November 24, 2024

Epuka haya unapotumia simu yako ya mkononi

Wapo watu ambao wanatumia simu za mkononi kinyume na maelekezo yaliyotolewa na watengenezaji na hivyo kusababisha simu kuharibika mapema.

  • Ni pamoja na kushindwa kusasisha simu yako pale maboresho yanapokuwa yamefanyika.
  • Usitumie simu yako ikiwa kwenye chaji.
  • Kuitunza simu yako na kuiweka katika hali nzuri itaweza kudumu kwa muda mrefu.

Dar es Salaam. Huenda simu janja ni miongoni mwa vifaa vya kielektroniki zinazotumika zaidi na Watanzania baada ya chakula na mahitaji muhimu.

Hata hivyo, baadhi wamekuwa wakifanya makosa katika kutumia kifaa hicho ambacho ni muhimu kwa ajili ya mawasiliano na kumbukumbu.

Wapo watu ambao wanatumia simu za mkononi kinyume na maelekezo yaliyotolewa na watengenezaji na hivyo kusababisha simu kuharibika mapema.

Yafuatayo ni kati ya makosa ambayo baadhi hufanya wakati wanatumia simu zao za mkononi na ambayo yanatakiwa kuepukwa ili simu idumu muda mrefu:

Kuitumia simu yako wakati ikiwa kwenye chaji

Ni rahisi kusema watu wengi wamefungamana sana na simu zao kiasi cha kutaka kuitumia kila mara hata inapokuwa kwenye chaji.

Kitendo hicho siyo kizuri kwani utaisababishia simu yako kupata joto hasa endapo utakua unaitumia kufanya kazi katika programu zinazotumia chaji au intaneti kwa wingi.

Kwa mujibu wa tovuti ya teknolojia (Tekno Kona) unashauriwa kuiacha simu yako kwenye chaji hadi itakapokuwa tayari kwani kuitumia wakati inaingiza umeme inaweza kuwa sababu ya simu kuripuka na hivyo kukupa hasara na hata kukujeruhi.

Ni rahisi kusema watu wengi wamefungamana sana na simu zao kiasi cha kutaka kuitumia kila mara hata inapokuwa kwenye chaji. Picha| Rodgers  George.

Kutokuianzisha simu yako

Jambo hili huenda likawa ni tatizo la wengi. Kwa kuwa simu hutumika hata ikiwa kwenye chaji, na inapojaa inaendelea kutumika tena, huenda baadhi husahau kuizima au kuianzisha upya (restart) simu ili kupumzisha mfumo endeshi na kuupatia mwanzo mpya.

Inashauriwa kuianzisha upya simu yako walau mara moja au mbili kwa wiki. Kwa kufanya hivyo, utaisaidia simu yako kuwa na ufanisi mzuri.


Soma zaidi:


Kushindwa kuisasisha simu yako

Ni kawaida kwa watengeneza programu na kampuni za simu kutoa toleo jipya la mfumo endeshi na hata programu. Kwa wengine huona jambo hilo kama usumbufu kiasi cha kushindwa kuruhusu programu (apps) na mfumo endeshi kusasishwa.

Kwa mujibu wa mdau wa teknolojia jijini Dar es Salaam, Brian Mallya watengeneza programu hutoa matoleo mapya ya programu kwa sababu zinakuwa zimeboreshwa na kuongezewa ulinzi zidi ya wadukuzi na hata vitusi vya kiteknolojia.

Endapo utaacha kusasisha simu yako, unaweza kushindwa kutumia baadhi ya programu na kuiweka simu yako katika hati hati ya kuvamiwa na virusi vya kiteknolojia.

Yapo mengi ambayo unaweza kufanya ili kuipatia simu yako ufanisi ili idumu kwa muda mrefu. Mathalani, baadhi ya watu hufunga (clear) apps ambazo wamezitumia wakidhani kuwa wanaipumzisha simu.

Hata hivyo ukweli ni kuwa, App hutumia nguvu ya ziada kufunguka kwa mara ya kwanza na hivyo pale inapukuwa imefunguka na ukalazimika kufungua app nyingine, itakuwa rahisi kuipata endapo haujaifunga.

Nukta Habari (www.nukta.co.tz) hukuletea dondoo lukuki kuhusu simu za mkononi na teknolojia. Kusoma zaidi, bonyeza kipengele cha “Teknolojia” na ufurahie uchambuzi wa kina juu ya teknolojia mbali mbali kiganjani mwako.