November 24, 2024

Mipango ya Jony Ive baada ya kuondoka Apple

Anatarajia kufungua kampuni ya usanifu ya LoveFrom itakayokuwa inasimamia miradi mbalimbali ya ubunifu.

Ive mwenye miaka 52, wakati akihojiwa na vyombo vya habari amesema licha ya kuondoka Apple bado ataendelea kufanya nayo kazi katika miradi mbalimbali ya teknolojia. Picha|Mtandao.


  • Anatarajia kufungua kampuni ya usanifu ya LoveFrom itakayokuwa inasimamia miradi mbalimbali ya ubunifu. 
  • Alikuwa Msanifu Mkuu na ameitumikia Apple kwa takribani miaka 30. 
  • Amehusika katika usanifu wa programu za iMac, iPhone na iPod. 
  • Apple imesema alikuwa kiungo muhimu cha mafanikio ya kampuni hiyo.

Msanifu Mkuu wa kampuni ya Apple ya nchini Marekani inayotengeneza simu za Iphone, Jony Ive anaondoka katika kampuni hiyo baada ya kuitumikia kwa takriban miaka 30. 

Ive amekuwa mfanyakazi muhimu wa Apple, ikizingatiwa kuwa amekuwa akifanya kazi ya usanifu na ubunifu wa bidhaa za Iphone, iMacs na iPod ambazo zimeifanya Apple kusimama katika soko la mawasiliano ya simu mpaka sasa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana (Juni 27, 2019), Ive ameamua kuanzisha kampuni yake binafsi ya usanifu ya LoveFrom ambayo itakuwa inaratibu miradi ya ubunifu kwa wateja mbalimbali.

Apple imeelezea kuwa Ive ni mtu muhimu katika kampuni hiyo kwasababu alikuwa anasimamia mfumo wa Apple, ‘interface’ ya mtumiaji, ufungaji na  miradi mikubwa ya usanifu kama vile Apple Park na maduka ya rejareja ya Apple, pamoja na mipango ya kampuni hiyo. 

“Jony ni mfano wa umoja katika ulimwengu wa kubuni na jukumu lake katika uamsho wa Apple haliwezi kasahaurika, tangu iMac ya 1998 hadi ujio wa iPhone,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Apple, Tim Cook.


Soma zaidi: 


Kampuni ya LoveFrom itakuwa na makao yake California, Marekani na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwaka 2020 huku Apple atakuwa mteja wake wa mwanzo. 

Ive mwenye miaka 52, wakati akihojiwa na vyombo vya habari amesema licha ya kuondoka Apple bado ataendelea kufanya nayo kazi katika miradi mbalimbali ya teknolojia. 

Dalili za kuongoka kwa Ive, zilianza kuonekana katika miaka ya hivi karibuni baada ya kujiondoa katika shughuli za kila siku za Apple, na kujihusisha na miradi ya nje ikiwemo kusaidia kubuni kamera ya mwisho ya Leica, mti wa Krismasi, na pete ya almasi iliyouzwa kwa zaidi dola za Marekani 256,000 sawa na Sh588.7 milioni.

Muda mfupi baada ya taarifa za Ive kuondoka Apple kutangazwa, kampuni hiyo imepoteza Sh21 trilioni (Dola za Marekani 9 bilioni) katika soko la hisa.