November 24, 2024

Programu za mauzo zinazoweza kuwatoa wanamuziki wa Tanzania

Zaidi ya Youtube, msanii anaweza kuuza kazi zake kupitia programu tumishi za Napster, Apple Music, Spotify na Tidal.

  • Zaidi ya Youtube, msanii anaweza kuuza kazi zake kupitia programu tumishi za Napster, Apple music, Spotify na Tidal.
  • Programu hizo zinamsaidia msanii kuwa na vyanzo vingi vya mapato kulingana na mashabiki na upatikanaji wa soko.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa mtandao wa Youtube umekuwa sehemu muhimu kwa wanamuziki kutangaza kazi zao na kujipatia kipato kuendeleza maisha yao. 

Mtandao ambo ni jukwaa la mtandaoni  linawapa fursa hata wanamuziki wanaochipukia kuonyesha kazi zao ili kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi. Lakini, Youtube ni sehemu pekee inayoweza kumpatia msanii mafanikio anayoyataka? Na siyo kuna fursa gani zingine ambazo wanamuziki wanaweza kuzitumia kufikisha ujumbe kwenye jamii na kufikia kilele cha mafanikio?

Baadhi ya wadau wa muziki wanaeleza kuwa kwa mwanamuziki kuanza kufaidika na yeye kutumia Youtube inatamlazimu kufanya jitihada mbalimbali za kuwashawishi watu kufuatilia akaunti yake 

Mmiliki wa studio ya muziki ya  “Work Of Arts Studios (WOAS)” iliyopo jijini Dar es Salaam, Erick Maleza ameiambia www.nukta.co.tz kuwa malipo ya mtandao wa YouTube siyo kitu ambacho msanii anayeanza anatakiwa kutegemea sana kwani ni ya kiwango cha chini.

“Mara nyingi youtube inalipa kwa tangazo na kwa Tanzania kiwango ni kidogo sana kwani unaweza ukakuta mtu akitazama wimbo wako ikawa ni sawa na dola moja ya Marekani au chini ya hapo,” amesema Maleza.

Kwa wastani mtu anatakiwa awe na wafuasi zaidi ya 1,000 na ili uanze kulipwa ni hadi pale pesa itakapofika walau Dola za Marekani 100 (takribani Sh229,900) jambo ambalo ni changamoto hasa kwa wasanii wanaoanza kuweka kazi zao katika mtandao huo ambao kwa wastani unalipa kiasi cha dola 0.8 (takribani Sh1800) kwa kila mtu anapotazama video ya muhusika.  

Ni sawa na kusema, kama msanii akaunti yake inafuatiliwa sana na watu, basi anaweza kutengeneza kati ya sh99,000 na163,250 ambayo ni zaidi ya mil 1.9 kwa mwaka.


Zinazohusiana:


Wakati wasanii wa Tanzania wakiendelea kujiimarisha Youtube, wana kila sababu ya kupanua wigo wa kuyafikia masoko mengine ya mtandaoni ili kuongeza idadi ya mashabiki na kipato pia. Nukta inayokupa yanayokuhusu inakuletea programu tumishi (App) muhimu ambazo zinaweza kuwasaidia:

Napster

App hii inapatikana kwenye simu janja ambapo mtu anapaswa kuipakua na kuanza kufurahia nyimbo zaidi ya milioni 40 kwa mtindo wa audio kwa gharama ya sh30,000 kwa mwezi.

App hii inaongoza kwa kulipa wasanii pesa nyingi kuliko majukwaa mengine yote.

Huku app hiyo ikilipa zaidi ya Sh40 kwa kila mtu asikilizapo wimbo, jukwaa hili linahitaji msanii afikishe idadi ya wafuasi zaidi ya 78,000 ili kulipwa pesa yake. 

Kwa muktadha huo, kwa msanii Diamond Platnumz kupitia wimbo wake wa Kanyaga wenye uliotazamwa zaidi ya milioni  7 hadi Agosti 15, 2019 kama angetumia app hiyoi angelipwa takribani milioni 3.1.

Muonekano wa programu ya Napster. Picha|Mtandao.

Apple Music

Ongezeko la watumiaji wa simu za “Apple” inaweza kuwa faida kubwa kwa wasanii kwani app ya muziki ya Apple linalipa kiasi cha Sh18 kwa kila mtu asikilizapo muziki wa msanii mwenye hati miliki. Pesa hiyo  ni sawa na Sh18,000 kwa kila wasikilizaji 1,000 kwa siku sawa na Sh558,000 kwa mwezi. 

Hivyo ni sawa na kusema, kama msanii anaweza kupata wasikilizaji milioni moja, ananaweza kulipwa milioni 18. Hata hivyo, msanii atatakiwa kufikisha idadi ya wasikilizaji zaidi ya laki mbili kupata pesa hiyo jambo ambalo ni rahisi kwa baadhi ya wasanii kama Diamond Platnumz mwenye wafuasi zaidi milioni 2 katika mtandao wa Youtube.

Spotify

App hii inapatikana bure nchini Marekani na kulipiwa kwa mtumiaji yeyote nje ya nchi hiyo. 

Kwa wastani, Spotify inalipa kiasi cha Sh10 kila mtu achezapo wimbo. Hivyo ni kusema kama wimbo umesikilizwa na watu 1,000 kwa siku, msanii anaweza kupata Sh310,000 kwa mwezi na hivyo milioni 3.7 kwa mwaka ambayo ni zaidi ya pesa ambayo YouTube inalipa kwa mtazamo sawa kwa mwaka.

Tidal Music

Hadi kufikia Desemba 2018, App hii ilikua imefikia nchi 53. App hi kama zingine zote, inahitaji mtumiaji ajiunge ili kuweza kufurahia video pamoja na audio kutoka kwa wasani mbali mbali.

Japo hakuna taarifa kamili za namna gani app hii inalipa wasanii lakini app hii imetajwa kati ya app inayolopa wasanii asilimia kubwa ya mapato yake.

Muonekano wa Tidal inaweza kuwa sehemu muhimu ya kuwatoa wanamuziki wa Tanzania. Picha|Mtandao.