November 24, 2024

Safari ya mwisho ya Google Plus

Watumiaji wapya hawawezi tena kupata fursa ya kujiunga na mtandao huo ili kutoa nafasi kwa kampuni ya Google kukamilisha mchakato wa kuufuta rasmi Aprili 2019.

Muonekano wa ukurasa wa Google+ ikiwa ni zimebaki siku chache kabla ya kufutwa kabisa April 2 mwaka huu. Picha|Daniel Mwingira.


  • Google+ imekosa ushawishi kwa watumiaji wake ambapo asilimia 90 ya wafuasi wake  walikuwa wanatumia sekunde tano kuingia na kutoka katika mtandao huo.
  • Google imesema kufikia Aprili mbili mwaka huu,  kurasa zote za Google+ zitaondolewa sambamba na maudhui yote zikiwemo picha, video na kumbukumbu zote za watu binafsi. 

Dar es Salaam. Kampuni ya Google imetangaza kuanzia leo (Februari 4, 2019) haitaruhusu mtu yeyote kufungua akaunti mpya katika mtandao wa Google+, ikiwa ni hatua za kukamilisha mchakato wa kuufuta kabisa mtandao huo ifikapo Aprili mwaka huu. 

Uamuzi kuifuta kabisa Google+ ulitangazwa mwishoni mwa mwaka 2018 huku sababu kubwa zilizotolewa na kampuni hiyo ya teknolojia duniani zinaeleza kuwa Google+ imekosa ushawishi kwa watumiaji wake ambapo asilimia 90 ya wafuasi wake  walikuwa wanatumia sekunde tano kuingia na kutoka katika mtandao huo. 

Kufutwa kwa mtandao wa Google+ ulioanzishwa mwaka 2011 kunafuata nyayo za huduma ya ‘Google Fusion’ ambayo nayo iko mbioni kuondolewa mwaka huu.    

Google imesema kufikia Aprili mbili mwaka huu,  kurasa zote za Google+ zitaondolewa sambamba na maudhui yote zikiwemo picha, video na kumbukumbu zote za watu binafsi. 

Hata hivyo watumiaji wa mtandao bado wana nafasi ya kuondoa taarifa na kumbukumbu muhimu katika mtandao huo kwa kufuata maelekezo yanayopatikana katika dawati la usaidizi la “Google+ Help Page’ kabla tarehe ya mwisho haijafika.

Kwa mujibu wa Google, maudhui mengine ya Google+ yataweza kupatikana kwa watumiaji wa mtandao wa kutunza nyaraka za G Suite.


Zinazohusiana: 


Duru za usalama mtandaoni zinaeleza kuwa sababu nyingine ya Google+ kufutwa ni kushindwa kudhibiti taarifa wa watumiaji zaidi ya 500,000 wa mtandao huo zilizodukuliwa na kuhatarisha usalama wao mtandaoni.  

Mdau wa  mitandao ya kijamii, Kenney Mmari amesema kuondoka kwa Google+ kunaweza kuwa na matokeo hasi kwa watumiaji waliopo katika maeneo mbalimbali duniani.  

Amesema Google+ ni mtandao wa kipekee uliowakutanisha watu wenye maono yanayofanana na kujenga mtandao wa mawasiliano ya kibiashara, kazi na taaluma, ambapo kufutwa kwake kutaondoa fursa hiyo ya kuwasiliana kwa urahisi.

“Unajua mtandao wa kijamii wa Google + ulikuwa kama Linkedlin sasa kufutwa kwake kutaondoa fursa kwa tabaka hilo la watu ambao tayari lilishajiwekea mtandao wao huko,” amesema Mmari

Pia amebainisha kuwa kundi lingine litakaloathirika ni lile la wachapishaji wa maudhui mtandaoni (Bloggers) ambao hawatapata nafasi ya kutumia Google+  kuandika na kusambaza maudhui kwa watu wengi.

Hata hivyo, kufutwa kwa mtandao huo ni fursa kwa kampuni zingine za teknolojia kubuni mtandao utakaowakutanisha watu pamoja kama WhatsApp na Facebook.