October 6, 2024

Instagram kuja na sera ya kudhibiti maudhi ya watumiaji wake

Mtoa maudhi sasa ataweza kukata rufaa kama maudhi yake yakifutwa.


  • Imebuni njia rahisi na ya haraka kubaini na kufuta akaunti za watu ambazo zinakiuka sera za maudhui za mtandao huo. 
  • Mtoa maudhi sasa ataweza kukata rufaa kama maudhi yake yakifutwa.
  • Sera hiyo inakuja baada ya sera hivi karibu kuja na mabadiliko ya kutaka kuficha ‘like’ na mfumo wa kuzibiti ulilishaji kwenye mtandao.

Mtandao wa Instagram umefanya mabadiliko tena ambapo sasa imebuni njia rahisi na ya haraka kubaini na kufuta akaunti za watu ambazo mara kwa mara zimekuwa zikikiuka sera za maudhui za mtandao huo. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa kwenye tovuti ya mtandao huo, imeeleza kuwa sera  zilizopo zinaruhusu kufuta akaunti ambazo zina asilimia fulani ya ukiukwaji wa maudhui.

“Sasa tunaanzisha sera mpya ambayo pamoja na kufuta au kuondoa  akaunti ambayo ina asilimia fulani ya ukiukaji maudhui, pia  tutaondoa tena akaunti zenye ukiukwaji mkubwa wa maudhui,” inaeleza taarifa hiyo. 

Mabadiliko hayo yataiwezesha Instagram kutekeleza sera hizo mara kwa mara na kufanya watu kuwajibika kwa kile wanachochapisha kwenye Instagram.

Pia Instagram imeanzisha kipengele  kipya cha taarifa za kufuta akaunti ambapo kitakuwa kinatoa taarifa kwa watumiaji wake kuzifahamu akaunti zao ambazo ziko  hatarini kufutwa au kusimamishwa.

Kwa kuanzia rufaa hizo zitajikita kwenye maudhi ya uzalilishaji wa kingono, unyanyasaji, uuzaji wa dawa za kulevya, maneno ya chuki na kukabiliana na ugaidi.

Taarifa hiyo ya instagrama imesema kuwa, “Ikiwa maudhui yatakuwa yameondolewa kimakosa basi yataweza kurejeshwa mara mmoja,”

Instagram imesema inatoa nafasi kwa mtumiaji wake  kukata rufaa kupitia kituo cha msaada wa ‘Help Center’ ambapo kwa miezi michache ijayo ataweza kupata moja kwa moja kwenye mtandao wa instagram.

Mabadiliko hayo ni muendeleo wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Instagram katika kuboresha mtandao wake ili kuwavuti watu wengi.