Dalili za Corona zilizotafutwa zaidi kwenye mtandao wa Google
Kupitia mtandao huo, watu wamekuwa wakitafuta vitu vingi kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) na zaidi kufahamu dalili za ugonjwa huo.
- Ni pamoja na dalili ya homa na uvimbe wa kwenye koo.
- Dalili zingine ni kukosa pumzi, kushindwa kung’amua harufu na ladha ya chakula.
- Viwango vya umaarufu zaidi kwenye utafutaji vimerekodiwa mwezi Machi ambapo ndio neno “Coronavirus” limetafutwa zaidi kwenye mtandao wa Google.
Dar es Salaam. Siyo kitu kigeni kwa watu kutembelea mtandao wa Google na kutafuta kitu fulani ili kujipatia ufahamu na maarifa mtandaoni.
Kupitia mtandao huo, watu wamekuwa wakitafuta vitu vingi kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) na zaidi kufahamu dalili za ugonjwa huo.
Kupitia king’amua mienendo ya utafutaji vitu katika mtandao huo kijulikanacho kama “Google Trends” hizi ni dalili za Covid-19 zilizotafutwa zaidi kwa miezi minne yaani kuanzia Januari 13, 2020 hadi Mei 8, 2020.
Dalili iliyotafutwa zaidi ni dalili ya homa ambayo ilitafutwa na watu wengi zaidi Machi 18 ambapo utafutwaji wake uligota kiwango cha juu zaidi kinachowakilishwa na namba 100 yenye maana ya umaaarufu zaidi siku hiyo.
Dalili ya pili kutafutwa zaidi katika kipindi hicho ni uvimbe wa kwenye sehemu ya koo (sore throat) ambayo ilitafutwa zaidi machi 17 ambapo kiasi cha umaarufu wake kimewakilishwa na namba 38 ambapo siku hiyo, dalili ya homa ilitafutwa kwa kiwango cha 96.
Rangi ya Kijani inaonyesha jjinsi watu walivyotafuta homa kama dalili ya ugonnjwa wa Covid-19. Zambarau inawakilisha uvimbe kwenye koo, Bluu inawakilisha shida ya upumuaji, Nyekundu inawakilisha kushindwa kung’amua ladha na Njano inaonyesha kushindwa kung’amua harufu. Picha| Google Trends.
Mbali na uvimbe kwenye sehemu ya koo, dalili ya tatu kutafutwa zaidi ni kukosa pumzi (shortness of breath) ambayo kiwango chake cha kutafutwa kilikuwa ni Machi 19, Machi 20 na Machi 24 ambapo kiwango cha umaarufu wake kipo kwenye namba 11.
Kingine kilichotafutwa zaidi ambayo ni dalili ya Covid-19 ni kutokupata ladha ya chakula (loss of taste) ambayo umaarufu wake umegota kwenye namba sita siku ya Machi 23.
Dalili ya mwisho kwa mujibu wa dalili tano zilizotolewa na Google Trends ni kushindwa kung’amua harufu (loss of smell) ambayo kiwango chake cha juu kimepimwa Machi 23 ambapo mzani wake umegota kwenye namba nane.
Zinazohusiana
- Jinsi ya kubaini picha zinazopotosha kuhusu Corona mtandaoni.
- Facebook yaendeleza vita ya Corona kupitia makundi
- Hapana! Waziri Ummy Mwalimu hajawahi kuambukizwa corona
Endapo umeangalia namba hizo vizuri, umaarufu wa dalili nyingi umegota kwenye mwezi Machi ambapo kwa mujibu wa kingamua mienendo cha Google Trends, Mwezi Machi ni mwezi ambao neno “Coronavirus” limetafutwa zaidi na kugota kiwango cha 100 kwenye umaarufu.
Ni vizuri kufahamu juu ya dalili za COVID-19 ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata tiba sahihii. Jambo la muhimu kulifanya baada ya kugundua kuwa una dalili za Corona ni kuwasiliana na mamlaka za afya ili usaidiwe.
Kumbuka siyo kila unazopata zinahusiana na ugonjwa wa Corona, wakati mwingine yanaweza maradhi mengine.
Ugonjwa wa Corona unazuilika endapo utachukua tahadhari ya kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kutokugusa pua, macho au mdomo na kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.