October 7, 2024

Benki Kuu ya China mbioni kuzindua sarafu yake ya kidijitali

Ni hatua ya kupunguza gharama za kuzungusha pesa za kawaida na kuwawezesha watunga sera kudhibiti usambazaji wa pesa wa nchi hiyo.

Benki Kuu ya China (PBOC)  inakusudia kuzindua sarafu yake ya kidijitali. picha|Mtandao.


  • Ni hatua ya kupunguza gharama za kuzungusha pesa za kawaida na kuwawezesha watunga sera kudhibiti usambazaji wa pesa wa nchi hiyo. 
  • Utafiti wa matumizi ya sarafu hiyo ulianza mwaka 2014. 

Benki Kuu ya China (PBOC)  inakusudia kuzindua sarafu yake ya kidijitali baada ya miaka mitano ya utafiti, ikiwa ni hatua ya kupunguza gharama za kuzungusha pesa za kawaida na kuwawezesha watunga sera kudhibiti usambazaji wa pesa wa nchi hiyo. 

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malipo ya benki ya PBOC, Mu Changchun aliyekuwa akizungumza jumamosi (Agosti 10, 2019) katika mkutano uliofanyika katika jimbo la Kusini Mashariki mwa China la Heilongjiang, amesema utafiti huo ulianza mwaka 2014 ili kuangalia njia nzuri za kuanzisha sarafu hiyo na kuimarisha ufanisi wa benki hiyo. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa vimemnukuu Changchun kuwa sarafu hiyo itasaidia kupunguza gharama za benki hiyo katika usambazaji wa pesa za kawaida na kuwawezesha wateja wake kwenda kidijitali zaidi. 

Changchun amesema sarafu hiyo itakuwa inatolewa na benki ya PBOC pamoja na taasisi za fedha za nchi hiyo. 


Soma zaidi: 


Hata hivyo, sarafu hiyo ya kidijitali haitajikita moja kwa moja katika matumizi ya teknolojia ya ‘blockchain’ kwa sababu teknolojia hiyo haitaweza kufanikisha miamala yote ya fedha za China. 

Blockchain ni teknolojia ya mfumo unaomruhusu mtu kutuma au kuhifadhi vitu vyake zikiwemo nyaraka na pesa kwa njia ya mtandao bila kumuhusisha mtu mwingine (third party) au kupitia sehemu nyingine ambayo haihusiki.

Hivi karibuni, mtandao wa Facebook nao ulitangaza kuwa unakusudia kuzindua sarafu yake ya kidijitali ili kurahisisha malipo na manunuzi kwa watumiaji wake. 

Lakini hatua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti ambapo baadhi ya wataalam wa masuala ya fedha duniani wamesema inaweza kuvuruga mfumo wa kawaida wa taasisi za fedha hasa benki za kibiashara.