November 24, 2024

Teknolojia ya utengenezaji mkaa mbadala inavyoweza kupunguza ukataji miti ovyo

Mkaa mbadala unaokoa kiasi kikubwa cha matumizi ya pesa kuliko mkaa wa kawaida.

  • Vifuu vya nazi, masuke ya mpunga, mimea mikavu, unga wa muhogo ni malighafi muhimu za utengenezaji mkaa mbadala.
  • Mkaa huo umekuwa kimbilio pekee la kupunguza uharibifu wa mazingira wa ukataji miti ovyo.
  • Mkaa mbadala unaokoa kiasi kikubwa cha matumizi ya pesa kuliko mkaa wa kawaida.

Dar es Salaam. Muhogo umekuwa na tija kubwa katika maisha ya binadamu hii ni kwasababu linadhihirisha matumizi mengi kwa wakati mmoja. Watu wengi wamezoea kutumia majani ya kisamvu kama mboga, mizizi ambayo ndio mihogo yenyewe nayotumika katika matumizi ya chakula kwa kukaanga, kuchemsha au kuipika kama futari.

Hata hivyo, ni wachache wanaojua matumizi ya unga wa muhogo katika utengenezaji wa mkaa mbadala unaotoa nishati bora ya kupikia na inayodumu kwa muda mrefu kuliko mkaa unaozalishwa na miti.

Unga wa muhogo unavyotumika kuzalisha mkaa mbadala 

“Unga wa muhogo, unapikwa kama uji na unatumika kama gundi yakuchanganyia na unga wa malighafi nyingine ili ziwe uji mzito unaopelekea uzalishaji wa mkaa mbadala hapa kiwandani,” anasema Abdullatifu Juma ambaye ni mfanyakazi katika kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala cha Charcoal Briquettes kilichopo Salasala jijini Dar es Salaam. 

Ukiondoa muhogo malighafi nyingine katika kutengeneza mkaa mbadala ni pamoja na vifuu vya nazi, mabaki ya mashambani na majani ambayo huunguzwa na kusagwa katika mashine.
“Malighafi zetu tunazipata kutoka Kibaha na Bagamoyo, tunawapa watu elimu jinsi ya kuchoma na baada ya hapo wanatuletea kwa kutuuzia kwa kilo,” anaeleza Shaban Waziri, Msimamizi wa Uzalishaji wa mkaa mbadala kiwandani hapo.

Ili kutengeneza mkaa huo, malighafi hizo zinazohusisha vifuu vya nazi, mabua na masuke ya mimea hupimwa katika hatua za awali na kusagwasagwa katika mashine na baada ya hapo hupimwa tena na kuingizwa katika mashine nyingine kwa ajili kuchanganya na uji wa muhogo.

Uji huo wa muhogo nao hupimwa kulingana na idadi ya kilo za malighafi zilizopimwa hapo awali. Mchanganyiko ambao huzalishwa katika hatua hiyo hupelekwa kwenye mashine ya kuzalisha mkaa na baada ya hapo huanikwa juani ili kuukausha vyema.Ili kuhakikisha hauharibiki katika mchakato wa usafirishaji, mkaa huo huwekwa kwenye viroba vya kilogramu 25 na kufungwa tayari kwa matumizi ya kupikia.

Hata hivyo malighafi muhimu katika utengenezaji wa mkaa huu ni uji wa muhogo kwasababu unafanya kazi kama ya maji katika kuchanganya mchanga na kokoto ili kupata zege.
Mkaa huo unaotengenezwa na kampuni mama ya ARTI Energy Tanzania ulianza kuzalishwa mwaka 2014 ikiwa ni moja ya njia za kuhamasisha kutunza mazingira kwa kutumia mimea mikavu na nishati mbadala.

 “Tulikuwa tunatoa elimu ya kutumia mimea mikavu kuzalisha nishati mbadala kwa watu tangu mwaka 2008 lakini tukawa hatuna mkaa wa kuwaonyeshea hapo ndo wazo la kiwanda cha Mkaa mkombozi lilipoanza,” anasema Abdalla Seushi, Ofisa Mauzo wa ARTI Energy Tanzania.

Kampuni hiyo ya Mkaa Mkombozi ambayo inatoa ajira kwa takribani watu 33 kiwandani hapo na wanazalisha karibu tani 4 kwa siku, hii inaonyesha kuwa kunahitajika viwanda vingi zaidi ili kuweza kukidhi soko la mkaa jijini Dar es Salaam inayotumia karibu tani 500,000 za mkaa wa kawaida kwa mwaka.

Walengwa wakuu wa nishati hii ya Mkaa Mkombozi ni kina nani?
“Tulifanya tafiti tukagundua Dar es Salaam zinaingia karibu tani laki tano za mkaa wa kawaida na wateja wakuu ni vyuo vikuu, shule zinazopika shuleni, wafugaji wa kuku, hoteli na mabaa na watu wa kawaida ni wachache sana,” anaeleza Seushi na kuongeza;

“Hivyo tumejikita sana katika kutafuta soko maeneo haya ambapo tunawauzia kwa bei ya kawaida kabisa ambayo kwa jumla kutoka hapa kiwandani tunauza elfu 15 kwa gunia la KG 25 ili waweze kununua na kuwavutia  waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida.”

Wauzaji na watumiaji wa mkaa wana maoni gani?

“Mimi nauza kiroba cha Mkaa Mkomboz Kilogramu 25 kwa wauza chips nawauzia kwa Sh19,000, na ni wauza wa chips wakubwa naweza kumuuzia viroba viwili akakaa nao kwa siku mbili na anatumia gharama ndogo sana ukilinganisha na kutumia mkaa wa kawaida,” anasema Beatrice Sawe muuza duka na wakala wa Mkaa Mkombozi Goba.
“Nilikuwa mbishi kutumia lakini kwa sasa nashukuru nilikuwa mwanzo natumia kwa siku hata Sh50,000 lakini kwasasa natumia Sh30,000 kwa siku, na mkaa pia unadumu kwa muda mrefu,” anaeleza Nastoli Benjamin muuza chips Goba.

Hata hivyo Nastoli aliiambia Nukta kuwa anatoa wito kwa wauza chips na watumiaji wengine kutumia mkaa mbadala ilikuweza kuokoa pesa nyingi inayotumika katika kununua mkaa wa kawaida ili kutunza mazingira.
“Watanzania tuache ubishi na tuanze kutumia nishati hii mbadala kama huu Mkaa Mkombozi ili tuweze kuokoa pesa na kutunza mazingira,” anamalizia Nastol.

“Mkaa  huu ni mzuri na unaokoa sana pesa hasa kwa sisi akina mama kwasababu unatumia kwa  muda mrefu kwa gharama ndogo, nawashauri wanawake wenzangu watumie mkaa mbadala waachane na mkaa wa kawaida, ukinunua Mkaa Mkombozi wa kilo nne ambao ni Sh3,500 unakaa nao wiki nzima” anasema Jennifer Charles ambaye ni mkazi wa Salasala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2016 zinaonyesha kuwa asilimia 88.2 ya kaya za jiji la Dar es Salaam zinatumia mkaa kama nishati huku asilimia 94.3 ya kaya za Simiyu zinatumia kuni, jambo linaashiria kuwa huenda miti mingi inakatwa kwa ajili ya nishati na kuchangia uharibifu wa mazingira.


       
 
“Asilimia 70 hadi 80 ya miti mikubwa inayokatwa nchini inatumika kutengenza mkaa, lazima tujifikirie kama nchi kuwapa watu wetunishati mbadala ili kupunguza matumizi ya mkaa” anasema Januari Makamba waziri mwenye dhamana ya Mazingira.

Wasanii na wadau wengine wa mazingira wanajitahidi kutoa elimu ya kutumia nishati mbadala ili kuyatunza mazingira msanii Beka Flavour ambaye ni msanii wa mziki nchini Tanzania ametoa wimbo unaotoa wito kuhifadhi mazingira yote kuelimisha watu walinde mazingira.

.                         

Wadau wa mazingira pia wanachukua hatua ya kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miti na kutumia nishati mbadala katika mitandao ya jamii ili kufikisha ujumbe