July 8, 2024

Apple kuingiza sokoni gari la umeme 2023

Litatumia mfumo endeshi wa iOS kama ilivyo kwa simu za iPhone na kuleta ushindani kwa kampuni zinazotengeneza magari duniani.

  • Duru zinasema gari la kwanza litaingia sokoni mwaka 2023
  • Litatumia mfumo endeshi wa iOS kama ilivyo kwa simu za iPhone.
  • Wadau wasema hatua ya Apple inaongeza ushindani kwa kampuni za magari kuongeza ubunifu.

Dar es Salaam. Mafanikio katika safari ya ujasiriamali ni pamoja na kuvumbua na kutumia fursa mpya za soko ambalo linaweza kuleta faida kubwa katika biashara yako. 

Basi ya kampuni ya Marekani inayohusika kutengeneza simu za iPhone na vifaa vingine vya mawasiliano ikiwemo kompyuta, inatanua wigo wake wa kutengeneza bidhaa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Apple Insider imesema kampuni hiyo inakusudia kuingiza bidhaa nyingine ya gari mnamo mwaka 2023 litakalokuwa linatumia umeme na mfumo endeshi unaotumika na simu za iPhone wa iOS.

Mchakato huo ulianza mwaka 2014 ambapo kampuni hiyo iliwaza kuendeleza mfumo wao wa kielektroniki kwa kutengeneza bidhaa nyingine tofauti na vile vilivyozoeleka. 

Hii ni moja ya hatua kubwa kwa kampuni hiyo kwani wamehama kutoka utengenezaji wa vifaa vya mawasiliano kwenda kwenye utengenezaji wa chombo cha usafiri.

Apple wameingia ubia na baadhi ya makampuni ya magari ikiwemo ya  Lexus RX450h SUVs ili kufanya majaribio ya mfumo wa iOS utakaokuwa unatumika kwenye gari hilo.

Hata hivyo, Apple itakuwa na kibarua kigumu cha kuhimili ushindani, ikizingatiwa ziko kampuni ikiwemo ya Tesla ambazo zinatengeneza magari ya yanayotumia umeme, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya petroli na dizeli.


Zinazohusiana:


Mtaalam wa masuala ya teknolojia, Lusajo Mwalukama amesema hatua hii ni kubwa sana kwa kampuni hiyo kwani inaonyesha mapinduzi makubwa kwa kampuni hiyo katika nyanja mbalimbali kwenye sekta ya biashara.

“Wametoka kwenye simu kwenda kwenye magari. Maana yake ni kwamba wanaenda kuwa na washindani wengine kwenye biashara. Kampuni inakuwa kwa matumizi mazuri ya teknolojia waliyonayo,” amesema Lusajo.

Hata hivyo Apple bado hawajaamua jina rasmi litakalopewa gari hilo kati ya majina matatu waliyonayo sasa ya Apple.car, Apple.cars na Apple.auto.

Gari hilo linatarajiwa kutumia mfumo wa iOS. Picha | Mtandao.