Miaka 15 ya Gmail inavyoongeza thamani bidhaa za Google
Barua pepe ya Gmail ilianzishwa rami mwaka 2004 ambapo imekuwa nyenzo muhimu ya kuipaisha kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Google duniani.
Gmail imeendelea kuwa maarufu kwa watumiaji kutokana na maboresho inayofanya kila inapohitajika. Picha|Google.
- Barua pepe ya Gmail ilianzishwa rami mwaka 2004 ambapo imekuwa nyenzo muhimu ya kuipaisha kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Google duniani.
- Gmail ina watumiaji zaidi ya 1 bilioni na haina dalili ya kushuka chini.
- Imekuwa mshindani mkubwa wa barua pepe zingine za Yahoo, Hotmail, Zoho na GMX.
Kama wewe ni mtumiaji wa bidhaa za Google hasa barua pepe ya Gmail huenda utakuwa umegundua kitu tofauti katika matumizi yako tangu Aprili 1, 2019. Kila ukifungua mtandao huo utakutana na neno ‘Gmail turns 15’ likiwa na maana kuwa Gmail inaadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004.
Gmail ambayo imejipatia umaarufu mkubwa duniani, imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kutuma na kupokea barua pepe zinazotumika kwa shughuli mbalimbali za ofisi, biashara na mambo binafsi.
Barua pepe hiyo ambayo inahudumia zaidi ya watumiaji 1 bilioni imekuwa ikitoa ushindani mkali kwa kampuni zingine zinazotoa huduma ambapo mwaka 2012 ilichukua nafasi ya Hotmail kwa umaarufu na haina dalili yeyote ya kushuka chini.
Washindani wake wengine ni Yahoo ambayo ina watumia takriban 255 milioni hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2018, Yandex, Outlook, Zoho, Proton, GMX, iCloud na AOL.
Umaarufu wa Gmail unatokana na uwezo wake wa kuwapa watumiaji huduma mbalimbali ikiwemo 10GB za kuhifadhi kumbukumbu na taarifa. Pia unapata kalenda, sehemu ya kutunza picha, ushauri wa masuala ya fedha, Youtube na hata uandishi wa habari (blogging).
Lakini Gmail imekuwa kiungo muhimu cha huduma zingine za kampuni ya Google ambazo zinapatikana katika duka lake la mtandaoni la Play Store. Ili mtumiaji apate bidhaa katika duka hilo analazimika kuwa na barua pepe ya Gmail, la sivyo hawezi kuzipata wala kupakua.
Hii imekuwa ni njia mojawapo wanayotumia Google kuhakikisha inabaki kileleni katika soko la ushindani wa huduma za mawasiliano pepe duniani.
Soma zaidi
Hata hivyo, imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kumuwezesha mtumiaji kuandika barua na kuipangilia vizuri katika muda ambao anataka imfikie mtumiaji (Scheduling).
Mathalan, unaweza kandika barua pepe leo na ukaipangilia ijutumie yenyewe baada ya siku tatu au saa chache zijazo kulingana na mahitaji yako. Maboresho hayo yanarahisisha maisha kwa sababu wakati mwingine tunakwama kutuma barua kwa sababu ya kubanwa na majukumu mengi ya kikazi.
Gmail ambayo inasimamiwa na kampuni ya Google ya nchini Marekani imekuja na kipengele cha ‘Smart Compose‘ kipengele hiki kinasaidia katika uandishi wa barua pepe ambapo kinatabiri neno unalokukusudia kuandika katika sehemu ya kuandikia kwa kukuwekea maneno mbele ya kiandishi ili kukurahisishia kazi ya kuchapa maandishi.
Kama wewe ni mtumiaji wa Gmail una kipi cha kujivunia katika maadhimisho ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwake? Unafikiri Gmail ni mahali salama kupata huduma za kutuma na kupokea barua pepe?