November 24, 2024

Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G

Kupoteza muda mrefu kwa kupakua vitu kwenye mtandao itakuwa historia kwa wengine.

  • Mtandao wa 5G unatarajiwa kuwa wenye kasi zaidi kuwahi kutokea.
  • Kampuni ya simu yajipanga kutengeneza simu zenye kuendana na kasi ya 5G.
  • Kutumia muda mwingi kupakua vitu kwenye mtandao itakuwa historia.

Inawezekana  unatumia muda mwingi katika kupakua vitu katika mtandao, lakini itakuwa historia kwa sababu mkombozi mpya wa mtandao amegunduliwa na atafanya kazi kwa kasi ya kubwa kuliko mtandao wa 3G na 4G iliyopo sasa.

Mkombozi huyo ni mtandao wa intaneti wa 5G ambao mwendelezo wa tano wa utumiaji wa mifumo ya simu bila kutumia waya, kwa simu na vifaa vingine huku ukiwa huna haja ya kuweka kifaa chochote katika ukuta wa ofisi au nyumbani na inaweza kuchukua nafasi ya WiFi.

Kwa mujibu wa kampuni ya Samsung, Mtandao huo wa  5G utakuwezesha kupakua GB moja kwa sekunde (1GB/Sec) lakini inakadiriwa kupakua GB 10 kwa sekunde na baadaye itakuwa na uwezo wa kupakua GB 800 kwa sekunde.

Pia utaweza kupakua filamu yenye uwezo wa HD ndani ya sekunde moja tu, vilevile kuweka programu na kuboresha progamu katika kompyuta itakuwa haraka na rahisi kuliko ilivyo sasa.

“Itakuwa nzuri sana hasa kwa tunaopenda kupakua vitu kwa haraka katika mtandao,” anasema Hafidhi Mketto ambaye ni mdau mkubwa wa kutumia mtandao. 

Mpaka sasa mtandao wa 5G uko kwenye majaribio na ukikamilika utaboresha huduma za mtandao  ikiwa sehemu ya kuchagiza shughuli za maendeleo kwa kasi zaidi. 


Je, 5G inamaanisha nini kwa mtumiaji?

5G ni njia rahisi na ya haraka ya kupakua na kuweka vitu mtandaoni. Utaweza kuangalia video na kusikia sauti yenye kiwango kizuri pasipo kukwama kwama kwa video au sauti hizo kwenye simu au kompyuta yako.   

Itapanua uwanja wa matumizi ya teknolojia hasa kwa wale wanaotumia mtandao kuendesha vyombo vya usafiri katika miji mikubwa duniani.

Ni mtandao wa kuaminika na kutegemewa katika simu za mkononi kutokana na kuwa rahisi katika kuunganisha na ni njia rahisi ya kuunganisha vifaa vya IoT ambavyo ni vifaa vinavyotuma data kwenda katika mtandao bila kuhusisha binadamu kwa binadamu au binadamu na kompyuta.


Lakini watumiaji watatoboa mifuko…

Kila teknolojia ina gharama zake, mtu atakayekubali huduma hiyo atalazimika kununua simu yenye uwezo wa 5G, hii ni kutokana na simu na vifaa vingi vinavyotumika sasa vimeunganishwa na mfumo wa 3G na 4G.

“Hapo kwenye kununua simu nyingine ndiyo shida ila kama watu tuliweza kutoka 3G hadi 4G hakuna kitakacho shindikana,” anasema Sabrina Shamte, mwanafunzi wa Chuo cha Biashara kampusi ya Mwanza (CBE) ambaye ni mtumiaji wa simu janja.

Katika kukabiliana na ushindani wa soko na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, makampuni mbalimbali yameanza kutengeneza vifaa vya elektroniki vinavyoendana na mfumo wa 5G.

Kampuni ya Huawei imekuwa ya kwanza duniani kumaliza majaribio ya 5G, na wamemtunuku zawadi, Dk Erdal Arikan; Mgunduzi wa ‘Polar Codes’ – mfumo wa unaosaidia utendaji na ufanisi wa mtandao wa 5G.

“Kuzaliwa kwa 5G ni mwanzo wa safari nyingine,” amesema Eric Xu, Mwenyekiti wa kampuni ya Huawei.  

Teknolojia ya 5G inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwaka 2020 duniani kote, huku nchi kama Marekani, China na Korea ya Kusini zinatarajiwa kuwa za kwanza kutumia mfumo huo katika nchi zao.