Huawei yafungua kesi kupinga zuio la kuuza bidhaa zake Marekani
Serikali ya Marekani iliweka zuio hilo kwa kile ilichodai kuwa kampuni hiyo inatumiwa na China katika shughuli za intelejensia.
Viongozi wa kampuni ya Huawei wakielezea hadhma yao ya kupata ufafanuzi wa kikatiba kuhusu zuio la kuingiza bidhaa zake Marekani. Picha|Mtandao.
- Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama ya Plano, Texas ili kupata tafsiri ya kikatiba kuhusu zuio hilo.
- Serikali ya Marekani iliweka zuio hilo kwa kile ilichodai kuwa kampuni hiyo inatumiwa na China katika shughuli za intelejensia.
- Huawei imesema madai ya Marekani hayana ukweli wowote bali yanalenga kuzoofisha kampuni hiyo kufaidika na fursa za matandao wa 5G.
Kampuni ya simu ya Huawei imefungua kesi mahakamani kupinga Serikali ya Marekani kuzuia bidhaa zake kuingia katika nchi hiyo kwa madai kuwa zinanatumika na China kwa shughuli za intelejensia na upelelezi.
Katika taarifa iliyotolewa jana (Machi 7, 2019), Huawei imeeleza kuwa imefungua kesi hiyo katika mahakama ya wilaya ya Plano, Texas nchini Marekani ili kupata ufafanuzi wa kisheria kutokana na taasisi za Serikali kuzuiwa kununua vifaa, huduma au kufanya kazi na wateja wa Huawei.
Hatua hiyo ya Huawei yenye makao makuu nchini China, inatoa ujumbe kwa dunia kuwa imepania kutumia njia zote ikiwemo mahakama za Taifa kuhakikisha inaingia kwenye soko la matumizi ya mtandao wa 5G ambao unatajwa kuwa utakuwa na kasi kubwa na mapinduzi makubwa ya teknolojia ya mawasiliano duniani.
“Bunge la Marekani mara kwa mara limeshindwa kutoa vithibitisho vinavyohalalisha zuio lake la bidhaa za Huawei. Tumejipanga kuchukua hatua hizi za kisheria kama njia sahihi na ya mwisho,” amesema Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Guo Ping.
Zuia la Marekani lilikuja baada ya China kutunga sheria ambayo inazilazimisha kampuni kuisaidia Serikali kwenye ulinzi wa Taifa.
Soma zaidi: Samsung, Huawei zinavyochuana katika soko la simu duniani
Kwa nyakati tofauti Huawei imesema madai ya Marekani hayana ukweli wowote bali yanalenga kuzoofisha kampuni hiyo kufaidika na fursa za matandao wa 5G.
Februari 24,2019, kampuni ya Huawei ilizindua simu mpya inayojikunja na yenye uwezo mkubwa ya Mate X ikiwa baada ya kupita siku tano tangu kampuni ya Samsung ilipotoa simu mpya za Galaxy S10 na toleo jijinge la simu ya kujikunja ya Galaxy Fold ambazo miongoni mwa sifa kubwa ni uwezo wa kuhifadhi taarifa nyingi hadi kiwango cha GB1,024.
Simu hiyo inatumia mtandao wa 5G ambao una kasi zaidi na unatajwa kuwa mapinduzi makubwa ya teknolojia ya mawasiliano duniani.
Hata hivyo, Huawei hawajaweka wazi ni wapi simu ya Mate X itauzwa, hata Marekani ambako inatumia teknolojia za viwango vya juu haijafahamika kama itafika.
Wiki cha zilizopita Rais wa Marekani Donald Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa anataka kuona mtandao wa intaneti wa 5G hata 6G unaanza kutumika mapema katika nchi hiyo na kuyataka makampuni kutobaki nyuma katika kuchangamkia fursa hiyo kwasababu mitandao hiyo ina kasi kubwa kuliko iliyopo sasa.