October 6, 2024

Teknolojia ya kuhakiki pembejeo feki za kilimo kuingia Tanzania

Mfumo huo utasaidia kutambua pembejeo feki za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu huku ukiongeza uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.

  • Mfumo huo utasaidia kutambua pembejeo feki za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu.
  • Utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.
  • Utazifaidisha nchi nyingine za Ethiopia, Burundi na Eswatini (zamani wa Swaziland).

Dar es Salaam. Huenda wakulima wa Tanzania wakaongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo, baada kubuniwa kwa mfumo wa kidijitali wa utakaodhibiti usambazaji wa mbegu feki kwa wakulima. 

Mfumo huo ambao unajulikana kwa Kiengereza kama ‘seed label online verification system’ utasaidia kudhibiti usambazaji wa mbegu zisizo na ubora na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao hapa nchini. 

Hatua hiyo inakuja baada ya kampuni ya teknolojia ya kimataifa ya mPedigree  kuanzisha ushirikiano na chemba ya biashara ya Jumuiya ya Soko la Pamoja la nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (Comesa) ili kupanua teknolojia ya ulinzi wa pembejeo za kilimo katika eneo lote la Comesa hasa kwa nchi ambazo hazikuwepo katika jumuiya hiyo. 

Licha ya kuwa Tanzania siyo mwanachama wa Comesa, lakini teknolojia hiyo itawafikia pia wakulima nchini. Tanzania iliondoka rasmi Comesa mwaka 2000 na kwa sasa ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika I(SADC), ambavyo vinaongeza maeneo ya biashara ya bure kwa nchi za Comesa.

mPedigree imekuwa ikitoa huduma za ulinzi kwa bidhaa muhimu za walaji kama vile madawa na pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu na mbolea katika soko la Tanzania kupitia Taasisi ya Vyeti vya Msaada wa Mbegu ya Tanzania (TOSCI) ili kupata mnyororo imara wa usambazaji bidhaa na msisitizo umewekwa katika uhakiki wa mbegu na uangalizi wa soko. 

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na mPedigree na Comesa, ushirikiano huo una maana kuwa wakulima nchini sasa wanaweza kufikiwa na usaidizi wa kanda katika kuchunguza na kutambua pembejeo za kilimo halisi na zile za bandia kwa kutumia njia ya intaneti pamoja na mfumo wa kificho wa ‘USSD’.

Mfumo huo ambao unajulikana kwa Kiengereza kama ‘seed label online verification system’ utasaidia kudhibiti usambazaji wa mbegu zisizo na ubora na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao hapa nchini. Picha|Mtandao. 

Huduma hiyo pia itapatikana katika nchi za COMESA zilizoongezwa katika mradi huo za Ethiopia, Burundi na Eswatini (zamani wa Swaziland).

“Mfumo huo utaisaidia kanda si tu kuondoa kesi za pembejeo za kilimo bandia kama vile mbegu, mbolea na bidhaa za ulinzi wa mazao lakini pia kuongeza biashara ya mbegu bora zilizohakikiwa,” amesema Mkurugenzi wa mPedigree, Selorm Branttie katika taarifa hiyo.  

Branttie alikuwa akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi na mafunzo ya Sekretarieti ya COMESA kwa makampuni ya mbegu juu ya kuagiza na kutumia lebo za mbegu za COMESA na vyeti nchini Zambia.

Uzinduzi huo ulifanyika chini ya Umoja wa COMESA wa Biashara ya Bidhaa katika Mpango wa Mbegu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (ACTESA).

“Ushirikiano huu mpya siyo tu utapenya zaidi ndani ya minyororo ya usambazaji wa pembejeo nchini lakini pia kufikia usaidizi mpya wa mfumo wa utendaji wa sekta ya kilimo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 


Zinazohusiana: 


Kama mradi huo utatekelezwa vizuri utasaidia kuondoa biashara ya udanganyifu katika pembejeo za kilimo bandia, ambayo imechangia katika utendaji mbaya wa wakulima wadogo takriban 80 milioni na uhaba wa chakula katika eneo la Comesa.

“Kwa kila mfuko wa mbegu ambao utakuwa na stika ya Comesa, inamaanisha kuwa chanzo cha mbegu hiyo kimehakikiwa na inaweza kufuatiliwa hadi pointi ya mwisho. Comesa itafanya kazi na Mamlaka ya Taifa ya Mbegu ili kuhakikisha kuwa pembejeo za kilimo kama vile mbegu feki zinaondolewa kutoka kwenye soko, “amesema Mkurugenzi wa Viwanda na Kilimo wa Comesa, Thierry Kalonji.