mtandaoni unaoweza kumpotezea mwelekeo wa maisha.
Watoto wanatakiwa kulinda wakati wote wanapoingia mtandaoni. Picha|Mtandao.
- Ni njia mojawapo ya kumlinda mtoto wa uhalifu wa mtandaoni unaoweza kumpotezea mwelekeo wa maisha.
- Pia ni kumuepusha na ukatili wa kijinsia unaoweza kukatiza ndoto zake za elimu.
Ni wazi kuwa teknolojia inakua kwa kasi kiasi cha kufanya mifumo ya kujifunza na kufanya mambo kuwavutia watu wengi hasa watoto wenye kudadisi kinachojiri mtandaoni.
Baadhi ya watoto wamekuwa wakitumia simu na kompyuta za wazazi wao kuingia mtandaoni ili kujifunza na kuburudika. Lakini wakati mwingine huwa tofauti kwa sababu baadhi ya mambo yanayopatikana mtandaoni yana madhara kiakili na kiafya kwa mtoto.
Hapo ndipo inakuja dhana ya wazazi kuwafuatilia watoto wao wanapokua mtandao ili kujua ni vitu gani wanaangalia na kwa kiasi gani vinachangia kuharibu au kuwakuza katika maadili mema.
Japokuwa bado kuna mjadala katika jamii wa umri sahihi ambao mtoto anatakiwa kuachwa huru bila kuingilia kwa kile anachokifanya mtandaoni. Lakini yapo baadhi ya mambo yanaweza kukupa nguvu ya kumlinda mtoto wako dhidi ya madhara ya intaneti;
Manyanyaso ya mtandaoni ni moja ya sababu ambayo inakutaka kama mzazi kumlinda mtoto wako. Watu wenye nia ovu wanaweza kutumia vifaa vya kidijitali vilivyounganishwa na intaneti kuwatisha, kuwasurutisha watoto kufanya mambo wasiyoyataka.
Vitendo hivyo vya kikatili vinadhoofisha afya na akili ya mtoto na kumfanya awe na msongo wa mawazo. Ni vema kama mzazi kufuatilia watu anaowasiliana nao ikiwemo wale wanaojiita marafiki zake mtandaoni.
Picha na jumbe zisizo na maadili zinaweza kusababisha kuharibika kwa saikolojia ya mtoto hivyo ni vyema mzazi akajihadhari mapema juu ya mambo yanayoangaliwa na mtoto wako na kuhakikisha anadhibiti matumizi ya simu ili kumkinga maudhui yasiyofaa.
Zinazohusiana
Ni vizuri pia kulinda taarifa zinazomhusu mtoto wako kwasababu mtoto akiwa kwenye mtandao ni rahisi kutoa taarifa zake kwa watu kirahisi bila kujali ni watu wa namna gani.
Njia hizo na nyingine nyingi zinaweza kumsaidia mwanao katika matumizi mazuri ya mitandao ya intaneti na mtandao kwa ujumla wake.
Hata hivyo wakati ukimlinda mwanao na uhalifu wa mtandaoni, tumia zaidi njia ya kumfundisha na kumuelewesha madhara ya kutumia mitandao vibaya huku ukimtia moyo kujikita zaidi katika kutekeleza ndoto zake za elimu.