November 24, 2024

Wabuni teknolojia kuzuia kelele zinazokunyima usingizi

Kimbilio kwa wanaoishi karibu na kumbi za starehe, nyumba za ibada.

  • Ni kifaa maalum cha kuweka masikioni kinachozuia kelele za nje ukiwa usingizini.
  • Kimbilio kwa wale wanaoishi karibu na kumbi za starehe, nyumba za ibada. 

Huenda wewe ni mmoja watu ambao wanaishi karibu na maeneo  yenye kelele nyingi kama kumbi za starehe, baa au nyumba za ibada ambazo wanapiga muziki wakati wa usiku. Au unaishi nyumba ya kupanga ambayo wapangaji wenzako wana tabia ya kutumia sauti ya juu ya redio zao. 

Hali hii pia huenda inakupata wewe ambaye una mwenza ambaye anatoa sauti kubwa (anakoroma) mkiwa mmelala. Kelele hizo zote zimekuwa zikikukera hata kukunyima usingizi katika muda ambao unahitaji kupumzika baada ya shughuli nyingi za siku nzima. 

Pamoja na usumbufu wote huo, umeishia tu kulaumu bila kuchukua hatua yoyote. Usijali hauko peke yako, tatizo hilo linawakumba watu wengi duniani. 

Lakini sasa una kila sababu ya kutabasamu kwasababu kila changamoto ina majibu yake hasa katika ulimwengu huu ambao kila siku wabunifu wanaibuka na njia rahisi ya kurahisisha maisha bila kugombana na watu. 

Huko nchini Uingereza, kampuni ya vifaa vya elektroniki ya Flare imebuni kifaa kidogo kinachojulikana kama Sleep ambacho unakiweka masikioni wakati wa kulala ili kuzuia kelele zozote kutoka nje. 

Flare ambayo inajishughulisha na utafiti, utengenezaji wa vifaa vya muziki, inaeleza katika taarifa yake kuwa kifaa cha ‘Sleep’ kimetengenezwa kwa ustadi mkubwa wa malighafi za chuma na plastiki na kukufanya usisikie sauti pindi utakapokiweka kwenye masikioni tofauti na viziba masikio vya kawaida.

Usingizi wa uhakika ni afya, ili ukamilike unahitaji mazingira tulivu. Picha| blogs.dal.ca

Wabunifu wa kifaa hicho wamekitengeneza kwa aina mbili yaani ‘Sleeep yenye ya asili ya madini ya aluminiumu na fedha; hiki ni maalumu katika kuzuia kama sio kupunguza sauti zote ukiwa umelala.

Aina ya pili ni ‘Sleeep PRO’ kilichotengenezwa na madini ya titani (Titanium) maalum kwa kupunguza nguvu ya  mawimbi ya sauti. Pia inasaidia kuzuia sauti za mtu anayekoroma na kukufanya upate usingizi mwanana na kumka ukiwa mchangamfu. 

Kuvipata vifaa hivyo muhimu kukuhakishia afya na usalama wa masikio yako, utalazimika utoboe kidogo mfuko wako. Sleep Aluminium utaipata kwa Sh 88,000 huku ‘Sleeep PRO’ ni Sh 146,000 kwa kununua moja kwa moja kupitia mtandao.

Hata hivyo, chaguo linabaki kwako kwamba uendelee kusumbiliwa na kelele za usiku ambazo zinaweza kukuletea matatizo ya kusikia au kutumia teknolojia kufurahia usingizi kupumzisha akili.