October 6, 2024

Facebook yaandaa mpango wa kufanya kazi na vyombo vya habari duniani

Facebook ina mpango wa kuongeza kipengele cha utoaji wa habari mbalimbali ikiwemo teknolojia, biashara katika programu yake tumishi (App) ili kuwapatia watumuaji wake habari za uhakika kila wakati.

  • Inaanzisha kipengele kitakachowapa fursa wanahabari kutoa habari zao katika mtandao huo.
  • Lengo ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa habari za kweli na uhakika katika mtandao huo.
  • Wadau wasema mpango huo itaifadisha zaidi Facebook kwa kuongeza wafuasi na mapato. 

Kama wewe ni mtumiaji wa Facebook na bado umekuwa ukitafuta vyanzo vingine kupata habari zinazoendelea duniani hasa katika eneo lako. Basi mtandao huo umekuja na mabadiliko mapya ya kihabari. 

Facebook ina mpango wa kuongeza kipengele cha utoaji wa habari mbalimbali ikiwemo teknolojia, biashara katika programu yake tumishi (App) ili kuwapatia watumiaji wake habari za uhakika kila wakati. 

Kwa mpango huo, watumiaji wa mtandao huo watakua na uwezo wa kupata habari mbalimbali zinazoshika vichwa vya habari kwa muda maalumu katika maeneo mbalimbali duniani.

Katika taarifa iliyotolewa na mtandao wa Social Media Today inaeleza kuwa facebook itashirikiana na vyombo vya habari vya kimataifa kama Financial Times ili kuwahakikishia wasomaji taarifa za kweli na kuondoa mkanganyiko wa habari za uzushi (Fake News). 

Siyo kila chombo kitapata fursa, bali vile vilivyokidhi vigezo na masharti yatakayowekwa kuhakikisha mtandao huo unakuwa mahali salama kwa watu kupata taarifa ambazo hawazipati sehemu nyingine kirahisi.

Dhumuni kubwa la kuweka kipengele hicho, ni pamoja na kuongeza wasomaji na watumiaji wa mtandao huo, jambo litakalosaidia kuongeza wigo wa mapato na kupunguza changamoto za tuhuma mbalimbali zinazoikumba Facebook hasa katika usambazaji wa habari za uzushi. 


Zinazohusiana:


Huenda mabadiliko haya yanaweza yasiwe na maana kubwa kwa vyambo vya habari kwa sababu Facebook itapata wasomaji wengi kwa kutumia habari yavyombo labda kama msomaji akitaka kupata taarifa kwa kina anaweza kuingia kwenye tovuti ya chombo husika.

Mtaalam wa masuala ya teknolojia, Emmanuel Feruzi amesema mabadiliko haya yanayoletwa na baadhi ya kampuni za teknolojia kufanya kazi za vyombo vya habari ni kujaribu kuweka mazingira mazuri ya wao kuongeza wasomaji na kipato kwa kwampuni zao.

“Kwa asilimia kubwa watakaokuwa wanapata wasomaji wengi ni Facebook kwa sababu wao wanapata faida kwa matangazo na wasomaji, kwa maana hiyo mtandao huo unaelekea kuingiza faida kubwa baada ya mabadiliko hayo kuanza”, Amesema Feruzi.

Mpango huo wa Facebook ulianza tangu mwaka 2018 na wanatarajia kuanza kutekeleza mwaka huu.

Hata hivyo, mtandao huo hawajatoa taarifa kamili juu ya faida itakazopata chombo cha habari au mwanahabari atakayekuwa anaripoti katika mtandao huo unaokuwa kasi duniani. 

Kila mwezi watumiaji takribani bilioni 2.4 hutumia mtandao wa Facebook huku ukiwa ni jukwaa muhimu linalowakutanisha watu na wafanyabiashara kutangaza biashara zao.