November 24, 2024

Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo

Hali hiyo imewakosesha fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta hiyo inayokua kwa kasi duniani.

  • Licha ya fursa nyingi zilizopo kwenye teknolojia bado ushiriki wa wanawake ni mdogo, jambo linalochelewesha utekelezaji wa ajenda za maendeleo.
  • Wadau wamesema msingi mbovu kuanzia ngazi ya chini ya familia unachangia wanawake kutoshikiri kikamilifu katika sekta ya teknolojia. 

Dar es Salaam. Kasi ya vijana wabunifu kuingia katika teknolojia inazidi kukua na kupelekea makampuni na mashirika mbalimbali uvumbuzi na utafiti kuwekeza katika sekta hiyo ili kutengeneza fursa zitakazowanufaisha vijana hao. 

Licha ya juhudi hizo, muitikio wa wanawake kushiriki katika shughuli za kuendeleza teknolojia umekuwa mdogo, jambo linaloweza kuichelewesha Tanzania kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ikiwemo kutoa elimu inayozingatia usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2030.   

Mtaalam wa programu za kompyuta kutoka kampuni ya Africa’s Talking, George Machibya anasema kukosekana kwa wanawake katika mikutano na makundi yanayowakutanisha wataalam wa mifumo na programu za kompyuta nchini ya “Google Developer Groups” (GDG) kunawakosesha fursa nyingi ambazo zinaweza kuwatoa kimaisha.

“Ushiriki wa wanawake ni mdogo katika haya matamasha ya GDG na wanakosa fursa nyingi sana kwa ajili yao,” amesema Machibya.

Kimsingi GDG ni jukwaa muhimu ambalo huratibiwa na vituo vya kijamii vya ubunifu kama Bun Hub kwa kushirikiana na kampuni ya Google ambayo hutoa msaada wa kifedha, ujuzi na maarifa kwa vijana wenye nia ya kuleta mabadiliko katika jamii kwa kutumia teknolojia rahisi.  

Machibya amesema wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuwavutia wanawake kushiriki katika majukwaa ya teknolojia ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa na vijana wanafaidika na fursa zinazojitkeza katika jamii.  

“Ukiondoa GDG, sisi huwa tuna hadi mikutano kwa ajili ya wasichana tu kwenye mambo ya teknolojia ila bado upokeaji ni mdogo,” amesema Machibya.


Zinazohusiana:


Matamasha  ya GDG maarufu GDG DevFest hufanyika sehemu mbalimbali duniani ambapo kwa Tanzania inatarajiwa kufanyika Novemba 17, 2018 katika kituo cha Buni Hub kilichopo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Ikiwa ni mwendelezo wa mikutano mingine iliyofanyika awali.

“Kupitia GDG  nimefanikiwa kupata kazi, hivyo vijana wajitoe na washiriki cha muhimu wawe na mawazo makubwa ambayo wakipata nafasi yatawalipa,” amesisitiza Machibya. 

Hata hivyo, Machibya ameeleza kuwa kushiriki kwenye mikutano ya GDG kwa watalaam wa programu za kompyuta ni nyenzo muhimu kwa vijana wa kitanzania  kujiendeleza zaidi katika sekta hiyo ikiwemo wanawake ambao hujiweka nyuma kwenye ushiriki.

Wanawake wakiwezeshwa katika teknolojia itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo nchini. Picha| WAAW Foundation

Ukiondoa kupata kazi kwa kushiriki mikutano kama hii, wabunifu wanaweza kupata mdhamini wa kuwasaidia kuendeleza miradi ya kibunifu inayolenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii inayowazunguka.

Georgia Rwechungura, mmoja wa viongozi wa GDG Dar es Salaam amesema bado kuna changamoto ya wanawake kutoshiriki katika shughuli za teknolojia inaanzia katika ngazi ya chini ya elimu ambapo ni wasichana wachache wanasoma masomo ya sayansi jambo linaloathiri hata wakifika katika ngazi za juu.

“Tatizo ni kuanzia chini, O level wasichana wengi hawasomi masomo ya sayansi lakini wengine wanasoma sayansi wanafanya kazi nyingine,” amesema Georgia ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache wanaanda matamasha mbalimbali ya teknolojia nchini.

Amebainisha kuwa wanaendelea kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuwashawishi wanawake wengi kuingia kwenye teknolojia ili wawe sehemu ya kuleta maendeleo katika jamii.

“Wazungumzaji wa siku ya GDG tumewaalika wanawake na watatu wamekubali kushiriki huku na mimi nitashriki pia katika mazungumzo,” amesema Georgia.