Simu benki inavyorahisisha matibabu kwa wanawake wenye fistula Tanzania
Mfumo huo hutumika kuwatumia waathirika wa ugonjwa huo pesa zinazokidhi mahitaji yao na usafiri mpaka kufika katika vituo vya afya kupata matibabu.
- Mfumo huo hutumika kuwatumia waathirika wa ugonjwa huo pesa zinazokidhi mahitaji yao na usafiri mpaka kufika katika vituo vya afya kupata matibabu.
- Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation na hospitali ya CCBRT kuendelea kushirikiana kuwapunguzia mzigo wa matibabu wanawake wenye fustula.
- Wanawake wenye ugonjwa huo watakiwa kujitokeza kupata matibabu.
Dar es Salaam. Sasa wanawake wenye fistula wameanza kupata ahueni kwa kupunguziwa gharama za usafiri na matibabu baada ya wabunifu kuanza kuwatambua na kuwawezesha kufika hospitali kwa kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
Shirika la Afya duniani (WHO) linakadiria kuwa wanawake 3,000 hupata tatizo la fistula kila mwaka nchini Tanzania hasa wakati wa kujifungua jambo linalohatarisha afya zao.
Taasisi ya Vodacom Tanzania Faundation kwa kushirikiana na hospitali ya CCBRT ya jijini hapa wametoa mafunzo kwa mabalozi 50 ya kuwatambua wanawake wenye fistula na kuwawezesha kufika hospitali kupata matibabu kwa kutumia mfumo wa Vodacom M-Pesa.
M-Pesa inatumika kuwatumia waathirika pesa ambazo zinakidhi mahitaji yao na usafiri mpaka kufika CCBRT au hospitali washirika kupata matibabu.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia amesema mpango huo wa mafunzo ulianzishwa na taasisi kama sehemu ya kuisaidia serikali kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Mabalozi hawa wanaungana na mabalozi wengine zaidi ya 3,000 wa fistula waliopo sehemu mbalimbali nchini, wenye uwezo wa kutambua na kuwawezesha waathirika wa Fistula kufika hospitali ya CCBRT au vituo vingine vya afya vinavyotoa matibabu hayo kama; Bugando (Mwanza), KCMC (Kilimanjaro), Nkinga (Tabora) na Selian (Arusha), kwa kutumia mfumo wa M-Pesa.
Mabalozi hao ametakiwa kutoa elimu kwa jamii zao kuhusu fistula kwa kuandaa semina ambazo zitaambatana na majadiliano ya changamoto mbalimbali zinazotokana na fistula.
Zinazohusiana:
- Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Wanawake wenye fistula wanakabiliana na changamoto ya kutengwa katika jamii zao na wengi wao hawatambui kama hali hii inatibika kutokana na ukosefu wa elimu na taarifa.
Utumiaji wa mabalozi wa Fistula ni hatua muhimu kwasababu wao hutumika katika kuwatambua na kuwapa rufaa wanawake wanaoishi na hali ya Fistula kwenda katika hospitali zilizobobea kutibu ugonjwa huo.
“Mwaka wa kwanza baada ya kuanza kutumia M-pesa kutoka Vodacom katika mfumo wetu wa rufaa tulishuhudia ongezeko la asilima 65 ya wanawake waliotibiwa ugonjwa wa fistula.
“Kufikia mwaka 2016, asilimia 87 ya wagonjwa wa fistula walipata rufaa kupitia mfumo wa M-Pesa ambao tunashirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, wakafanikiwa kufika CCBRT ambapo tulifanya upasuaji wa wagonjwa 1,012”, amesema Afisa Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi.
Msangi amesema fistula ni hali inayozuilika na kutibika na katika karne hii hakuna mwanamke anayestahili kutengwa au kunyanyapaliwa na jamii yake kwa sababu ya fistula.