Fab Lab kuongeza idadi vituo vya ubunifu Tanzania
Ni kituo cha ubunifu wa teknolojia kutoka Ireland ambacho kinakusudia kufungua tawi nchini ili kuwafikia vijana wenye mawazo ya kibunifu.
- Ni kituo cha ubunifu wa teknolojia kutoka Ireland ambacho kinakusudia kufungua tawi nchini ili kuwafikia vijana wenye mawazo ya kibunifu.
Taasisi ya Fab Foundation ya nchini Ireland inayomiliki kituo cha kijamii cha Fab Lab inakusudia kufungua tawi Tanzania ikiwa ni hatua ya kuwafikia na kuwasaidia vijana wenye mawazo ya ubunifu wa ujasiriamali kufikia ndoto zao.
Fab Lab ina vituo vya kijamii 7 nchini Ireland ambapo imejikita katika kusaidia mabadiliko ya kisera katika elimu, mafunzo, maendeleo ya jamii kwa kutumia ujasirimali wa teknolojia.
Akizungumza katika Wiki ya Ubunifu jijini Dar es salaam, Patrick Colgan mjumbe kutoka taasisi hiyo amesema wameona kuna umuhimu wa kuja Tanzania ikizingatiwa kuwa kuna vijana wanafanya kazi nzuri za ubunifu wa teknolojia na wanahitaji kuendelezwa ili kuifikia jamii kwa upana.
“Mawazo ya wajasiriamali ni muhimu, hivyo taasisi hiyo imeanzishwa ili kubadili mawazo hayo kua kitu kikubwa kwa jili ya nchi,” amesema Colgan.
Soma zaidi:
Katika kuhakikisha Fab Lab inaingia Tanzania kwa wakati, imeanza mchakato wa utafiti wa jinsi kituo hicho kitakavyojiendesha nchini na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Ujio wa Fab Lab nchini itakuwa ni fursa ya nyingine kwa wabunifu kufaidika ikizingatiwa kuwa bado uhitaji wa vituo vya ubunifu bado ni mkubwa na watu wengi hasa wa vijijini hawajafaidika kikamilifu na kazi za ubunifu.
Ripoti ya utafiti wa mtawanyiko wa vituo vya ubunifu Tanzania (A mapping of Tanzanian hubs and innovation spaces) iliyotolewa Novemba 2018 na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) unaeleza kuwa Tanzania ina vituo vya ubunifu 43 ambavyo vinapatikana katika mikoa tisa tu ya Tanzania bara huku Zanzibar ikiwa na vituo vinne tu.