Boeing yaja kivinge kuzuia ajali ndege za 737 Max
Imetangaza kuzifanyia marekebisho ndege hizo ikiwemo kufunga mfumo wa onyo wa kuashiria ajali utaowasaidia marubani kupata taarifa mapema.
- Imetangaza kuzifanyia marekebisho ndege hizo ikiwemo kufunga mfumo wa onyo wa kuashiria ajali utaowasaidia marubani kupata taarifa mapema.
- Imebainika ndege za Ethiopia na Indonesia zilizopata ajali hazikuwa na mfumo wa kuashiria ajali.
Kampuni ya ndege ya Boeing imetangaza kuzifanyia marekebisho ndege aina ya Boeing 737 Max ikiwemo kufunga mfumo wa onyo wa kuashiria ajali, ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari za usalama kufuatia ndege za shirika la Ethiopia na Indonesia kupata ajali na kuua watu takriban 350.
Inaelezwa kuwa ndege zilizopata ajali hivi karibuni hazikuwa na mfumo wa kuashiria ajali ambapo marubani walikuwa hawapati taarifa wakati mtambo wa uongozaji wa safari za ndege unapotoa taarifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa Machi 27, 2019 inaeleza kuwa itafanya marekebisho katika mfumo wa MCAS (Maneuvering Characteristics Augmentation System) , ulioundwa kuzuia ndege kupoteza mwelekeo na unasaidia kutambua ndege kama iko kwenye mwinuko wa kasi isiyo ya kawaida.
Hata hivyo, taarifa ya Boeing imeeleza kuwa kubadilishwa kwa mfumo wa usalama wa ndege zake hakumaanishi kuwa mfumo uliokuwepo ulisababasiha ajali zilizotokea hivi karibuni.
Soma zaidi:
- Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus A380 Superjumbo
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa vimesema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na Boeing inatakiwa ithibitishwe na Shirika la safari za anga la Marekani (FAA) kufikia mwisho wa wiki.
Lakini FAA bado wanahoji kwa nini Boeing haikuweka vipengele vya kiusalama kwa ndege zake kubwa ambavyo vingesaidia kuzuia ajali hizo.
FAA imeeleza kuwa ndege zitakazowekewa mfumo huo wa MCAS zitatakiwa kutoa mrejesho juu ya utendaji wake na kuwapatia mafunzo marubani kabla ya mabadiliko hayo kuidhinishwa na ndege kufikia viwango vya kupaa tena.
Kampuni hiyo ya Marekani imesema itahakikisha inawapatia mafunzo ya utendaji wa mfumo huo wa MCAS marubani wote na kuzishirikisha kikamilifu mamlaka za usafiri wa anga za nchi hiyo ili ajali zisotokee tena.