November 24, 2024

Facebook kumzuia raia wa Ufaransa kurusha kifo chake mubashara

Ni Alain Cocq anayeugua ugonjwa usio na tiba nchini humo ambaye alitangaza uamuzi huo Jumamosi baada ya kuanza kukataa chakula na kumeza dawa.

Alain Cocq akiwa kitandani nyumbani kwake mjini Dijon ambapo ametangaza kuondoa uhai wake. Picha|RTL.fr.


  • Ni Alain Cocq ambaye anaugua ugonjwa usio na tiba nchini humo. 
  • Alitangaza uamuzi huo Jumamosi baada ya kuanza kukataa chakula na kumeza dawa.
  • Facebook yasema sheria zake haziruhusu matangazo mubashara ya watu kujitoa uhai. 

Facebook imesema itamzuia raia wa Ufaransa, Alain Cocq ambaye anaugua ugonjwa usio na tiba aliyepanga kurusha mubashara kifo chake kwenye mtandao huo. 

Cocq mwenye umri wa miaka 57 alipanga kurusha moja kwa moja maisha yake ya siku za mwisho baada ya kuanza kukataa chakula, kunywa chocchote na kumeza dawa siku ya Jumamosi Septemba 5, 2020.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mwanaume huyo anataka sheria ibadilishwe nchini Ufaransa ili kuruhusu watu walio kwenye maumivu makali kufa kama watakavyopenda. 

”Njia ya ukombozi inaanza na mini, nina furaha,” ameandika Cocq kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook siku ya Jumamosi akiwa kitandani nyumbani kwake mjini Dijon.

Akiwa kitandani hapo alitangaza kuwa ‘amemaliza mlo wake wa mwisho’ na anasubiri kifo tu. 

Imeelezwa na vyombo vya habari vya kimataifa kuwa Cocq ana ugonjwa ambao umeathiri tishu na viungo na kusababisha kuta za mishipa ya ateri kushikana.

Hata hivyo, Facebook imezuia Cocq kurusha moja kwa moja kifo chake na kubainisha kuwa hairuhusu kuonesha matukio ya kujitoa uhai.

”Ingawa tunaheshimu uamuzi wa Cocq kutokana na ushauri wa kitaalamu tumechukua hatua kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya suala la Alain,” amesema Msemaji wa Facebook wakati akihojiwa na shirika la habari nchini humo la AFP .

 ”Sheria zetu haziruhusu kuonesha majaribio ya kujikatisha uhai.”