November 24, 2024

CAG aisuta Costech matumizi mabaya ya fedha za wafadhili

Ripoti yake ya ukaguzi ya 2017/2018 inaeleza kuwa Tume hiyo ya Sayansi na Teknolojia haikuzingatia sheria na kanuni za manunuzi, kutotumia vizuri fedha za wafadhili katika baadhi ya miradi ya ubunifu na teknolojia.

  • Ripoti yake ya ukaguzi ya 2017/2018 inaeleza kuwa Tume hiyo ya Sayansi na Teknolojia haikuzingatia sheria na kanuni za manunuzi, kutotumia vizuri fedha za wafadhili katika baadhi ya miradi ya ubunifu na teknolojia.
  • Hali hiyo imesababisha wafadhili kurejesha fedha zao na kutoendelea kwa miradi kwa sababu ya kukosekana kwa fedha.
  • Yashauriwa kupitia upya tathmini ya miradi, manunuzi na kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Juma Mussa Assad amesema Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) imeshindwa kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi, kutotumia vizuri fedha za wafadhili katika baadhi ya miradi ya ubunifu, jambo linalorudisha nyuma jitihada za ukuzaji wa teknolojia na ujuzi nchini. 

Katika ripoti yake  ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kuhusu mashirika ya umma iliyotolewa jana (Aprili 10, 2019), Prof Assad amesema Benki ya Dunia ilitoa fedha kiasi cha Sh1.15 bilioni  kupitia Mradi wa Sayansi na Teknolojia Elimu ya Juu Tanzania (Tanzania Science and Technology Higher Education Project (STHEP)) ili kuongeza uwezo wa mtandao (bandwidth) mpaka kufikia STM 1 lakini tume hiyo ilikiuka sheria ya manunuzi na fedha za wafadhili zilirejeshwa.

“Mradi huu ulichukuliwa na Benki ya Dunia kuwa mradi wenye manunuzi yasiyofaa. Hii ni kutokana na kutozingatiwa kwa sheria na kanuni za manunuzi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kufuatilia ruhusa (no objection) toka benki hiyo wakati wa kutathmini zabuni,” inasomeka sehemu ya ripoti ya CAG.

Kutokana na mkanganyiko huo, Costech ililazimika kutumia kiasi cha Sh. bilioni 1.17 kutoka vyanzo vingine kilichokuwa kimepangwa kutekeleza miradi mingine. 

“Zaidi ya hayo, Dola za Kimarekani 716,207 (Sh1.6 bilioni) zilirejeshwa Benki ya Dunia moja kwa moja kutoka FDR kutokana na matatizo katika manunuzi,” inaeleza ripoti hiyo.


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, CAG amesema tume ilishindwa kutekeleza shughuli za kujenga uwezo zilizokuwa zimefadhiliwa na Benki ya Dunia katika kipindi kilichokuwa kimepangwa. 

Matokeo yake, kiasi cha Dola za Kimarekani 530,440 na 64,035 ikiwa sawa na Sh1.17 bilioni  na Sh140.88 milioni, mtawalia, zilirejeshwa Benki ya Dunia na SIDA (Shirika la Maendeleo la Sweden). 

“Ni maoni yangu kuwa haya yalisababishwa na mipango mibovu na uzembe katika kuzingatia matakwa ya makubaliano 171 na wafadhili. Hivyo, napendekeza Costech izingatie masharti ya fedha za wafadhali,” inaeleza ripoti hiyo.

Costech imekuwa sehemu muhimu ya kuendeleza ubunifu na teknolojia hasa kwa vijana wabunifu. Picha!Mtandao.

Pia imebainika kuwa Costech haifanyi tathmini ya umuhimu wa miradi na uwezo wa kuitekeleza kabla ya kutoa fedha, ambapo CAG alifanya mapitio katika miradi mitano yenye thamani ya Sh874 milioni nakubaini kuwa ilikuwa imekamilika bila kuwa na tathmini ya tija kwa miradi hiyo. 

Matokeo yake, miradi hiyo ilikosa uendelevu na haikuweza kufikia malengo yaliyotarajiwa. Miradi hiyo ni mradi wa viazi vitamu, kuongeza uzalishaji wa kuku kupitia chanjo ya kuthibiti magojwa ya mfumo wa hewa, utafiti wa kuboresha uzalishaji wa zao la muhogo. 

Miradi mingine ni utafiti wa kusaidia utumiaji wa njia mbadala ya kutunza misitu ili kuhuisha bustani za majumbani na kuzijaribu njia zilizobuniwa za kufanya ufugaji wa kijadi kuwa wa kibiashara katika miradi ya Tanzania.

“Nilibaini kuwa Costech haikuwa na kanzidata kwa aina za tafiti na miradi iliyofanywa, matokeo yaliyopatikana, mafundisho yaliyotokana na tafiti/miradi hiyo na kinachotakiwa kufanyika kwa kila utafiti au mradi uliotekelezwa ili kuwa na rejea imara kwa maamuzi na ushauri,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Kutokana na mapungufu yaliyojitokeza, CAG amependekeza kuwa Costech ihakikishe inazingatia kikamilifu masharti ya fedha za wafadhili ili kuwahamasisha kuendelea kufadhili miradi ya Tume na ihakikishe inafanya tathminni ya tija ya miradi na uendelevu wake kabla ya kuitekeleza ili kupata thamani ya fedha na faida kwa wananchi.

Pia kuanzishe na kutekeleza kanzidata kama nyenzo ya kupata na kutunza vizuri taarifa.