October 6, 2024

Teknolojia 4 zinazoangaziwa zaidi 2019

Ni zile zinatoa suluhisho la changamoto mbalimbali za jamii lakini zinahitaji kufanyiwa tafiti zaidi kuziongezea ufanisi.

  • Ni teknolojia zinatoa suluhisho la changamoto mbalimbali za jamii lakini zinahitaji kufanyiwa tafiti zaidi kuziongezea ufanisi.
  • Zinajumuisha ndege zisizokuwa na rubani, printa za 3D, upeo usio halisi na ‘virtual reality’. 
  • Zinachukua sehemu kubwa ya utendaji kazi wa binadamu ili kurahisisha shughuli za uzalishaji.
  • Pia zinaweza kuleta mgongano wa maslahi hasa katika soko la ushindani na ajira duniani.

Mwaka 2019, unaangaziwa kuwa ni mwaka wa matumizi ya teknolojia na uvumbuzi wa vitu vingi vitakavyochukua sehemu kubwa ya utendaji kazi wa binadamu ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na maisha. 

Hali hiyo huenda ikasababisha mgongano wa maslahi hasa katika soko ushindani na ajira duniani ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi zitakuwa zikifanywa na mashine.  

Nukta tunakuletea teknolojia nne ambazo wabunifu wanatazamia kuzitumia zaidi mwaka huu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo dunia inashuhudia. 


Ndege zisizokuwa na rubani (Drones)

Awali zilikuwa zinatumika katika shughuli za kijeshi zikiongozwa kwa kutumia rimoti na programu za kompyuta kwa ajili ya kushambulia kambi za maadui na kufanya uchunguzi katika maeneo ya mapigano.  

Ndege hizo za kisasa zimewekewa vifaa ambavyo  vina uwezo wa kukabiliana na hali ya hewa wakati wowote. Zina uwezo wa kujibadilisha  kutokana na eneo ambalo kunatarajiwa kutoa huduma ili kuleta matokeo chanya.

Lakini matumizi yake yamezifikia sekta nyingine kama kilimo hasa kuangalia maendeleo ya mashamba makubwa, kupima ardhi na kuchora ramani, ulinzi, kuokoa watu waliopata maafa yaliyopo mbali na huduma za jamii.

Pia sekta ya afya nayo haijaachwa nyuma hasa kusafirisha vifaa tiba na madawa. Lengo ni kupunguza kwa kiasi kikubwa muda unaotumiwa kutuma vifaa hivyo kwenye kliniki za afya katika mataifa ya Afrika kwa njia ya barabara na njia nyinginezo.

Mwishoni mwa mwaka 2018, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ya Tanzania ilianza kufanya majaribio ya usambazaji dawa katika visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani. Teknolojia hiyo ya kusambaza huduma za afya inatumia na nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo MalawiGhana na Rwanda. 

Ndege zisizokuwa na rubani zinasaidia kuinua huduma za kijamii hasa katika maeneo yenye miundombinu ya barabara. Picha| mydronelab.com

Printa ya 3D (3D Printer)

Ni printa ya kisasa inayotumika kuchapa vifaa vya maumbo mbalimbali  ambayo yanatumika katika shughuli za utoaji huduma na uzalishaji.  

Teknolojia hiyo ya machapisho ya pande tatu inahusika katika kubuni majengo, vifaa vya kufundishia watoto mashuleni, vifaa vya kusaidia kusikia na kutengeneza nyenzo kuwasaidia wanyama wenye ulemavu.

Printa ya 3D ina uwezo wa kutengeneza maumbo mbalimbali ya plastiki kulingana na ubunifu wa anayetumia mashine hiyo. Picha| Small Business Trends

‘Virtual Reality’ (VR)

Ni teknolojia nyingine inayohusisha kuvaa kisanduku kilicho na matundu mawili usawa wa macho. Matundu hayo yanakuwezesha kaangalia video, kucheza michezo mbalimbali kama ukiwa katika ulimwengu halisi. 

Kupitia VR unaweza ukatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kuvuka mito mikubwa, kuona majengo na fahari ya dunia. Kimsingi VR ni njia nyingine ya kuota ndoto zako kabla hujalala.Ili VR ifanye kazi inahitaji  kompyuta au simu yenye uwezo wa kuzalisha picha zinazoonekana katika kisanduku hicho. 

Mtandao wa Facebook wameifanya teknolojia hii kupata umaarufu mkubwa kwa kusambaza visanduku vya VR vijulikanavyo kama ‘Oculus’

Kampuni za Sonny, Google na Samsung nao wameungana na Facebook katika kuhakikisha teknolojia hiyo inasambaa duniani.


Zinazohusiana: 


Faida za VR zinagusa katika maeneo ya elimu, kufundishia wanafunzi masomo yanayohitaji mazoezi ya vitendo. Kwa wapenzi wa ‘games’ inawapa msisimko wa kushiriki mchezo husika vizuri na zinawasaidia wasanifu majengo kufahamu hali halisi ya eneo wanalofanyia kazi.

VR inakupa msisimko wa aina yake kwa kuona vitu halisi vinavyotokea duniani ukiwa umevaa kisanduku chenye matundu mawili. Picha| Oculus.

Kwa Tanzania teknolojia hii imeanza kutumiwa na kampuni inayochipukia ya Ona ambayo inajihusisha na utengenezaji wa video zenye uwezo wa kumuona mtu kama alivyo.

“Tumeanza kufanya hivi katika sekta ya habari na masimulizi ni teknolojia mpya na watu wengi wanahitaji kuifahamu japo kuna changamoto juu ya uzalishaji wake kwani inahitaji vifaa vyake binafsi katika hatua za mwisho za uzalishaji wa video” anaeleza Tulalana Bohela mwanzilishi wa Ona.


Teknolojia ya AI (Artificial Intelligence)

Hufahamika zaidi kama teknolojia ya ufahamu au nafsi (Upeo usio halisi) ya kutengenezwa inayotumiwa na mashine kwa msaada wa programu ya kompyuta ili kufanya kazi kama binadamu katika kutafakari na kutoa maamuzi ya mambo mbalimbali.

Utendaji kazi wa AI unahitaji sehemu ya kutunzia kumbukumbu, nguvu ya kompyuta ambayo inaunganishwa na intaneti na umeme ili kuipa nguvu ya kutekeleza majumuku yake.

Mfano wa AI ni roboti binadamu, Sophia aliyetengenezwa mwaka 2015 na kampuni ya Marekani ya Hanson Robotics yenye makazi yake Hong Kong, China. Sophia ana uwezo mkubwa wa kuzungumza na mwanadamu ambapo unaweza kuhisi anazungumza na kiumbe chenye nafsi.

Sophia amewahi kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed (kushoto). Picha| Face2Face Africa

Hata hivyo AI ina changamoto zake kwa sababu bado zinamuhitaji binadamu ili kukamilisha baadhi ya majukumu yake.

Wataalamu wa masuala ya teknolojia wanabainisha kuwa ikiwa mikakati ya uvumbuzi na ubunifu itaimarishwa mwaka huu, huenda ikasaidia kuchochea shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi ikiwemo kuwapunguzia wananchi umaskini hasa katika nchi za Afrika.