Mfumo mpya kuharakisha mashauri ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Ofisi hiyo imekabidhiwa mfumo huo ambao utasaidia katika usajili, upangaji na ufuatiliaji wa mashauri kwa urahisi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Clement Mashamba (Kulia), akipokea rasmi Mfumo wa Usimamazi wa Mashauri kutoka kwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Tehama wa Wakala ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba (Kushoto) Makabidhiano hayo yalifanyika leo Ijuma, Juni 7,2019 Jijini Dar es Salaam. Picha|Habari-Maelezo.
- Ofisi hiyo imekabidhiwa mfumo huo ambao utasaidia katika usajili, upangaji na ufuatiliaji wa mashauri kwa urahisi.
- Utawaondolea wananchi kero ya kuchelewa kupata huduma katika ofisi hiyo.
Dar es Salaam. Huenda ufanisi wa usajili na uendeshaji wa mashauri katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali utaimarika, baada ya Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) kukabidhi mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa taarifa katika ofisi hiyo ili kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na haraka.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Tehama wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), Benedict Ndomba aliyekuwa akizungumza katika makabidhiano ya mfumo huo leo (Juni 7, 2019), amesema kuwa ofisi yake inatumia wataalam wake wa Tehama kutengeneza mifumo inayorahisisha utendaji wa kazi katika taasisi mbalimbali nchini.
Amesema mfumo huo utasaidia katika utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi katika taasisi hiyo muhimu serikalini.
“Mfumo huu umebuniwa, umesanifiwa na kutengenezwa na watumishi wa umma na tumekubaliana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa mfumo huu utekelezwe kwa awamu mbili ili kuweza kukidhi mahitaji ya wadau wote,” amesema Ndomba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari-Maelezo, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfumo huo, imetengenezwa kwa moduli itakayoisaidia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yake hasa ya ndani kwenye masuala ya usimamizi mashauri ambapo pia itakuwa ni nyenzo muhimu ya utekelezaji majukumu kwa haraka.
Zinahusiana:
- Apple yaingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Clement Mashamba amepongeza eGA kwa kutengeneza mfumo huo kwa mahitaji ya ofisi ya Wakili wa Serikali na kudai kuwa watakuwa wanatekeleza majukumu kwa haraka na kwa ufanisi zaidi katika kutatua kero za wananchi.
“Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao ili kuhakikisha awamu zote za utengenezaji wa mfumo huu zinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaostahili, lakini pia ofisi yangu inatambua mchango huu mkubwa kwa kazi zetu ya kisheria,” Dk Mashamba.
Aidha Dk Mashamba amesema mfumo huo utasaidia katika usimamizi wa majalada ya mashauri; usajili wa mashauri; upangaji wa mashauri yanayoshughulikiwa; na ufutiliaji wa maendeleo ya ashauri.
Huduma zingine ni usimamizi wa ratiba za mashauri; utoaji wa taarifa; uhakiki wa mwenendo wa mashauri na uhamishaji wa taarifa na takwimu.