November 24, 2024

Taka za kielektroniki fursa nyingine kwa vijana kujiajiri

Serikali duniani zimetakiwa kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya kuchakata na kutumia upya taka za kielektroniki ili kuwafungulia fursa za ajira vijana wenye ndoto ya kujiajiri.

ILO inasema ni asilimia 20 ya taka hizo za kielektroniki ndiyo hurejelezwa katika mazingira rasmi. Taka hizo pia zimekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo ambayo hayana teknolojia ya urejelezaji. Picha|Mtandao.


  • Serikali duniani zimetakiwa kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya kuchakata na kutumia upya taka za kielektroniki ili kuwafungulia fursa za ajira vijana wenye ndoto ya kujiajiri.
  • Kila mwaka huzalishwa tani 50 milioni za taka za kielektroniki lakini ni asilimia 20 ya taka hizo hurejelezwa katika mazingira rasmi.
  • Imekumbusha pia umuhimu wa kutumia vijana ikisema kuwa vijana wana  ubunifu mkubwa wa kutumia taka za kielektroniki na hivyo ni fursa ya kuongeza nafasi za ajira.

Dar es Salaam. Shirika la kazi duniani (ILO) limetaka hatua za haraka zichukuliwe katika udhibiti wa  taka za kielektroniki zinazozalishwa katika maeneo mbalimbali duniani ili zifungue fursa za ajira zenye utu kwa vijana. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa leo (Aprili 18, 2019), rai hiyo imetolewa katika mkutano wa ILO unaofanyika Geneva, Uswisi ambako wawakilishi wa serikali, wafanyakazi na waajiri wamesema wakati umefika kwa serikali kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya kuchakata na kutumia upya taka za kielektroniki.

Wawakilishi hao wamebainisha kuwa kasi ya ongezeko la taka hizo ni kubwa ambapo kila mwaka huzalishwa tani 50 milioni  zikiwa na thamani ya Dola za Marekani 62  bilioni (Sh142.44 trilioni).

Hata hivyo, ILO inasema ni asilimia 20 ya taka hizo za kielektroniki ndiyo hurejelezwa (recycling) katika mazingira rasmi. 

Taka hizo pia zimekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo ambayo hayana teknolojia ya urejelezaji.

“Kama hiyo  haitoshi, mazingira ambamo wafanyakazi wanaookota taka hizo ili ziweze kurejelezwa nayo ni magumu, wakiwa hawana mamlaka yoyote juu ya  ujira wa fedha zitokanazo na kazi hiyo ya suluba huku wakivunja taka hizo kwa mikono mitupu bila vifaa vya kujikinga,” inaeleza sehemu ya taarifa  hiyo.


Soma zaidi:


Mwenyekiti wa jopo la kimataifa la mashauriano kuhusu kazi zenye utu na taka ngumu kutoka ILO, Nikhil Seth amesema taka za kielektroniki zinazidi kuwa rasilimali muhimu kwa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi.

Amesema wakiwekewa mazingira mazuri wanaweza kuingia kwenye mnyororo wa thamani kuanzia kwa wanaoziokota, wanaozitengeneza upya, wanaozitumia tena na wanaorejeleza vifaa vya kielektroniki ambapo wataleta huduma bunifu na bidhaa kwenye soko na kurahisisha ukuaji wa uchumi.

“Kuhakikisha kuwa taka za kielektroniki zinazozalishwa hazileti aina ya madhara kwa  mazingira, kwa afya ya binadamu na kwa wale wote wanaofanya kazi kwenye viwanda  ya usimamizi wa taka za kielektroniki,” amesema Seth katika taarifa hiyo.

ILO imekumbusha pia umuhimu wa kutumia vijana kwasababu wana  ubunifu mkubwa wa kutumia taka za kielektroniki na hivyo ni fursa ya kuongeza nafasi za ajira.

Hata hivyo, matumizi ya teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira yatasaidia kuongeza ubunifu kwa vijana kutengeneza bidhaa zitakazotumika katika shughuli za maendeleo.