October 6, 2024

COSTECH yafungua milango kwa wabunifu kufaidika kiuchumi

Mbunifu awe na wazo linaloweza kutatua changamoto za jamii inayomzunguka

  • Mbunifu awe na wazo linaloweza kutatua changamoto za jamii inayomzunguka.
  • Watakaofanikiwa kupata Sh40 milioni kuendesha miradi yao.

Dar es salaam. Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) wanakusudia kuanzisha mradi kuwajengewa uwezo wajasiriamali kubuni miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi nchini.

Mradi huo uliopewa jina la “Fursa ya Kukuza Ubunifu” utawahusu wajasiriamali. wabunifu na watafiti, ambao watapatikana kupitia ushindani wa maandiko ya miradi inayolenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kupitia tafiti zinazolenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii. 

Wajasiriamali ambao mawazo yao yatakubalika watapata mitaji ya kuendesha shughuli zao ili kuboresha maisha ya jamii zinazowazunguka. Kigezo cha kupata ufadhili huo ni kuwa na mawazo ya kibunifu yaliyowekwa kwenye maandishi yakielezea tatizo, njia ya kutatua, matokeo tarajiwa, mgawanyo majukumu na ufanisi wa timu ya watu ambao watatekeleza wazo husika.

”Kusudio la ubunifu ni  kutoa msaada wa kifedha katika kuendeleza ubunifu ambao utachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa Tanzania,” inaeleza sehemu ya taarifa ya COSTECH ambayo inawataka wajasiriamali wenye nia ya kupata mtaji wawasilishe maandiko yao mpaka Septemba 9 mwaka huu. 

Watu ambao wanaweza kuingia kwenye mradi huo ni watu binafsi wenye mawazo ya mabadiliko, taasisi au mashirika yanayotengeneza bidhaa au kutumia teknolojia kuendeleza ubunifu katika jamii.  Wajasiriamali 15 ambao mawazo au maandiko yao yatathibitika kukidhi vigezo watapata ruzuku ya kuendesha miradi yao yenye thamani Sh40 milioni kwa kila mradi.

Mradi huo unakusudia kufanywa kwa mwaka mmoja ambao utagawanywa katika makundi matatu ya watafiti ambao wanatakiwa wawe wanne, wabunifu (4) na kundi la mwisho ni watafiti na wajasiriamali ambao watakuwa saba.

Utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya  jitihada za ndani na nje ya nchi zinazofanywa na mashirika mbalimbali katika kukuza ubunifu na ujasiriamali nchini katika sekta za afya, elimu, kilimo na teknolojia.