November 24, 2024

Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania

Ni programu za simu zilizosheheni taarifa mbalimbali zinazofungua fursa zilizopo katika sekta ya kilimo nchini.

  • Ni programu za simu zilizosheheni taarifa mbalimbali zinazokufungulia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo nchini.
  • Zikitumika vizuri zinaweza kuongeza uzalishaji na soko la mazao ya kilimo.
  • Wadau wa kilimo wataka Apps ziendane na hali ya halisi ya wakulima wa Tanzania ambao wanakabiliwa na changamoto ya teknolojia duni. 

Dar es Salaam. Una mpango wa kuingia au tayari umeingia kwenye shughuli za kilimo? Lakini huna maarifa na taarifa za kutosha kuhusu mbegu, mazao, ardhi, pembejeo na teknolojia ya kisasa kukusaidia kuinua kilimo chako? Simu yako ya mkononi inaweza kukupa yote hayo kiganjani mwako.

Nukta inakuletea programu 10 za simu (Apps) ambazo zina taarifa muhimu za kilimo hapa nchini. Apps hizo unazipakua kwenye simu yako na popote utakapokwenda utaendelea kuelimika na maarifa unayoyahitaji.

1.Kilimo Bora Tanzania (Kilimo Bora Tanzania)

App ya kilimo ambayo inaelezea mbinu mbalimbali za kilimo cha mazao kuanzia hatua ya uchaguzi wa mbegu, jinsi ya kulima hadi kufikia hatua ya kuuza.

Faida ya kutumia App hiyo ni jinsi ilivyotengenezwa kuwa rafiki kulingana na uelewa wa mtu kuhusu kilimo, maana unaweza kujifunza mwenyewe kimyakimya huku ukijipanga na kujua fursa ya unachotaka kulima na ulime kwa wakati gani.

2.Kilimo Taarifa (Kilimo Taarifa

Ni kiungo muhimu kwa wakulima,wauza pembejeo, wataalam wa kilimo na watafiti ili kumsaidia mkulima kuweza kufanya kilimo bora na cha kisasa kulingana na eneo alipo.

“Lengo la Kilimo Taarifa ni kumpa taarifa mkulima jinsi ya uzalishaji, kuhudumia shamba mpaka upatikanaji wa masoko,” anasema Adam Andrew, mwazilishi wa App ya kilimo Taarifa.

Kilimo Taarifa imeenda mbali zaidi hadi kutumia mfumo wa ujumbe mfupi (USSD) kwenye simu, ambapo mkulima atapata nafasi ya kuuliza mambo mbalimbali ikiwemo njia sahihi za kulima na soko la mavuno yake. Huduma ya ujumbe mfupi wa maneno ama arafa inaweza hupatikana katika simu zote za kawaida maarufu kama ‘kitochi’ na zile simu janja ama rununu.

Hata hivyo, programu hiyo haijafanikiwa kukusanya taarifa nyingi za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini ili kumfikia mkulima mahali popote alipo.

3.Shamba Konnect (Shamba Konnect)

Ni tovuti inayowakutanisha wauzaji, wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali za kilimo.

Kupitia Shamba Konnect, ambayo inataka ujisajili ili kuingia katika mfumo huo wa kununua na kuuza bidhaa, mtumiaji amerahisishiwa kupata huduma ya manunuzi ya bidhaa za kilimo kwa kutumia simu au mtandao kuepuka muda wa kuzunguka kwenda sokoni kufuata bidhaa hizo.

Pia unaweza kufahamu bei za mazao mbalimbali na wapi zinapatikana lakini unaweza kuagiza na ukaletewa popote ulipo.

Kama zilivyo apps nyingine na huduma za mtandaoni, Shamba Konnect huwezi kutumia iwapo haujajisajili. 

4. Ninayo Sokoni (Ninayo

Ni jukwaa la wazi ambalo linatumiwa kuweka matangazo ya kilimo na bidhaa zake ili kuwaunganisha wakulima wa wanunuzi.

Jukwaa hilo la Ninayo linaruhusu kuweka tangazo la bure la kununua au kuuza bidhaa au mazao, ambapo mtumiaji atachagua “ninataka kuuza” katika ukurasa wa mwanzo na kujaza fomu, kisha kubofya “tangaza” na baada ya kumaliza kutangaza wanunuzi na wauzaji watawasiliana naye wakivutiwa na tangazo lake.

Faida ya jukwaa hilo ni kukuwezesha kuwasiliana na mkulima kwa ujumbe mfupi wa maneno au kumpigia simu. 

Hatua iliyosalia ya mauziano inafanywa nje ya mfumo baada ya wahusika kukubaliana bei na mchakato wa uwasilishaji bidhaa kupitia mawasiliano ya simu za mkononi. Miongoni mwa watumiaji wengi wa Ninayo wanaonekana katika mtandao huwa wanatoka katika mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Morogoro na Arusha.

Hata hivyo, kwa wakulima na wanunuzi wapenda apps, Ninayo haipo kwenye Android wala Apps Store hivyo watahitajika kufungua huduma hiyo kwenye kitafutishi (browser).

5. Kilimo Utabiri (Kilimo Utabiri)

App hii imetenegenezwa maalum kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kulingana na maeneo ya kilimo. Mkulima ataweza kufahamu mwenendo wa hali ya hewa katika eneo lake na kumpa nafasi ya kupanga aina ya mazao anayotakiwa kulima kwa wakati husika.

Katika App hiyo ukiondoa kuhusu utabiri wa hali ya hewa kuna sehemu ya habari ambayo inakutaarifu kinachoendelea katika sekta ya kilimo, na changamoto zilizopo kama wadudu wanaoweza kuhatarisha kilimo.

Hata hivyo, taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinatolewa kwa muda wa siku tatu ili mkulima aweze kujiandaa vizuri na hata kukiwa na dharura basi mkulima atatahadharishwa kwa ujumbe mfupi wa maneno. 

Hata hivyo, haijawa bayana iwapo TMA imeithibitisha app hiyo ama la. Nukta haikufanikiwa kuthibitisha hili kwa wakati.

Kwa wanaotaka taarifa za kina na za kila siku huenda Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ikawaongezea taarifa zaidi katika kipindi app hiyo haitoi taarifa.

Muonekano wa App ya Kilimo Utabiri mahususi kwa kutoa taarifa za hali ya hewa. Picha| Kilimo Utabiri.

 

6. Kilimo Smart (Kilimo Smart)

Hili ni jukwaa maalum kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimobiashara, ufugaji wa kisasa, manunuzi ya mazao na mifugo, ushauri kuhusu udongo, magonjwa ya mazao.

Ukiondoa elimu kuhusu kilimo na ufugaji, App hii inachambua taarifa kuhusu kilimo katika mikoa mbalimbali na kukufundisha jinsi ya kutengeneza mbolea za asili na matumizi yake katika kilimo.

Kupitia Kilimo Smart unaweza kuweka na kusoma maoni, kutazama video na kujifunza vitu vingi kuhusu kilimo katika simu yake. Ili kuitumia app hii ni lazima uwe na intaneti ya kutosha kutokana na uwezo wake wa kukusafanya na kutunza taarifa nyingi na zenye umuhimu katika sekta ya kilimo. Huwezi kuitumia app hii iwapo hauna intaneti imara.

7. Kilimo na Ufugaji (Kilimo na Ufugaji Blog App)

App hii ipo kwenye mfumo wa blogu ambayo inawasaidia vijana au wajasiriamali kujifunza jinsi ya kujiajirii kupitia fursa za kilimo na ufugaji. Ina watalaam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ambao watakupa elimu sahihi ya kilimo bora.

Hapo utajifunza kilimo cha kisasa cha ‘greenhouse’ ambacho kinatumia eneo dogo kupata mazao mengi yanayomuhakikishia mkulima soko la uhakika.

Hata hivyo changamoto ya App hii ni kuwepo kwa taarifa nyingi kwa wakati mmoja, jambo linaloweza kuchukua muda mrefu kupata taarifa anayotafuta.


Zinazohusiana: 


8. Ufugaji na Matibabu Vet (Ufugaji na Matibabu Vet)

Hii ni App maalum kwa wafugaji ambayo inaelekeza njia za kisasa za kufuga mifugo mbalimbali na kupata faida iliyokusudiwa. Pia, mfugaji anafundishwa njia za kutengeneza vyakula vya mifugo, kujenga mabanda ya mifugo, dawa za mifugo na jinsi gani unavyoweza kuongeza soko na biashara ya ufugaji. 

Pamoja na huduma hiyo, unashauriwa kumuona daktari wa mifugo iwapo hujaelewa baadhi ya magonjwa yanayoisumbua mifugo yako. 

Kwa wanaotaka kujifunza njia za kudhibiti magonjwa ya wanyama na mazao, App ya Ufugaji na Matibabu Vet inaweza kuwa sahihi. Picha| Ufugaji na Matibabu Vet

9.Kilimo na Ufugaji (Kilimo na ufugaji by Farmers)

Ni maalum kwaajili ya soko la kuwezesha mazao ya kilimo kupatikana kirahisi mahali popote ulipo ambapo inatoa fursa kwa vijana kutumia mtandao kujiingizia kipato na kuondokana na umasikini.

Licha ya kuwa na uchaguzi wa taarifa mbalimbali, lakini utakutana na matangazo mengi yanayoweza kukutoa katika lengo la kupata unachotafuta. Matangazo lukuki ambayo haijapangwa vyema yanachelewesha mtumiaji kupata taarifa anazozitaka kwa haraka. 

10. Ufugaji (Ufugaji)

App hii imeandaliwa kwa ajili ya wanaopenda kujifunza ufugaji bora wa mifugo au wanaopenda kuboresha ufugaji. Inatoa elimu ya mifugo yote inayofugwa sehemu mbalimbali duniani.

Kupitia app hii utajifunza mbinu mbalimbali za ufugaji na namna ya kukabiliana na changamoto za ufugaji ikiwemo magonjwa. Kama zilivyo app nyingine za kilimo nchini, inatoa huduma bure kwa watumiaji wake.

Apps hizo zina maana gani kwa wakulima wa Tanzania?

Pamoja na uwepo wa huduma hizo nyingi kuhusu kilimo bado swali linabaki kuwa kiasi gani zinaendana na hali ya wakulima wadogo ambao wanakabiliwa na changamoto za teknolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za kilimo? 

Mkulima wa kilimobiashara kutoka Wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani, David Shao ameiambia Nukta kuwa licha ya apps hizo kusaidia wakulima lakini bado wanahitaji kufanya tafiti zaidi. Hii ni kutokana na kutokuwepo kwa maelezo sahihi hasa kwenye aina za udongo na hali ya hewa ya mahali alipo mkulima.

“Nyingi hazina uhalisia, ambazo ukifuatilia zaidi hazina ukweli, mfano utakuta wanakwambia papai usimwagie maji mengi lakini hawasemi kwenye udongo gani,” anasema Shao.

Baadhi ya wataalam wa mifumo ya kampyuta wanasema wanaoleta njia za kutatua matatizo katika sekta ya kilimo waangalie hadi wakulima wa chini ambao hawafikiwi mtandao wa intaneti na wasiomiliki simu janja.

“Kama huduma za kibenki zinapatikana bila kutumia intaneti basi wana uwezo wa kurahisha apps zao ziweze kuwafikia watu wanatumia simu za aina zote,” anasema Joshua Mabino, mtaalam wa programu za kompyuta Jijini Dar es Salaam.

Wadau wengine wanashauri nguvu ielekezwe katika kutoa elimu kwa wakulima hasa namna gani teknolojia itawasaidia kuongeza uzalishaji na kuwahakikishia masoko ya uhakika kwa mazao yao.  

Mjasiriamali wa mazao ya biashara kutoka kampuni ya JAYMAR ya mkoani Songea, Damian James anasema changamoto anayoiona ni kukosekana kwa huduma kwa wateja katika Apps hizo na hivyo kuwakosesha wakulima taarifa sahihi wanapozihitaji. 

“Watafute njia rafiki ya kufikiwa ikiwezekana hata kuwa na huduma kwa wateja ambapo mkulima anaweza kupiga simu wakati wowote,” anasema James.