November 24, 2024

Facebook yajipanga kuunda bodi huru kusimamia maudhui

Bodi hiyo itakuwa na wataalam mbalimbali kwa ajili ya kufuatilia maamuzi ya uhariri wa maudhui ya mtandao huo.

Facebook yajipanga kujiweka kando kusimamia maudhui ya watumiaji wake. Picha|Mtandao.


  • Bodi hiyo itakuwa na wataalam mbalimbali kwa ajili ya kufuatilia maamuzi ya uhariri wa maudhui ya mtandao huo.
  • Huenda itasaidia kupatikana kwa haki za watumiaji kutokana na kesi mbalimbali zinazohusu maudhui.

Huenda watumiaji wa mtandao wa Facebook wakapata haki katika maamuzi ya kesi zinazohusiana na maudhui ya mtandao huo baada ya kuwepo kwa mipango ya kuundwa kwa bodi huru itakayokuwa inafuatilia uhariri wa maudhui ya mtandao huo. 

Mpango huo unakuja wakati Facebook ikikabiliwa na shutuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya taarifa za watumiaji wake lakini kuwepo kwa maudhui yanayohamasisha chuki na uhasama katika jamii. 

Mtandao huo, ulioanzishwa na kuongozwa na raia wa Marekani, Mark Zuckerberg utatumia miezi sita kuunda bodi hiyo ambayo inaweza kutoa mfumo mpya kwa ajili ya kufungua kanuni na njia mpya kwa watumiaji kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya uhariri.

Bodi hiyo itakuwa huru na itapewa mamlaka ya kubatilisha au kupitisha maamuzi ya uhariri wa maudhui ya Facebook kwa kuzingatia haki za watumiaji wa mtandao huo.  


Zinazohusiana: 


Bodi hiyo itajumuisha wataalam wa maudhui, faragha, uhuru wa kujieleza, haki za binadamu, uandishi wa habari, haki za kiraia na usalama mtandaoni.  

Pia wajumbe wa bodi hiyo watatoa kwa uwazi jinsi walivyoamua kila kesi wanayokutana nayo katika mtandao huo. 

Hata hivyo, bodi hiyo inatarajiwa kuundwa baada ya Facebook kukutana na wadau mbalimbali ili kuweka misingi bora ya kikanuni na jinsi bodi hiyo itakavyotekeleza majukumu yake. 

Katika kipindi hicho, Facebook yenye watumiaji zaidi ya bilioni 2 itafanya warsha katika miji ya  Singapore, Delhi, Nairobi, Berlin, New York, Mexico City na maeneo mengine ili kupata maoni ya wadau.  

Kuundwa kwa bodi hiyo kunatajwa kama njia ya Facebook kujiweka kando juu ya maamuzi mbalimbali ya uhariri wa maudhui kutokana malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai hawatendewi haki.